The House of Favourite Newspapers

Ukiwa mke wa mtu usithubutu kufanya ujinga huu!

1

Couple-in-Bed

KWA rehema zake Mungu, Jumamosi nyingine anatukanisha wadau wa Love Story. Hapa tunapeana elimu ya uhusiano. Wiki iliyopita tulijifunza kuhusu ubinafsi. Nilisema ni kirusi hatari katika uhusiano. Nawashukuru wote mliosoma na kuelewa.

Ni matumaini yangu mtakuwa mmejifunza kitu, nimeona mrejesho kupitia meseji zenu mlizonitumia. Hakuna sababu ya kuwa mbinafsi katika uhusiano. Ukiona mwenzako anakufanya jambo fulani linalokufurahisha, mfanyie na wewe.

Mjali kama anavyokujali wewe. Jali ndugu zake kama anavyojali wa kwako. Thamini ugonjwa wake kama anavyothamini wa kwako. Mpende kama anavyokupenda na maisha yenu ya uhusiano yatakuwa ya raha mustarehe kwa msaada wa Mungu, mtaishi vizuri kwa amani na furaha.

Turudi kwenye mada ya leo. Leo nazungumza na wanawake zaidi ingawa naamini pia mada hii itawasaidia wanaume. Kwa namna moja au nyingine, wanaweza kuwasaidia wake zao, migogoro itapungua ndani ya nyumba.

Kwa hakika kila mtu anatambua thamani ya ndoa. Kumkubali mtu awe mume au mke wako, lazima uwe tayari kuwa na maisha mapya. Unatoka katika maamuzi ya binafsi na kwenda kwenye maamuzi ya pamoja.

Kabla ya ndoa, mwanamke anajiamulia mambo yake. Anapoingia kwenye ndoa, mambo mengi wanaamua pamoja na mumewe. Ratiba zinabadilika. Aina ya marafiki wanabadilika, haimaanishi uwatenge kabisa, hapana. Namna ya kuwasiliana nao inabadilika.

Kunakuwa na mipaka fulani kati ya maisha ya ndoa na yale ya kabla. Ule utani uliozidi mipaka unapaswa kupungua. Kama walikuwa wanazoea kufika nyumbani kwako, kuingia hadi chumbani kwako, mkakaa kwenye kitanda kupiga stori, unapoolewa hutakiwi kuruhusu jambo hilo.

Hapo ndipo kwenye msingi wa mada yangu. Kuna watu wanaingia kwenye ndoa huku kwa kujua au kutojua wanajikuta wakifanya mambo ya kijinga. Wanashindwa kujitambua. Wanashindwa kuendana na muktadha wa ndoa.

Mke anajikuta akifanya mambo yaleyale ambayo alikuwa akiyafanya kabla ya ndoa. Mfano; utakuta mwanamke alikuwa na utani wa uliopitiliza na marafiki. Marafiki hao wanaweza kuwa wa kike au wa kiume. Yeye anaendelea kuwatania na wao kumtania.

Mazoea ya kuitana ‘baby’ au majina mengine ya kimahaba yanayofanana na hilo. Kutaniana vitu vya kijinga katika simu anaendelea nayo pasipokujua kama anapaswa kuviacha.

Anashindwa kuelewa kwa kufanya hivyo anawarahisishia kazi marafiki hao kufanya mambo ya ajabu yatakayoweza kuhatarisha ndoa yake.

Hutakiwi kuruhusu tena mazoea ya kutumiana picha kwenye mitandao, eti mnataniana. Mwanaume asiye mumeo anakuomba picha, umtumie eti halafu akuambie umependeza. Huo ni ujinga. Unaporuhusu kufanya vitendo hivyo jua kabisa unatoa mwanya kwa huyo unayemtumia kukutongoza.

Wewe ni mke wa mtu, una sababu gani ya kuitana baby, mpenzi au majina mengine yanayofanana na hayo na mtu ambaye si mume wako? Una sababu gani ya kumtengenezea mtu mazingira ya kujirahisisha?

Usijichekeshe kwa mwanaume asiye mume wako. Unapozungumza na mwanaume asiye mumeo, usitumie lugha ambayo haina staha. Kufanya hivyo kunamfanya unayezungumza naye akuone hujiheshimu. Kama hujiheshimu unampa ruhusa ya kukutongoza maana anaona unatongozeka.

Kuishi kwa maigizo nao ni ujinga mwingine ambao mwanamke hapaswi kuufanya. Hupaswi kuishi kwa kuiga marafiki zako. Unapokuwa kwenye ndoa wewe na mumeo ndiyo mnaunda ‘serikali’ yenu. Hupaswi kutaka kuvaa kama marafiki zako ambao hawajaolewa wanavyovaa.

Unapaswa kuvaa mavazi ya heshima maana wewe sasa ni mke wa mtu. Haimaanishi kwamba usipendeze lakini vazi unalovaa liwe na staha. Likutofautishe na madada poa wanaojiuza barabarani. Usifanane sana na wale wadada ambao hawana ndoa.

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri! 

1 Comment
  1. Nesphory Ntuyahaga says

    Vizuri sana.
    Ni busara kutafuta sababu za kuimarisha ndoa zaidi ya kutengeneza mazingira ya kuiteteresha.

Leave A Reply