The House of Favourite Newspapers

Ukitafuta mafanikio kwa njia za mkato, itakula kwako!

0

Mpenzi msomaji wangu, mafanikio katika maisha yako yatatokana na utendaji wako wa kazi halali huku ukiwa umejiwekea malengo.
Lakini sasa linapozungumziwa suala la kutafuta maisha mazuri na yenye mafanikio, wapo watu wanaodiriki kujiingiza katika shughuli zisizo halali ambazo mwisho wa siku zinaweza kuhatarisha maisha yao.
Zipo kazi nyingi tu ambazo ukizifanya kwa nguvu zote na kwa malengo, unaweza kuwa na mafanikio makubwa na ukaishi maisha ya furaha na amani. Hapa nazungumzia zile kazi ambazo ni halali.

Lakini huwa najiuliza, hawa wanaofanya kazi zisizo halali walishawahi kujiuliza hatima ya maisha yao itakuwaje?
Kwa nini ufikie hatua ya kufanya kazi ambayo itafanya maisha yako yawe hatarini? Wapo wanaosema eti wanafanya hivyo kwa sababu maisha ya sasa ni magumu hivyo ugumu huo unaweza kuukabili kwa kufanya kazi hizo.

Hii ni hatari sana na hata hao wanaojipatia mapesa kwa kufanya kazi kama vile za kuuza madawa ya kulevya, bangi, utapeli, uchangudoa na shughuli nyingine za namna hiyo, maisha yao si ya furaha kama watu wanavyodhani. Wanaishi maisha ya wasiwasi huku wakihofia usalama wao.

Uchunguzi unaonesha kwamba wengi wanaofanya biashara hizo haramu mwisho wao huwa mbaya sana ambapo baadhi yao huishia kuuawa, kufa ama kufungwa jela.

Nenda kwenye magereza leo hii, utakuta waliojaa huko wanatuhumiwa kwa ujambazi, wizi, uuzaji wa madawa ya kulevya, watu ambao walidhani kwa kufanya hivyo wanaweza kuyafanya maisha yao yakawa mazuri, kumbe ndiyo wanajiweka katika wakati mgumu zaidi.

Tambua kwamba zipo kazi nyingi tu ambazo unaweza kuzifanya na ukawa tajiri ama kuwa na mafanikio makubwa bila kuiba kitu cha mtu wala kudhulumu.
Kwa kutumia akili yako, nguvu zako pamoja na maarifa aliyokujaalia Mungu, naamini kabisa unaweza kufanikiwa na kuishi maisha ya amani yaliyojaa furaha.

Siyo mpaka uibe ndiyo ufanikiwe, siyo lazima uuze madawa ya kulevya wala kuuza mwili wako ndiyo uukate. Fahamu wapo watu wengi waliopata mafanikio makubwa kwa kupambana kihalali. Mifano ya watu hao ipo huko mtaani.
Kwa kifupi kaa ukijua kwamba hakuna njia za mkato kwenye kutafuta mafanikio ya kweli. Wazungu wanasema ‘Life has no shortcut’. Kwa maana hiyo basi, wanaoendesha maisha yao kwa njia ya mkato, hawana furaha na mafanikio ya kweli katika maisha yao.
Ndiyo maana inaelezwa kuwa wanaotegemea kuendesha maisha yao kwa kufanya kazi ambazo siyo halali, wako katika nafasi nzuri ya kukumbwa na balaa kiasi cha kuwafanya kutozifurahia fedha walizo nazo.

Kwa mfano; wapo akinadada ambao wameridhika kabisa kuendesha maisha yao kwa kufanya biashara ya kuuza miili yao. Wanaofanya hivyo wanaeleza kwamba kinachowasukuma ni ugumu wa maisha.
Maisha yanaweza kuwa magumu kama hutajishughulisha. Lakini hata kama maisha ni magumu kiasi gani, ndiyo ufikie hatua ya kuweka rehani maisha yako?

Leave A Reply