Umafia! Simba Yamalizana na Beki Aliyekubaliana na Yanga

IMEELEZWA kuwa beki wa Klabu ya Polisi Tanzania, Idd Mobby, amemalizana na mabosi wa Simba kwa kusainishwa dili la miaka miwili ili kuitumikia timu hiyo.

 

Awali iliripotiwa kuwa, Mobby tayari alishamalizana na Yanga, na kilichokuwa kimebaki ni kumalizana na uongozi wa Polisi Tanzania kwani mchezaji huyo bado ana mkataba nao.

 

Mobby mwenyewe alikiri kuwa: “Ni kweli Yanga nimeshazungumza nao na tumemalizana na waliniambia nisubiri muda wowote watamalizana na klabu yangu ya Polisi.”

 

Lakini kabla hata Yanga haijamalizana na Polisi Tanzania, mabosi wa usajili wa Simba wanadaiwa kufanya umafia kwa kumtorosha mchezaji huyo usiku wa manane wakitaka kumsainisha.

 

Chanzo cha kuaminika kimeeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa juhudi za Yanga na Azam FC za kuipata saini ya Mobby zikakwama maana tayari Simba wameingia wazima-wazima na kumtorosha kambini mchezaji huyo.

 

“Mimi nilikuwa nafahamu wazi kabisa kuwa klabu ambayo ilikuwa imeingia miguu yote ni Azam FC, wengine walikuwa ni Yanga, ila ghafla mambo yalibadilika jioni ambapo tulimkosa Mobby ghafla kambini na tulipoulizia tulisikia kuwa kuna viongozi wa Simba wameondoka naye.

 

“Hadi muda huu ninapoongea na wewe Mobby hayupo kambini na wachezaji wenzake na kwamba simu zake zote zimezimwa, hivyo hata mimi napata wasiwasi kabisa kama watakuwa si Yanga au Azam waliomficha basi ukweli Simba watakuwa wamefanya umafia huo,” kilisema chanzo chetu.

 

Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwalo,  alisema: “Taarifa za Mobby kufichwa na Simba sisi hatuna isipokuwa ni kweli aliomba ruhusa maana ana matatizo ya kifamilia.

 

“Kubwa ninachoweza kukwambia mchezaji bado ana mkataba na sisi, hivyo yyyote anayemhitaji anatakiwa kuwasiliana na klabu yetu ili tumalizane, hivyo nikutoe wasiwasi tu kwamba, Mobby hawezi kwenda Simba wala Azam FC,” alisema Lukwalo.

 

Dirisha dogo la usajili limefunguliwa Desemba 16, mwaka huu na litafungwa Januari 15, mwakani.

Chanzo: Championi

Toa comment