UMAFIA! WATEKA MTOTO WAPATELI FEDHA WAOANE

DAR ES SALAAM: Watu wawili waliotajwa kuwa ni wachumba waliofahamika kwa majina ya James na Happy wakazi wa Kivule jijini Dar wanadaiwa kumteka mtoto kisha kumlazimisha mama yake atoe pesa ili wamrudishe la sivyo wanamuua.

 

Tukio hilo la kustaajabisha lilitokea mwanzoni mwa wiki iliyopita maeneo ya Kimara jijini Dar ambapo inaelezwa kuwa, utekaji huo ulifanyika wakati mtoto huyo wa kike akitokea shule.

Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo aliyefahamia kwa jina la Tina alisema: “Siku ya tukio mwanangu alienda shuleni kama kawaida lakini muda wa kurudi tukachelewa kwenda kumfuata.

 

Dada alipofika shuleni hakumkuta, akarudi na kuniambia kamkosa. Ikabidi mimi niende pale shule na kumpigia simu madam, madam akaniambia mtoto ameshachukuliwa na dada. Kwa kuwa dada alikuwa hajamchukua, ikabidi tuanze kumtafuta kwa majirani na ndipo kuna mtu mmoja akatuambia mtoto alichukuliwa na dada mmoja.

 

“Ikabidi twende kutoa taarifa kwa mjumbe, serikali ya mtaa na msikitini. Huko wakatuambia tusubiri baada ya masaa 24 ndiyo twende polisi. Kesho yake ndiyo tukaenda polisi Oysterbay, tukatoa maelezo, wakatupa RB. Ilipofika mchana wale watu waliomteka mtoto wakanipigia simu na kuniambia wao ndiyo wanaye, wakanipa nikaongea na mwanangu kisha wakasema ili wamrudishe niwatumie shilingi milioni 52, laa sivyo baada ya masaa 48 watamuua, nikawaambia sawa.

 

“Cha ajabu aliyekuwa amemteka mwanangu ni mtoto wa binamu yangu, nimekaa naye kwangu kwa miaka minne, nimemlea na kumsomesha. Basi siku hiyo waliponipigia na kuomba pesa, nikaenda polisi kutoa taarifa, polisi wakaniambia niwape namba ya simu waliyotumia, wakai-track na kubaini kuwa anayeitumia yuko Mbagala.

 

“Baada ya muda walipoicheki tena wakaona anayeitumia yuko Kivule. Wakati polisi wakiendelea kufuatilia, wale watu wakanipigia tena simu, wakaniuliza kama pesa nimeshaipata, nikawaambia bado, wakakata simu.

 

“Wakanipigia tena wakasema kama sijapata hiyo pesa watamuua mtoto wangu, nikawaambia sijapata bado hela subirini. Mara ya mwisho waliponipigia wakaniambia nisipotoa hiyo hela mtoto wangu watamtoboa macho, kumuua na kumtupa kisha wataniambia walipomtupa.

“Kwa kweli nilichanganyikiwa sana, na hivi nilivyo mjamzito nilitamani kwenda leba siku hiyo. Sasa baada ya kukaa siku 5, leo (Ijumaa iliyopita) ndiyo mtoto amepatikana akiwa na nguo zake zilezile. Kwa kweli nalishukuru sana Jeshi la Polisi,” alisema mama huyo.

 

Ikaelezwa kuwa, mtoto aliyekuwa ametekwa alipoulizwa maisha aliyokuwa akiishi huko alikokuwa kwa siku hizo tano alisema, alikuwa akila vizuri, kuogeshwa kisha kulala na Happy.

 

Mama wa mtoto alizidi kusimulia kuwa, alipokutana na mtuhumiwa (Happy) na kumuuliza kwa nini alifanya kile alichokifanya alisema eti ni shetani tu kampitia na kwamba aliyemshawishi alikuwa ni mchumba wake.

 

“Happy ambaye ana mimba ya miezi mitano anasema eti alishawishiwa na mchumba wake ambaye alikuwa anatafuta pesa ya mahari, kwa hiyo alikuwa akitaka hiyo milioni 5 ili 3 atoe mahari na zinazobaki wapate za matumizi.

 

“Hata mchumba wa Happy nilipoongea naye anasema eti na yeye ni shetani tu amempitia, yeye shida yake ilikuwa ni hizo milioni 5. Kikubwa nashukuru tu kwamba nimempata mwanangu akiwa hai maana nilikuwa na hali mbaya sana,” alimaliza kusema mama huyo.

 

Kufuatia tukio hilo la kutekwa kwa mtoto huyo na kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Jolisi, Amani lilifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Mussa Athuman Taibu lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

 

Hata hivyo gazeti hili linatoa tahadhari kwa wazazi kuwa makini na watoto wao kwa kuhakikisha wapo salama kila wanapokuwa kwani utekaji umekuwa ukitumiwa kama njia ya baadhi ya watu kujipatia pesa haramu.
Toa comment