Ulega Aitaka Temesa Kuja Na Tathmini Chanya Ujenzi Vivuko Vipya
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kufanya tathmini ili kujua athari chanya zitakazopatikana kwa jamii kutokana na ujenzi wa vivuko vipya sita vinavyoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Akikagua ujenzi huo katika Karakana ya Songoro jijini Mwanza Waziri Ulega amesema Serikali kupitia TEMESA imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa Vivuko vipya sita na ukarabati wa vivuko vingine vitano.
Amesema vivuko hivyo licha ya kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi pia vitachochea ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu (TEMESA), Lazaro Kilahala, amevitaja vivuko vipya vinavyoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni kuwa ni Kivuko cha MV. UKEREWE kitakachotoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza ambako kinakwenda kukiongezea nguvu kivuko MV. UJENZI ambacho kimeonekana kuzidiwa na wingi wa abiria wanaovuka kati ya maeneo hayo.
Kivuko kingine kipya ni MV. KOME II kitakachotoa huduma kati ya Nyakarilo na Kome Halmashauri ya Wilaya Buchosa, Kivuko hicho pia kinakwenda kukiongezea nguvu kivuko cha MV. KOME ambacho kimeonekana kuwa kidogo kutoka na kuongezeka kwa abiria katika maeneo hayo.
Kilahala amesema kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Buyagu na Mbalika Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza pia kiko katika hatua za mwisho kukamilika ambapo eneo hilo awali halikuwa kivuko.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Sengerema Hamis Tabasamu amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa Vivuko kwani vitakwenda kunusuru vifo vya wananchi ambao walikuwa wakivuka kwa mitumbwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro, Major Songoro amesema kuwa wataanza kutoa vivuko vipya kuanzia mwezi Machi mwaka huu.