The House of Favourite Newspapers

Ulinzi Waimarishwa Mchezo Wa Yanga Vs CBE New Amaan Complex Zanzibar

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Elisante Mmari

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Elisante Mmari amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama limejipanga vizuri kuhakikisha linaimarisha ulinzi katika mchezo wa kimataifa wa mpira wa miguu utakaokutanisha timu ya Yanga dhidi ya CBE SA ya nchini Ethiopia.

ACP Mmari ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari Madema, Zanzibar.

Amebainisha kwamba, mchezo huo utakaochezwa leo Septemba 21, 2024 katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar majira ya saa 2:30 usiku kwamba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama watahakikisha ulinzi unaimarishwa kabla, wakati na baada ya mchezo huo kumalizika.

Amesema uzoefu unaonesha kuwa wahalifu hutumia michezo ya kimataifa kama fursa ya kufanya vitendo vya kihalifu, hivyo Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia kwa mujibu wa sheria watakaobainika kufanya vitendo vyovyote vya kihalifu ikiwemo uvunjifu wa amani.

Aidha, ametoa onyo kali kwa madereva wa vyombo vya moto ambao hutumia michezo hiyo kuwa fursa ya kuvunja sheria za usalama barabarani, kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mchezo huo ni hatua ya kufuzu hatua ya makundi kwenye Mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika 2024/2025

MO AWAITA MASTAA AWEKA DAU NONO-CHAMA KUIPELEKA YANGA MAKUNDI-FEI TOTO AZUA BALAA