Ulimwengu: Nitafunga Mabao Ya Kutosha Yanga

MSHAMBULIAJI wa Rayon Sports ya nchini Rwanda, Mrundi, Jules Ulimwengu, amefunguka kuwa kama mpango wake wa kujiunga na Yanga utakwenda sawa, basi atahakikisha anafunga mabao ya kutosha katika kila mchezo kama alivyokuwa akifanya kwenye Ligi ya Rwanda.

 

Mrundi huyo ana rekodi nzuri ya mabao katika Ligi ya Rwanda kufuatia msimu uliopita kuweka kambani jumla ya mabao 30 katika mechi 32 alizocheza huku akifunga mabao matatu kwenye michuano ya Cecafa Senior Challenge mwaka 2019.

 

Inaelezwa Yanga imefanya mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo kwa ajili ya kumuongezea kwenye safu ya ushambuliaji wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu ujao na michuano ya Kombe la FA.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ulimwengu alisema kuwa ikiwa dili lake la kutua Yanga litakwenda sawa basi kazi yake itakuwa ni kuhakikisha anafunga mabao katika kila mchezo atakaoweza kucheza kwa lengo la kusaidia timu.

 

“Nadhani kitu kikubwa ambacho nakiona ni kuona naweza kufunga mabao katika kila mchezo kwa sababu hilo ndilo jambo ambalo limesababisha wao kuongea na wakala wangu, sasa lazima nihakikishe nawapa kile ambacho wanakitaka kutoka kwangu kwa ajili ya timu.

 

“Kwanza sioni sababu ya kuhofia kitu chochote kwa sababu kama nimeweza kufanya vizuri nikiwa Rwanda kwenye timu ya Rayon, kwa nini nishindwe huko? Kwa sababu ninachokiangalia ni jinsi gani naweza kufikia malengo ya timu na yangu binafsi katika kila mchezo kwa kuona timu inafika mbali,” alisema Ulimwengu.


Loading...

Toa comment