The House of Favourite Newspapers

ULAJI SAHIHI KWA WATU WENYE KISUKARI

UGONJWA wa kisukari ni tatizo ambalo siku hizi husababishwa na mfumo wa maisha tunayoishi, tafiti zilizowahi kufanywa zinaonesha kuwa vijana wapo kwenye hatari kubwa ya kupata kisukari kwa sababu ya mfumo usio sahihi wa maisha wanayoishi.  

 

Kuna kisukari kinachotegemea Insulin. Kazi ya Insulin ni kurekebisha hali ya sukari kwenye damu, ikiwa ni nyingi inapunguzwa kurudi kwenye hali ya kawaida na ikiwa chache huruhusu irejee kwenye hali ya kawaida pia. Kunapokuwa na hitilafu kongosho likazalisha homoni hii kwa wingi, sukari hupungua mwilini, au isipozalishwa, sukari huongezeka mwilini.

 

Hospitalini, aina hii ya sukari inatibiwa kwa kutumia sindano za Insulin na kurekebisha ulaji wa vyakula.

Kutokufanya mazoezi, kukosa muda wa kupumzika na kutokula mlo sahihi, unywaji wa pombe na uvutaji sigara wa kupitiliza, hizi ni sababu chache zinazochangia vijana kuishi katika mfumo wa maisha hatarishi wa kupata maradhi ya kisukari.

 

Leo tunaangalia suala zima la chakula kwa watu mwenye maradhi ya kisukari, wataalamu wapo wengi sana kwenye hospitali zetu pamoja na majumbani mwetu lakini wewe mwenye ugonjwa wa kisukari ndiyo daktari namba moja katika kutibu afya yako.

 

Kitu muhimu kwa mgonjwa wa kisukari ni kufahamu ya kwamba ana uwanja mpana sana wa vyakula anavyoruhusiwa kula tofauti na mazoea yaliyojengeka miongoni mwetu kuwa mtu anayeugua maradhi haya basi ana vyakula vyake vya kipekee kabisa.

 

Maisha ya mtu mwenye kisukari yanatakiwa kuendelea kama kawaida na unaruhusiwa kula aina zote za vyakula isipokuwa tu vile venye sukari. Unakula kile kilichopo na kinachokuwepo na usijiulize ule nini ila jiulize ule vipi hicho chakula kilichopo, kwa mfano, nyumbani kuna pilau, usipoteze muda na kusema mimi nina kisukari kwa hiyo siwezi kula pilau, la hasha.

Kitu unachotakiwa kujua ni ule vipi hiyo pilau. Pilau ni chakula chenye wanga na kwa kuwa vyakula vya wanga kazi yake ni kutengeneza nishati mwilini kwa maana hiyo wanga hutengeneza sukari, na tayari wewe una kisukari, basi hautakiwi ule wanga mwingi, sasa hapa cha kufanya ni kula kiasi kidogo cha pilau ili kuepuka utengenezwaji mwingi wa sukari mwilini.

 

Upawa mmoja tu wa pilau, nyama kidogo na mboga za majani au kachumbari na samaki kwa wingi hivyo ndiyo unavyotakiwa kula kila mlo wako, hakikisha unakula kiasi kidogo cha wanga, na kiasi kikubwa au kingi cha mboga za majani.

 

Sasa leo napenda kuwakumbusha ni vitu gani mtu wenye kisukari anatakiwa kuviepuka. Kama tujuavyo kuwa endapo Kisukari haitadhibitiwa ipasavyo basi inaweza kuleta madhara mengi kama kupata kiarusi, upofu, matatizo ya moyo, vidonda ndugu, matatizo ya figo na ini, kwa wanaume kukosa nguvu za kiume, matatizo ya misuli na kadhalika.

 

Wenye kisukari wanatakiwa kufanya yafuatayo, jambo la kwanza ambalo mara nyingi napenda kuwakumbusha watu wenye kisukari kuwa ni muhimu sana kujikubali, kuwa una tatizo la kisukari inakuwa rahisi sana kubadili mfumo wa maisha uliyokuwa unaishi kabla ya kupata tatizo.

 

Jambo la pili ni kuepuka kabisa kutumia vitu ama vyakula vinavyoweza kupandisha sukari yako kwa haraka, vitu kama soda, juisi, keki, sukari, asali, chokoleti na vitu vya kupunguza hasa hasa ni vyakula vya wanga.

 

Tunda liliwe kwa muda, saa moja baada ya chakula. Jambo la tatu ni kuepuka kupata vidonda kwa kuwa kama hujaweza kudhibiti kisukari ni rahisi sana kidonda kuchelewa kupona. Kwa wanawake, epuka kuvaa viatu virefu kwa sababu vinazuia damu kufanya mvunguko wake wa kawaida

Comments are closed.