The House of Favourite Newspapers

UKWELI MAMA DIAMOND KUMTUSI MCHUNGAJI HUU HAPA!

DAR ES SALAAM: Mama wa staa mkubwa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim ‘Bi Sandra’ hana furaha na Mchungaji wa Kanisa la Emmaus Bible Pentecostal Church (EBC) la Mbezi-Luis jijini Dar, Daudi Mashimo ‘Komando Mashimo’.  Mchungaji Mashimo anadai kutukanwa na mama Diamond kwa kumuita; “mwanaume asiye riziki” hivyo Gazeti la Amani kulazimika kutafuta ukweli wa jambo hilo. Katika mahojiano maalum na Gazeti la Amani, Mashimo anayejiita Mchungaji wa Mitume na Maaskofu Tanzania alidai kuwa alipigiwa simu na mama Diamond kisha kumtusi.

KISA UGONJWA WA BABA DIAMOND

Mashimo alisema chanzo cha mama Diamond kumtusi ni kutokana na maneno yake aliyofunguka kuwa yeye (mama Diamond) anahusika na matatizo ya kuumwa ya baba Diamond, mzee Abdul Jumaa.

UGONJWA WA BABA DIAMOND

Baba Diamond anasumbuliwa na ugonjwa wa kuvimba miguu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni dalili za kansa ya ngozi. Wiki kadhaa zilizopita katika mazungumzo yake na televisheni moja ya mtandaoni, Mashimo alimtuhumu mama huyo kuhusika kwa kumloga mzee huyo kisha kumshikilia Diamond na kumnyima kumhudumia baba yake huyo jambo ambalo gazeti hili halikuliamini.

ADAI KUMWAGIWA MATUSI

Kwenye mahojiano hayo na Gazeti la Amani, Mashimo alisema kuwa alipokea simu ya mama Diamond ambaye alimmwagia matusi kisha akatoa namba ambayo ilitumika kumtukana aliyodai ni ya mama Diamond. Mashimo alisema alipopokea simu ya mama Diamond hakuwa na shaka kuwa siyo yeye kwani ana namba zake zote na kwamba anamjua kwa sauti kwani amekuwa akiwasiliana naye mara kwa mara.

AMWACHIA MUNGU…

Alisema, hata hivyo, suala la kutukanwa na mama Diamond anamwachia Mungu na kwamba Mungu ndiye atakayemwadhibu mama huyo. “Mimi siwezi kumfanya chochote, mimi nilisema juu ya maono yangu hivyo suala la nimechukua hatua gani kwa mama Diamond kunitusi, nimemwachia Mungu ndiye atakayemalizana naye kwani vita yetu si ya nyama na damu, bali ni ya rohoni,” alisema Mashimo anayelalamikiwa ‘kudandia’ mambo ya watu kwa kigezo cha kuoneshwa maono.

Katikati ya madai hayo mazito, mapema wiki hii, Gazeti la Amani lilimtafuta mama Diamond au mama Dangote ambapo alipopatikana alidai yupo bize atafutwe baadaye. Alipotafutwa tena, mama Diamond aliendelea kusisitiza kuwa yupo bize.

ESMA AMALIZA UTATA

Akizungumza na Amani juu ya sakata hilo, dada wa Diamond, Esma Khan ‘Esma Platnumz’ ambaye alimaliza utata. Esma alidai kuwa amemsikia mchungaji huyo akitumia jina la mama yake na kumchafua kwa jambo ambalo halina ukweli.

“Kwanza mama yangu anajiheshimu, hawezi kufanya jambo kama hilo. “Nimemsikia huyo mchungaji, hana lolote, anamchafua tu. Mama yangu hawezi kumtukana mtu, amtukane ili iweje? “Huyo mchungaji anatafuta tu kiki ndiyo maana tumempotezea kwani hiyo ishu haina ukweli wowote,” alisema Esma.

AMANI LAMRUDIA MASHIMO

Baada ya kumsikia Esma, Amani liligeuka kijumbe na kumfikishia Mashimo ujumbe kuwa upande wa mama Diamond ulimruka ambapo aliweka msisitizo; “Ni yeye (mama Diamond) ndiye alinipigia na kunitusi. Nina namba na rekodi zake zote, lakini ndiyo hivyo nimeamua kusamehe na sitachukua hatua yoyote.

“Nasisitiza kile nilichokisema kwamba ni maono ya wazi kuwa yeye (mama Diamond) ndiye aliyemshikilia na kumshinikiza Diamond amchukie baba yake. “Maono yalinionesha Diamond hana shida na baba yake, shida ipo kwa mama yake.” Hivi karibuni Mashimo alidai kuwapigia simu simu mama Diamond na meneja wa Diamond, Babu Tale na kuzungumza nao juu ya sakata la Diamond kukataa kumsaidia baba yake mzazi ambaye amekuwa akidaiwa kuwa ni mgonjwa, hali inayosababisha hadi kukosa huduma za matibabu kutokana na kutokuwa na fedha.

Comments are closed.