Ukiwa na hamu, ndoa utaiona tamu

blackcouple-bedsmile

MMH! Makubwa madogo yana nafuu, kweli maisha yamekuwa zigizaga, vipofu ndiyo wanaotuongoza, matokeo yake tunatumbukia shimoni.

Kwa hili siwezi hata kidogo kulifumbia macho, kwa nini wasiojua maana ya ndoa wanawadhalilisha wanawake wenzetu?

Wahenga walilitambua hili zamani, ndiyo maana msichana hakupewa ndoa mpaka apitie mafunzo kujitambua yeye ni nani ndani nyumba.

Kweli asiye na hamu hawezi kuiona tamu. Jamani kuolewa si mchezo wa kuigiza bali ni maisha yanayotambulika kwa Manani.

Napenda kukupasha shoga yangu kwamba ndoa ina raha yake hasa ukiijua, mumeo utamuona mfalme na wewe utakuwa malkia.

Nakumbuka nilipovunja ungo, niliwekwa chini na bibi yangu mzaa mama, Mwenyezi Mungu amrehemu huko aliko.

Kutokana na mapishi yake, kila nilipokuwa nikimaliza kula lazima nilijilamba vidole na kumsifia bibi kwa utamu wa chakula.

Siku zote alinijibu kuwa nikikiona chakula ni kitamu ni kwa sababu nilikuwa na hamu nacho.

Siku zote sikumwelewa, lakini kabla ya kuolewa aliniuliza swali kwa nini chakula kinakuwa kitamu?

Jibu langu lilikuwa jepesi tu ni kwa sababu kimeungwa vizuri. Akaniuliza swali, cha chukuchuku hakina utamu? Nami nilimjibu hakina utamu. Akaniuliza tena mihogo ya kuchemsha ni mitamu au siyo mitamu? Nilimjibu ni mitamu, akaniuliza kwa nini? Sikuwa na jibu.

Basi bibi akanielezea kuwa utamu wa vyakula unazidiana, vipo vya kuungwa lakini vingine siyo vitamu na vipo visivyoungwa vikawezekana kuwa vitamu.

Nilimuuliza kwa nini? Alijibu, hamu siku zote huwa haishindi tamu, huleta utamu hata kwa chakula cha chukuchuku.

Basi, hapo akaniuliza unapenda kuolewa? Nilimjibu napenda, akaniuliza ndoa una hamu nayo? Nikamjibu tena sana, akaniambia kama kweli nina hamu nayo, lazima nitaiona tamu na kuiheshimu.

Hata nilipokuja kuolewa, kutokana na mafunzo niliyopewa, nilikubaliana na bibi kuwa kweli ndoa ni pepo ya dunia, hasa pale ukimpata anayekupenda na huweza kuwa moto wa dunia ukipata aliyeingia bila ya kuwa na hamu nayo.

Nasema hivi nina maana gani? Kuna mchezo mchafu wa ndoa unaoendelea hivi sasa kwa wasichana kuolewa na kuwa wazururaji wanaokamatwa na mgambo wa jiji na mwisho wake ndoa kuwa kichekesho.

Leo hii mtu anaolewa, hakai na mumewe zaidi ya kuzunguka kila kona, anakuwa kiguu na njia.

Inaoneka wazi hiyo ndoa yako umeolewa ili uonekane nawe umeolewa, lakini huna hamu nayo, siku zote kwako huioni tamu kwa sababu huna hamu nayo.

Mwenye kuwa na hamu na ndoa hawezi kukaa mbali na mumewe, wala kujichukulia madaraka mkononi, bali huikumbatia ndoa yake kwani hiyo ndiyo pingu ya maisha yake.

Yangu ni hayo, kama hujawa na hamu na ndoa usiolewe. Hakuna tamu bila kuwa na hamu. Ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.


Loading...

Toa comment