The House of Favourite Newspapers

UKIONA MPENZI WAKO HAKUFUATILII, UJUE KUNA KINACHOENDELEA

0

ukiona mpenzi wako hakufuatilii

MPENZI msomaji ungana nami katika kumshukuru Mungu kwa nafasi aliyonijalia kuweza kuandika makala haya (ukiona mpenzi wako hakufuatilii…) ya XXLove katika Jumatatu hii njema kabisa.

 

Pongezi za pili zikufikie wewe msomaji popote ulipo kwa kuwa sehemu ya familia hii kubwa ya XXLove kwa kunitumia ushauri na maoni mbalimbali kuhusu mada zetu hapa jamvini. Mada ya leo inazungumzia maisha ndani ya mapenzi yaani ukiona mpenzi wako hakufuatilii ujue kuna kinachoendelea.

 

Kwa mfano upo kwenye uhusiano wa kimapenzi, uchumba au ndoa na mwenza wako kwa muda mrefu kidogo, yawezekana ni miezi sita, mwaka mmoja au miaka kadhaa. Katika muda wote huo, umekuwa ukikumbana na misukosuko ya kawaida ya kimapenzi ya hapa na pale.

 

Lakini katika hali kama hiyo, ghafla unashtuka kuona mambo yamebadilika na siyo kama zamani tena. Ukiona hivyo, basi ujue kuna jambo au kinachoendelea hivyo unatakiwa kushtuka. Mapenzi yanahitaji wivu wa dhati na wenye maana ya upendo kwa mwenza wako, ingawa wivu huo ukizidi sana huleta matatizo. Inawezekana ukawa unaona wivu wakati mwingine kwa kuhisi tu kuwa, mwenza wako anachepuka au ana uhusiano na f’lani. Kisa, umemuona akiongea au akiwa karibu zaidi na mtu huyo.

 

Kwa mtindo huo wa wivu uliopitiliza, unaweza ukajikuta hata ndugu zako ukiwaonea wivu. Ingawa wivu mwingi huwa kipindi kile cha utamu wa mapenzi yaani katika kipindi ambacho mapenzi yenu yakiwa motomoto, japokuwa hata ujazo wa wivu wenyewe hutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine. Mpenzi wako kuwa na wivu dhidi yako si jambo baya.

 

Ni jambo zuri linaloashiria anakupenda, anakuhitaji na bado anataka muendelee kuwa pamoja. Lakini inapofika sehemu baadhi ya tabia ambazo ulikuwa umezizoea kwa mpenzi au mwandani wako hazipo, basi fahamu kuna haya mambo yanaendelea:

 

MMEANZA KUKINAHIANA

Inawezekana kwa kuwa mko kwenye mapenzi kwa muda mrefu sasa umeanza kumkinahi au kwa lugha rahisi amepoteza mvuto kwako.

 

ANACHEPUKA AU MNACHEPUKA

Mtu mwingine anaweza akawa amemkinahi mwenza wake kisha akavumilia, lakini mwingine anaweza kutumia nafasi hiyo na kuanza kuchepuka. Hivyo unapoona mpenzi wako ameacha au amepunguza kukufuatilia, jitahidi kumchunguza kwa umakini mkubwa. Katika uchunguzi wako unaweza ukakuta amekuwa hakufuatilii kwa sababu amepata mchepuko ambao ufuatiliaji wake ameuhamishia huko.

 

MMEZOEANA

Wakati mwingine anaweza kuwa amepunguza kukufuatilia kwa sababu anakuamini, amekuzoea na anaona ni kweli huna tabia za ujanjaujanja kama ilivyokuwa awali. Pengine amekuzalisha au amekuzalia watoto ambao wanamfanya awe bize kuwafuatilia wao kuliko wewe.

 

AMECHOKA TU KUKUCHUNGUZA

Wakati mwingine mwenza wako anaweza kufika tu sehemu akachoka kukuchunguza na kukushauri kuhusu mwenendo wako. Kwa mfano, mume au mke alikuwa akipenda sana kufuatilia kila unapokwenda au kila unachokifanya au kuulizia muda utakaoenda kutumia sehemu husika. Au uhitaji kujua kwa undani kile ambacho umeenda kukifanya.

 

Unaweza kukuta awali mwenza wako alikuwa kila muda anapekua simu yako na sasa ameamua kukuacha na unajikuta na wewe unakuwa ‘free’ muda mwingi kuchati na kila unayemtaka. Kwa msomaji ambaye umeanza kukutana na mambo hayo niliyoyaorodhesha hapo juu, basi usitahamaki. Unachotakiwa kufanya ni masahihisho na penzi lako ili kulifanya kuwa jipya, kwa sababu ya muda mwingi wa kuwa kwenye uhusiano ni lazima mzoeane, lakini hampaswi kuwa kama kaka na dada au ndugu wa damu. Bali lazima muunganiko wenu wa mapenzi uendelee kama kawaida.

Ukiona mpenzi wako hakufuatilii, ujue kuna kinachoendelea…

GABRIEL NG’OSHA SIMU; +255 679 979 785

Leave A Reply