The House of Favourite Newspapers

Ukiona Haya Kwa Mpenzi Wako, Jua Hakutaki!

MAPENZI wakati mwingine ni kama uchizi. Mwanadamu hujikuta anapoteza uwezo wake wa kufikiri kwa sababu tu ya nguvu ya mapenzi. Kwa ambaye hayupo penzini, ni vigumu sana kuelewa ‘uchizi’ wa mwenzake.

 

Ni kama vile shabiki wa mpira anavyokuwa akishangilia timu yake halafu wachezaji wake wakawa hawafanyi vizuri. Ni rahisi sana kusema, fulani amefanya makosa na kusababisha wafungwe. Anajiona yeye anaujua mpira kuliko wale wachezaji wa timu yake.

 

Ndugu zangu, utamu wa ngoma uingie kucheza. Anayecheza ndiye anayejua tamu na chungu ya ngoma, shabiki wewe huwezi kuelewa, kifupi ni kwamba mapenzi yanaumiza. Mapenzi yanasumbua mno vichwa vya watu.

Ndio maana kwenye ulimwengu wa leo, wapo watu wanateseka kwenye uhusiano kwa sababu tu ya kutokubaliana na ukweli. Anapewa usumbufu mkali kutoka kwa mwezi wake, dunia yote inamshangaa yeye lakini wapi bwana, anakomaa tu.

 

Moyo unakuwa umependa haukubali kuacha kirahisi. Moyo unasukumwa na nguvu ya ajabu ambayo mtu wa pembeni hawezi kuibaini. Sanasana atakuonea huruma tu na kukuona labda pengine umechanganyikiwa bila kujua ni mapenzi tu.

 

Unakuta mtu anakufukuza, anakuoneshea dhahiri kwamba hakutaki lakini wewe upo tu. Hakupokelei simu, hajibu ujumbe wowote ambao utamtumia. Ukikaa kimya wewe, kwake yeye ndiyo nt’olee. Hana habari na wewe. Anaendelea na maisha yake kama kawaida.

 

Anainjoi maisha na marafiki zake, kama kwamba hajawahi kukutana na mtu wa aina yako. Bahati mbaya sana, wakati huo yawezekana akawa hata na mpenzi wake mwingine. Wewe unabaki unahaha tu, unatesekea penzi lake. Hapa ndio pale zinaposikika zile kauli za ‘siwezi ishi bila yeye.’

 

Marafiki zangu, pamoja na moyo kupenda lakini kuna wakati inabidi uifanye akili yako ifanye kazi vizuri na kuweza kuutoa nishai ujinga wa moyo.

Sema na moyo wako kwamba kwa hapo ulipofikia inatosha na pengine uanze kuangalia ustarabu mwingine.

 

Kama mtu hana habari na wewe, haoneshi tena mapenzi na wewe unamng’ang’ania wa nini? Kwani umeambiwa mwanaume au mwanamke ni huyo tu? Mbona wapo wengi tu, unafikiri moyo wako uliumbwa kwa ajili ya huyo tu? Unajiongopea!

Maisha yapo tu, hakuna sababu ya kulia kila uchwao. Hakuna sababu ya kulia kwamba umepoteza muda mrefu na huyo aliyekuwa mtu wako. Jambo la msingi ni kushukuru Mungu kwa aliyokufanyia. Yawezekana kwa kipindi chote hicho alikufanya wa ziada.

 

Yawezekana kabisa hakuwa na mapenzi ya dhati na wewe hivyo hata ukiendelea kulazimisha, utaishia tu kuumia bila sababu za msingi. Ifike mahali useme inatosha. Kataa kuwa mtumwa wa mapenzi. Ruhusu akili yako iwaze vitu vingine tofauti na mahusiano.

 

Kaa mbali kabisa na mhusika. Tafuta furaha ya moyo wako kwa gharama yoyote. Anza kuzu-ngukwa na watu wataka-oingiza mambo mapya katika akili yako.

 

Mambo ambayo yata-kuondoa kabisa kwenye mawazo ya mapenzi.

Hata ikitokea umeanzisha tena uhusiano, kuwa makini sana na mtu ambaye unaingia naye. Usiruhusu kumpenda kabla hujamjua kiundani. Jiridhishe sana kabla ya kuruhusu moyo wako kuzama penzini.

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii. Instagram na Facebook natumia jina Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

 

 

Comments are closed.