UKIPARAMIA PENZI LA USIYEMJUA, ANDIKA MAUMIVU!

NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia uwanja huu wa mahaba. Ni eneo pekee ambalo unaweza kujifunza mambo ambayo yanaweza kuboresha maisha yako ya kimahaba. 

Mpenzi msomaji wangu, juzikati nilikutana na rafiki yangu wa muda mrefu sana! Urafiki wetu ulianzia tangu tulipokuwa wadogo, tulicheza na kusoma pamoja hadi kumaliza elimu ya msingi na ndipo tukapotezana.

Aliniita nyumbani kwao kunitambulisha kwa mchumba wake ambaye walitarajia kufunga naye ndoa. Kwa bahati nzuri au mbaya, binti ambaye rafiki yangu huyo alitarajia kumuoa namfahamu.

Iko hivi, huyo binti anaishi karibu na nyumbani kwetu. Kwa kifupi alikuwa binti mcharuko sana. Hakuna mwanaume mwenye pesa zake pale kijijini ambaye hakutembea naye.

Alipewa jina baya kwamba yeye ni malaya, asiyejua kukataa kila mwanaume anayemtaka. Huyo ndiye ambaye nilikwenda kutambulishwa kama mke mtarajiwa wa rafiki yangu. Nilishituka sana lakini nikaona si vyema kuanika kilicho moyoni mwangu.

Nilijaribu kumuuliza rafiki yangu huyo alimpataje, jibu likawa ni kwamba walionana jijini Dar mwaka jana wakati binti huyo anaingia mjini kwa mara ya kwanza, akampenda na akaona amuoe. Kwa kifupi hakumjua vizuri binti huyo. Alikuwa ni mzuri wa sura na umbo, alikulia kijijini lakini alishindwa kujitunza. Rafiki yangu alipomuona, akajua amepata mke.

Kwa nini nimeanza kwa kisa hicho? Ni kwa sababu najua tulio wengi tunaingia kwenye uhusiano na watu ambao hatujui historia zao. Wanaume wanakutana na wasichana wazuri lakini ukiwafuatilia historia zao utagundua ni wachafu kupita maelezo.

Wanawake nao wanakutana na wanaume ‘handsome’, wanaojiweza kifedha lakini historia zao ni mbaya. Katika mazingira hayo unawezaje kujiaminisha kwamba umepata mtu sahihi?Mbaya zaidi unaanzisha uhusiano leo, baada ya wiki unataka kuingia kwenye ndoa. Eti umechoka kusubiri. Jamani, hivi umetumia muda gani kumchunguza na kubaini kwamba hata ukiingia naye kwenye uhusiano au ndoa hutajuta?

Tunafahamu kwamba si kila kinachong’ara ni dhahabu, wapo wanaume ambao ni wazuri kwa kila jambo lakini hawana sifa za kuitwa mume. Vivyo hivyo kwa wanawake, wapo ambao ukiwaona unasema umepata mke lakini kumbe ni full matatizo.

Kwa maana hiyo basi, tunatakiwa kuwa makini sana na watu ambao tunakutana nao na kutokea kuwapenda. Imetokea umempenda, ukafukia historia yake na kuamua kuingia naye kwenye maisha ya ndoa.

Hilo ni kosa kubwa sana ambalo linawaliza wengi sasa. Kumuoa au kuolewa na mtu ambaye humjui vizuri ni majanga kwani unaweza kukuta unaoa mtu ambaye ameathirika na ukaja kujua mkiwa mmeshaoana na kujiachia.

Mwisho niseme tu kwamba, tujihadhari sana kuoa au kuwa kwenye uhusiano na watu ambao hatuwajui kisa ni wazuri na wana pesa kisha wametuzimikia.

Balaa lake huko mbele ni zito ambalo linaweza kuyafanya maisha yako yakawa ni kulia tuu. Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.


Loading...

Toa comment