Umekata Tamaa ya Kuolewa, Soma Hapa Ufarijike!

JUMAMOSI nyingine mpenzi msomaji wa safi hii tunakutana kwenye uwanja wetu huu wa kuelimishana, kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo maisha ya uhusiano.

Maisha ya uhusiano yana nafasi kubwa sana katika maisha yetu kwani uwekezaji wake unatoka moyoni.

 

Moja kati ya matarajio makubwa ya binadamu yeyote aliyeko na anayetaka kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi huwa ni suala zima la ndoa. Ndoa ndiyo kilele cha mafanikio ya uhusiano wowote ule wa mapenzi.

Hiyo inatokana na nini; mbali na kuwa mnahalalisha suala zima la kiimani lakini pia ndoa huwaletea heshima katika jamii. Mtu akisikia fulani ni mke au mume wa mtu, kuna ‘kaheshima’ fulani kanaongezeka tofauti na yule mtu ambaye hana ndoa.

 

Tatizo ambalo limekuwa likiwasumbua watu wengi katika suala zima la ndoa ni kutopata mtu sahihi. Mwanaume au mwanamke anatamani kuingia kwenye ndoa lakini anakosa mtu sahihi wa kuanzisha naye ukurasa huo mpya wa maisha.

 

Kila anayeingia naye kwenye uhusiano anakuwa mzinguaji. Si mtu mwenye nia ya dhati ya kuingia kwenye ndoa. Matokeo yake anamchezea kwa muda fulani kisha anamuacha. Matokeo yake anajikuta amepotezewa muda na kuachwa kwenye mataa.

 

Muda unapozidi kwenda hapo ndipo majuto yanapoanza kuongezeka. Hilo liko kwa pande zote mbili lakini limekuwa likiwatesa zaidi jinsi ya kike.

Wengi sana wamekuwa wakikata tamaa ya kuolewa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika mahusiano yao.

 

Inafika wakati binti anaamua tu kutamka ‘sitaki hata kusikia kitu kinachoitwa ndoa.’ Sanasana utakuta anahaha kupata angalau mtoto ili kujiliwaza.

Anaamini mtoto huyo ndiyo atakuwa faraja yake. Atakuwa kipozeo chake cha mawazo pindi atakapokuwa na mawazo ya mume. Akimuona mtoto basi anajisikia amani moyoni.

Marafiki, unapoona hilo linakutokea wala hauna sababu ya kukata tamaa. Usiumizwe na suala la kuona wenzako wameingia kwenye ndoa na wewe huna, subiri tu wakati wako.

 

Achana na kuwa na mawazo kwamba sijui umri sahihi umekupita, kwamba ulipaswa kuingia kwenye ndoa sijui mathalan na miaka 20 hadi 25, nani kasema ni sheria?

Hakuna muda maalum wa kuingia kwenye ndoa bali upo muda muafaka wa wewe kutekeleza jambo hilo sawasawa na mapenzi ya Mungu.

 

Wakati wako upo. Usiwe na presha, uwe na amani ya roho na ya mwili. Jiweke tu kwenye mazingira ya kuwa mke wa mtu.

Jiulize unataka kuwa mke wa mtu, una heshima? Una roho ya upendo? Una hofu ya Mungu? Huna gubu? Sio mwepesi wa kukata tamaa na maisha?

Unatambua kwamba maisha ni shida na raha, uzima na ugonjwa? Ukishajitathimini na kupata majibu basi ni wakati wako wa kujisahihisha pale ambapo unaona haujakamilika.

 

Rekebisha tabia zako, rekebisha mwenendo mbaya na uwe kwenye wakati mzuri wa kuolewa halafu mwisho sasa kwa imani yako umuombe Mungu akupe mume mwema.

Muachie yeye atende, wewe kazi yako ni kuomba. Omba bila kuchoka maana Mungu ana wakati wake wa kukujibu. Usiumie kuona majibu yanachelewa, wakati wako utafika na wewe mwenyewe utashangaa.

Utajiuliza wewe ndiye yule ambaye ulikuwa na wasiwasi? Mbona mambo yamekuwa rahisi na wewe unaitwa mke wa mtu?

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

 

 

 

 

Loading...

Toa comment