The House of Favourite Newspapers

Ukuta; Jaribio no 1 kwa Mwigulu

0

Mwigulu (1)STORI: ELVAN STAMBULI, WIKIENDA

DAR ES SALAAM: Baadhi ya wananchi wameliambia Wikienda kuwa, jaribio namba moja la Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Lameck Nchemba ni tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambalo limesema chama hicho hakitarudi nyuma katika azma yao ya kufanya maandamo ya kuzindua Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) Septemba Mosi, mwaka huu.

Tamko hilo limekuja baada ya Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ kuwataka Chadema kutofanya maandamano waliyopanga na kwamba watakaopuuza amri hiyo watakiona cha mtema kuni.

Kufuatia kauli hiyo, Wikienda lilifanya mahojiano na watu mbalimbali ambao walisema Mwigulu ana kazi ya ziada kwa sababu tamko la Chadema kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu, Salum Mwalimu na mwanasheria wao, Tundu Lissu ni jambo zito kuwahi kutokea tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo Juni 11, mwaka huu akichukua nafasi ya Charles Kitwanga.

Mohammed Ali, mkazi wa Mwananyamala aliliambia gazeti hili kuwa ingefaa msuguano huo kati ya serikali na wapinzani ukapatiwa ufumbuzi kuepusha maafa kama yale yaliyotokea Pemba mwaka 2001 ambapo wananchi walipoteza maisha.

Salum Mwalimu, alipoulizwa juzi kuhusu marufuku ya Rais Magufuli kuhusiana na mikakati yao ya kuzindua Ukuta kwa maandamano kama alivyotamka mwenyekiti wao, Freeman Mbowe alisema mipango yao ya Septemba Mosi, inaendelea kama kawaida ikiwemo kukutana na wadau wa Ukuta, hakuwataja.

Naye Tundu Lissu alisema hakuna sheria inayomruhusu kiongozi yeyote wa nchi kupiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa.

Akizungumza kwa njia ya simu, Lissu alisema kitendo cha rais na mkuu wa polisi (IGP) kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa ni kinyume cha sheria ya vyama vya siasa na polisi nchini.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema kifupi. “Hayo mambo ya siasa waulize wanasiasa wenyewe.”

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye ndiye aliyetoa tamko la chama, Juzi (Jumamosi) alisema: “Nimepata wito nikitakiwa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar, Kamanda Wambura, akihitaji nifike leo (Jumamosi), lakini nipo Marangu (Kilimanjaro) kuhudhuria maziko ya baba yake mzazi wa Devotha Minja, Mbunge wa Viti Maalum Chadema.

“Jumapili (jana) nitakuwa katika shughuli za kuuaga mwili wa mfanyakazi mwenzetu na aliyekuwa mpiga picha wa Gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga aliyefikwa na umauti akiwa kwenye matibabu India, ikiwemo mimi kusafiri kwenda Kwimba, Mwanza kwa maziko Jumatatu (leo). Najaribu kurekebisha ratiba zangu niweze kwenda Jumapili (jana)…sifahamu naitiwa nini.”

Hata hivyo, Mwigulu hakupatikana kuzungumzia sakata hilo.

Leave A Reply