The House of Favourite Newspapers

Ukweli Kuhusu Tetesi…. TRA Kuifungia Serena Hotel

0

tmp_14269-Dar-es-Salaam-Serena-Hotel1489278414HOTELI ya Kimataifa ya Serena jana ilikumbwa na msukosuko wa kuandamwa na waandishi wa habari baada ya kusambaa kwa tetesi kuwa imefungwa kwa amri ya serikali kwa kosa la ukwepaji wa kodi.

Tetesi hizo zilisambaa jana kwenye mitandao ya kijamii, zikieleza kuwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameifunga hoteli hiyo baada ya uongozi wake kukwepa kulipa kodi serikalini kwa mujibu wa sheria.

Mbali ya kusambaa kwa uvumi huo, zilitumwa picha zilizokuwa zikionesha sehemu ya hoteli hiyo ikiwa imezungushiwa uzio uliokuwa na rangi nyeupe na nyekundu ambao ni alama inayotumika kuonesha kusitishwa kwa huduma katika eneo hilo.

Tetesi hizo zilikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa uongozi wa hoteli hiyo ulikuwa mbioni kubadilisha jina kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.

Baada ya taarifa hizo kuenea mitandaoni waandishi wa habari walifika hotelini hapo kwa lengo la kufuatilia ukweli wa tetesi hizo na kukuta shughuli za ukarabati wa sehemu ya mapkezi zikiendelea, huku wageni wakielekezwa kutumia mlango wa dharura ambako kumetengezwa sehemu ya muda ya kupokelea wageni.

Uongozi wa Hoteli ya Serena kupitia Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko, Seraphine Lusala, ulilazimika kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ukikanusha kufungwa kwa hoteli hiyo na kusisitiza kuwa kinachoendelea hotelini hapo ni matengenezo.

“Si kweli kama hoteli imefungwa, tunafanya matengenezo na yalikuwa yafanyike tangu miaka mitatu iliyopita, kilichofanyika sasa ni kubadilisha eneo la mapokezi yaliyohamishiwa milango mingine na tumeanza na eneo hilo pamoja na sehemu ya mazoezi,” alisema Lusala.

Alisema matengenezo hayo yanalenga kuifanya hoteli hiyo kuwa ya kiwango cha juu zaidi na yatachukua miezi 10 ili kukamilika.

Lusala alisema awamu ya kwanza ya matengenezo itachukua miezi minne na miezi minne ijayo itahusu matengenezo sehemu ya vinywaji, chakula, eneo la uwanja na baadaye maeneo mengine ya wazi.

CREDIT: MPEKUZI

Leave A Reply