UKIWA KWENYE NDOA, MAZOEA NA WATU WA NJE NI SUMU HATARI

MIMI nipo kwenye ndoa, huu ni mwaka wa tatu sasa. Tatizo lililonifanya niombe ushauri, mume wangu ana kawaida ya kuwa anachati na wafanyakazi wenzake wa jinsia ya kike kwenye simu yake, na wakati mwingine hata mbele yangu. “Nimegombana naye mara kadhaa kwa sababu hiyo lakini mwenyewe ananiambia nisiwe na wasiwasi, ni marafiki zake wa kawaida na hakuna chochote kibaya kinachoendelea.

“Kinachoniumiza, akiwa anachati nao muda mwingine anakuwa na furaha kwelikweli, mara atacheka, atatabasamu kuonesha kwamba huyo anayechati naye anamfurahisha. Nisaidieni jamani nifanye nini? Nahisi ndoa imekuwa chungu.”

Hayo ni malalamiko kutoka kwa msomaji wangu, Shamal wa Kurasini jijini Dar es Salaam ambay amekubali hata jina lake liandikwe kwenye ukurasa huu. Nimeanza moja kwa moja na ujumbe huo ili nisikuchoshe msomaji wangu. Hebu vuta picha wewe ndiyo dada Shamal, utafanya nini ukiwa katika hali kama hiyo? Lakini pia vuta picha wewe ndiyo mume wa Shamal, unaelewa ni kwa kiasi gani unauumiza moyo wa mwenzako?

Ipo tabia ya baadhi ya watu kuwa na mawasiliano na watu wa jinsia nyingine, kwa madai kwamba ‘huyu ni rafiki yangu’. Wakati mwingine inakuwa kweli kwamba hakuna chochote kibaya kinachoendelea kati yao, ni urafiki wa kawaida kabisa lakini je, ni sahihi kwa mtu ambaye yupo kwenye ndoa kuwa na ukaribu wa aina hii na mtu wa nje?

Unaishi na mkeo, kwa nini unaendeleza mawasiliano na wanawake wa nje? Hata kama hakuna chochote kati yenu, kwa nini unawapa muda wako? Kwa nini unawaruhusu wavuruge amani iliyopo ndani ya ndoa yako? Kwa wanawake pia, unaishi ndani na mumeo. Kwa nini unakuwa na mazoea na wanaume wa nje kwa kisingizio cha ‘nilisoma nae’, au ‘ni mpenzi wa rafiki yangu’?

Simu yako kutwa iko bize, mara dereva wa bodaboda anayekubeba anakuuliza maswali yasiyohusiana na kilichowakutanisha, mara muuza bucha anakuuliza kama akuwekee mboga gani na mambo mengine mengi yenye kuudhi.

Kwa nini unakosa nidhamu na matumizi ya simu yako? Wasichokijua watu wengi ni kwamba kuwa na mazoea na watu wa jinsia nyingine wakati upo kwenye ndoa, ni jambo la hatari ambalo ukilichekea, linaweza kusababisha hata ndoa yako ikavunjika kimasihara.

Tukirudi kwenye swali la dada Shamal, hata kama mumewe anamhakikishia kabisa kwamba hana uhusiano wowote zaidi ya urafiki wa kawaida, dalili zinaonesha kuna tatizo kubwa linaenda kutokea mbele. Hakuna ukaribu au urafiki wa watu wa jinsia mbili tofauti, unaoweza kubaki kuwa urafiki kwa muda mrefu.

Wengi huanza hivihivi lakini mwisho huzoeana na taratibu mapenzi huanza kuchipuka. Ukiwauliza watu wengi waliowahi kusaliti ndoa zao, walifanya hivyo na watu wao wa karibu, waliozoeana nao, iwe ni wafanyakazi wenzao, majirani zao au watu waliowahi kusoma pamoja.

Usiishie kuamini tu kwamba ‘huyu ni rafiki wa kawaida tu’, hakunaga urafiki wa kawaida kati ya mwanaume na mwanamke, ipo siku watavunja amri ya sita kwa kutumia kigezo hichohicho kwamba hakuna atakayejua kwa sababu sisi ni marafiki kwa hiyo itabaki kuwa siri yetu.

Kama kweli unampenda na kumheshimu, achana na hayo mambo na namshauri Shamal awe mkali katika hilo, ikiwezekana awashirikishe watu wazima ambao mumewe atawasikiliza kwa sababu akiendelea kumchekea mumewe, ipo siku atalia na kusaga meno. Kwa leo ni hayo tu, tukutake wiki ijayo.

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment