Ukiwa na Sifa Hizi Lazima Uolewe!

MOJA kati ya kilio kikubwa cha mabinti ni kupata wanaume sahihi wa kuwaoa. Ishu si tu kuolewa lakini kupata mume sahihi ni jambo lingine.

Wengi wanaishia kukutana na wanaume ‘wasanii’ ambao hawana mpango wa ndoa. Wao wanafurahia maisha ya ujana hadi pale watakapojisikia. Kwa kuwa kiasili mwanaume ndio humfuata mwanamke, fursa ya kuanza kuchagua mke mtarajiwa, mchumba, ‘girlfriend’ huwa inaanza kwa mwanaume.

Wazo la kukufanya wewe kuwa rafiki, mchumba na baadaye mke mara nyingi huwa linaanza kwa mwanaume. Hivyo basi utakubaliana na mimi kwamba, kwa kiasi kikubwa mwanaume ndio mwenye ‘funguo’ ya ndoa. Ndiye anayeweza kusema ‘Yes’ au ‘No’. Mara nyingi mwanaume ndiyo mwenye maamuzi ya kusema nioe au nisioe kwa sasa.

Ndio mwenye uamuzi wa kusema nioe mwanamke huyu au nisimuoe nitaoa mwingine. Nimuoe huyu kwa sababu ananifaa, nimuache huyu kwa sababu hanifai. Licha ya kuwa mwanaume anaweza kuwa na matatizo yake lakini pamoja na yote hayo, jukumu la kufanya maamuzi huwa linabaki kuwa kwake.

Hapo ndipo kwenye msingi wa mada yangu, umeishi kwa muda mrefu na umri umeenda hujapata mchumba? Yawezekana kweli ukawa na bahati mbaya ya kukutana na watu ambao si sahihi lakini leo acha nikupe mbinu sahihi za kumpata mwanaume sahihi.

Jitathimini mwenendo wako, ni rafiki kwa waoaji? Kama kila siku wewe ni mtu wa viwanja, mtu wa kupenda starehe leo huku kesho huku jua kwamba kuolewa utachelewa sana.

Ishi kwenye mazingira ya kistaarabu. Jiheshimu na sio kila siku kuwa mtu wa starehe, utaishia kuwapata watu wanaopenda starehe ambao mara nyingi nao huwa wana kasumba ya kubadilishabadilisha wanawake. Wanabadilisha kwa sababu maisha yao ni ya anasa. Kubadilisha wanawake pia kwao ni anasa, ni burudani na wanapenda kwelikweli.

Kuwa na haiba ya kike. Wanaume wengi waoaji huwa wanapenda kuoa wanawake wapole, wasikivu ambao hawapendi malumbano. Sio mwanamke unapenda malumbano kama kitu gani, wanaume hawapendi kelele nyingi kwani kiasili wanachoshwa na mihangaiko ya kila siku.

Wanaume wanapenda wanawake ambao wanaongea kidogo na kusikiliza zaidi. Mwanamke ukiwa muongeaji sana, unaweza kuwakosa wanaume ambao hawapendi kelele. Jiweke karibu na Mungu, ishi katika misingi ambayo inakuonesha hata kwa macho tu kwamba una hofu ya Mungu.

Kwa imani fauta ile misingi ya dini, kama Muislamu nenda Msikitini na kama ni Mkristo nenda Kanisani. Usiishi kama vile upo kwenye dunia yako. Usiwe na kasumba za chuki, kupenda ugomviugomvi kila mara na pia uwe mtu wa kujali matatizo ya mwenzi wako pamoja na roho nzuri kwa ndugu na jamaa wa mwenza wako.

Epuka kuwa na gubu. Fungua moyo wako kwa mtu sahihi. Muombe Mungu akupe mume mwema, kubali kukosolewa, kubali kumsikiliza mchumba wako, atakupenda sana.

Mheshimu mwanaume wako mtarajiwa, mpe heshima yake na yeye atakupenda sana! Kwa leo inatosha!

Tukutane wiki ijayo hapahapa. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia jina la Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Toa comment