The House of Favourite Newspapers

UKISTAAJABU YA KANUMBA , MAJUTO UTAYAONA YA MAVOKO NA WCB

BASATA si jina geni Bongo kwa sababu ya urafiki wake wa karibu na wanasanaa wote Bongo na ndiyo maana kirefu chake ni Baraza la Sanaa la Taifa. Moja kati ya kazi wanazofanya ni pamoja na kusimamia wasanii, kuthibiti maadili ya kazi za sanaa na mengineyo, kwa hilo big up!

Baraza hili limekuwa bega kwa bega na wasanii hasa pale wanapopata nafasi ya kuiwakilisha nchi, tumeona likifanya hivyo kwa wasanii mbalimbali. Mfano, Januari, mwaka jana, lilipomkabidhi Bendera ya Taifa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kwa ajili ya shoo yake ya kutumbuiza ufunguzi wa Michuano ya Afcon 2017 iliyofanyikia nchini Gabon.

Lilifanya hivyo pia Aprili, mwaka huu kwa msanii wa filamu Bongo, Yvonne-Cherry Ngatikwa ‘Monalisa’ baada ya kuchaguliwa kuwania Tuzo za African Prestigious nchini Ghana, vivyo hivyo kwa wasanii wengine wengi waliobahatika kuiwakilisha nchi.

Kitu kikubwa kilichoanza kutia doa baraza hili ni kitendo cha kuanza kufungia nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva sambamba na kuwapa adhabu za jukwaani wasanii husika, walianza kufanya hivyo kwa msanii, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ mwaka 2015 kwa kumfungia mwaka mmoja baada ya picha zake kusambaa zilizoonesha baadhi ya maeneo ya kifua chake kikiwa wazi akiwa katika moja ya shoo zake nje ya nchi.

Liliwahi pia kumfungia Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kwa kipindi kisichojulikana baada ya kuachia Wimbo wa Pale Kati, likafanya hivyo kwa wasanii wengine ambao ni Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ aliyefungiwa miezi sita, kisa wimbo wake wa Kibamia, Snura kupitia Wimbo wa Chura na wengine wengi.

Mbali na kuwafungia wasanii na baadaye kukaa nao kisha kuwafungulia waendelee na sanaa, baraza hilihili bado limezifungia nyimbo kadhaa hadi leo zikiwemo Hallelujah na Wakawaka za Diamond Platnumz, Hainaga Ushemeji ya Man Fongo, Iam Sorry JK ya Nikki Mbishi, Tema Mate Tumchape ya Madee, Uzuri Wako ya Jux, Nampa Papa wa Gigy Money na nyingine nyingi, ukiangalia kwa jicho la tatu zipo baadhi kosa lake hulioni.

ISHU YA MAJUTO NA KANUMBA

Mwishoni mwa Aprili, mwaka huu bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2018/19, Waziri Dk Harrison Mwakyembe kupitia Basata alisema ameunda kamati ya wanasheria ya kuchunguza mikataba ya kibiashara waliyoingia marehemu Steven Kanumba na King Majuto.

Lengo la kamati hiyo ni wasanii waweze kulipwa fidia zao kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa na makampuni mbalimbali bila kunufaika.

Aidha, Mwakyembe alisema kuwa, kamati hiyo maalum ya wanasheria itakagua mikataba yote ya mashirika na makampuni waliyoingia wasanii King Majuto na marehemu Steven Kanumba na endapo kutakuwa na uonevu wowote watalipwa fidia.

Tangu kuongea kwa Mwakyembe Aprili, mwaka huu, baraza ambalo ndilo linahusika kutekeleza ishu hiyo bado halijatoa chochote kinachoendelea. Licha ya ushapu wao katika kuwasimamisha na kufungia nyimbo za wasanii, kwa hili limeshindwa kuwa wepesi katika kuweka wazi kinachoendelea katika kamati iliyoundwa.

Hatuwapangii majukumu, lakini hatujatajiwa au kuwekwa wazi ni makampuni yapi yaliyokuwa yakinyonya wasanii ambao kwa sasa ni marehemu kama Kanumba na King Majuto, mikataba ya aina gani walipitia na hawajanufaika nayo.

Ukiwa bado unastaajabu hayo, lipo mezani suala jingine la aliyekuwa msanii wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Richard Martin ‘Rich Mavoko’ ambaye anadai kuingia mkataba wenye ‘makengeza’.

Licha ya msanii mwenyewe kukwepa maswali ya waandishi juu ya hili, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alithibitisha kuwa na tatizo kati ya Mavoko na WCB kupitia mkataba wa kikazi waliosaini kipindi cha nyuma.

Mngereza alisema kuwa, Mavoko alitua barazani hapo kuwasilisha malalamiko yake pamoja na kujisajili katika baraza hilo na kukiri pia kupata mkataba huo kutoka kwa Mavoko. Mngereza alidai ataupeleka kwenye ‘ile kamati’ iliyoundwa na Waziri Mwakyembe kwa ajili ya kuuangalia ambapo pia alisema watauita uongozi wa WCB.

Wakati hayo yakiendelea, kumbuka kamati bado haijatoa hatua hata moja iliyofanikiwa, bado inaendelea kupokea mikataba mingine ya wasanii.

Nawasilisha!

Comments are closed.