Ukizingatia haya, simu haiwezi kuwa kikwazo cha uhusiano wenu!

phoneMUNGU ni mwaminifu kila wakati, ametukutanisha kwa mara nyingine Jumamosi ya leo. Hapa tunajadili masuala mbalimbali yahusuyo uhusiano.

Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita, nilieleza kuhusu mambo ya kufanya ili mwanamke usiishie kuzalishwa na kuachwa.

Lilikuwa ni somo lililowagusa wengi, niwashukuru wale wote walionitumia ujumbe kueleza hisia zao juu ya mada hiyo.

Wiki hii, tunaijadili mada iliyopo hapo juu. Miaka ya nyuma, hususan wakati simu za mkononi zilipokuwa hazijaingia nchini, matatizo kwa wanandoa au wapendanao yalikuwa machache sana kulinganisha na sasa baada ya ujio wa simu.

Wachambuzi wa masuala ya uhusiano wamekuwa wakitaja simu kama kichocheo kikubwa cha wapendanao au wanandoa kugombana.

Simu ndizo zinazoleta uhasama na kuvunja ndoa nyingi. Simu ndizo zinawafanya watu wengi waliopo kwenye uhusiano kugombana.

Bahati mbaya sana, kati ya kesi nyingi za simu, zipo ambazo zinakuwa na ukweli lakini nyingine huwa hazina ukweli. Mtu anaanzisha ugomvi kwa sababu tu ujumbe wa kimahaba umeingia kwenye simu ya mke au mumewe.

Hahitaji kuhoji. Anapoona tu ujumbe umeingia, kinachofuata ni ugomvi kwa mwenzi wake. Atamtukana, atampiga na atafanya kila linalowezekana kuhakikisha anaondoa hasira zake kwa kile alichokiona.

Kumbe pengine angejipa nafasi ya kutafakari, akahoji, labda hata wasingefikia hatua ya kugombana. Anaanzisha ugomvi kumbe yule aliyetuma ujumbe huo, mwenzi wake wala hamjui.

Amekosea namba, ujumbe ukaingia kwenye simu ya mpenzi wake. Wapo ambao wakiona ujumbe huo wa kimahaba, eti wanakaa kimya na kujisemea kimoyomoyo; “ngoja na mimi nitamuoneshea.”

Eti ataruhusu uhusiano na mtu mwingine ili wawe ngoma droo na mwenzake. Hilo ni tatizo kubwa. Unafanya malipizi kwa mtu ambaye hajafanya kosa. Matokeo yake ni nini? Mwenzi wako atakapokugundua umefanya hivyo kwa makusudi, mtagombana na hata kufikia hatua ya kuachana.

NINI CHA KUFANYA?

Suala la kwanza unalopaswa kufanya kabla hujaingia kwenye uhusiano, mchunguze vizuri mhusika. Hakikisha ni mtu mwenye moyo wa kuridhika.

Ninaposema moyo wa kuridhika nina maana gani? Awe tayari ameshaamua kuwa ‘serious’ na mtu mmoja. Macho yake si ya kutangatanga. Hababaishwi na kila mwanamke au mwanaume amuonaye. Mtu wa aina hiyo hafai. Atakupotezea muda. Atakusababishia ugomvi kila wakati mbele ya safari. Anzisha uhusiano na mtu aliyetosheka na ujana.

Kuna baadhi ya watu huingia kwenye uhusiano wakiwa angali hawajamaliza ujana, hao ni hatari sana. Hawatulii. Kila anayemuona mbele yake anatamani awe wake. Ni vyema mkazungumza mapema mikakati yenu na kila mmoja akampima mwenzake kulingana na safari ya uhusiano wenu.

UAMINIFU

Ukishafanikiwa kuwa na mtu mwenye sifa hizo, kinachofuata ni suala la uaminifu. Jenga imani kwa mwenzako. Mfikirie katika fikra chanya zaidi na si hasi. Muamini kwamba hawezi kukusailiti.

Ukimuwazia mwenzako katika mazuri ni rahisi hata kukabiliana na wazushi watakaokuletea maneno ya uongo ili kukugombanisha na mwenzi wako.

Unapomtengenezea mazingira ya kumuamini zaidi mtu, unampa nafasi ya kukufanya wewe kama sehemu ya maisha yake. Unamfanya ahisi kukusaliti ni kukupa maumivu mazito. Hiyo inasaidia kuleta amani katika uhusiano.

Mnapoaminiana, hamuwezi kuwa watu wa kukaguana simu kila wakati. Hamtakuwa na hofu ya kupokea simu mnapokuwa pamoja. Yale mambo ya kwenda kuzungumzia chooni au kumkatia simu yule anayepiga hayatakuwepo.

Tukubali tukatae, unapoamua kuwa kwenye uhusiano makini, lazima ujitoe. Hakikisha huna makandokando maana ukiwa nayo, hata kama unajua kujificha kiasi gani, za mwizi wanasema ni arobaini, ipo siku utaumbuka tu.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.


Loading...

Toa comment