Umemsikia Hussein Machozi…. Life yake elimu tosha kwa wasanii!

 

Kwa ajili yako naimbaa,

Sauti hii sikiaa,

Habari hii pokeaa,

Ni kionjo tu cha Ngoma ya Kwa Ajili Yako ya Hussein Machozi ambaye ni mmoja kati ya wakali wa Bongo Fleva kuwahi kutokea Bongo.

Machozi alikuwa kichwa hasa kwenye muziki mwanzoni mwa miaka ya 2000, mbali na ngoma hiyo alitikisa na nyingine kibao kama vile Hello, Promise pamoja na Utaipenda.

Kwa muda sasa staa huyu amepotea kwenye ramani ya muziki na kuna picha zilikuwa zikimuonesha akila bata nje ya nchi.

Risasi Mchanganyiko limefanikiwa kumpata na kufanya naye mahojiano Exclusive na katika makala haya anafunguka kama yoote;

 

 

 

Risasi: Kwa kipindi kirefu umepotea kwenye muziki sababu ni nini?

Machozi: Ukisema nimepotea unakosea, nimekaa kimya yaani sijatoa ngoma kwa sababu ngoma zangu bado zinapigwa na wanaopiga hata hawanipi shilingi kumi bado wanaendelea kufaidi muziki wangu mzuri, kwa hiyo nimetulia nina maana yangu lakini siyo kwamba nimeacha muziki hapana nipo bize natengeneza albamu ambayo natarajia kuiachia hivi karibuni.

 

Risasi: Maisha ya huko Italia unayaonaje?

Machozi: Nayaona ya kawaida tu kwa sababu tayari nimeshazoea japokuwa mara ya kwanza ilikuwa inaniwia vigumu sana kuishi mazingira ya huku na mtihani mkubwa ulikuwa chakula na lugha lakini kwa sasa hakuna kinachonisumbua nimeshapata chakula nachokiweza basi sasa burudani tu.

Risasi: Huko kuna kiki katika muziki?

Machozi: Hakuna kabisa yaani ukiona msanii kasema kitu au kafanya kitu basi ujue kweli kimemtokea hawana drama kama tunavyofanya Wabongo.

 

 

 

Risasi: Ulishafikiria kuomba uraia wa huko wa moja kwa moja?

Machozi: Nitakaaje nchi ya watu halafu nisiwe raia wa huku jamani mimi ni raia wa huku ila siwezi kusema kama ni moja kwa moja au la ila ni raia wa huku na ni Mtanzania Pia.

Risasi: Unakumbuka nini kwenye Bongo Fleva?

Machozi: Vingi sana, manyanyaso kwa sababu Bongo Fleva haijanipatia mafanikio kihivyo zaidi ya manyanyaso tu na kusujudia watu kitu ambacho kinauma sana.

 

Risasi: Ushafanya kolabo na msanii yoyote kutoka huko?

Machozi: Yeah wengi sana na wote mtawafahamu albamu yangu itakapotoka maana ndiyo ina kila kitu humo.

Risasi: Ulikutana wapi na huyo Mzungu wako?

Machozi: Tulikutana kwenye sherehe ya rafiki yangu huku Italia ndiyo nikamwelewa mtoto nikaona nafaa kuishi naye.

 

Risasi: Anaelewa Kingereza au Kiswahili?

Machozi: Bwana wee hapo ndio nilipata shida mtoto hajui Kiswahili wala Kingereza lakini nikasema wacha nioneshe kuwa mimi ni Mbongo haswa sishindwi kitu nikamuonesha ishara pale zile kibubu bubu mara hee mtoto kashaingia laini yaani hadi sikuamini kama alinielewa kuna muda naona kama Mungu tu alimleta.

 

 

 

Risasi: Inasemekana huyo Mzungu amekuzidi umri na ndio anakulea yaani wewe marioo je, ni kweli?

Machozi: Wanaosema hivyo wanajua mimi na mke wangu tuna miaka mingapi? Nimemzidi miaka sita halafu anilee kwani mimi sina mikono wala miguu ya kutoka na kwenda kupambana na maisha eti kisa naposti sana nipo nyumbani na mtoto wangu basi sina kazi najua kinachowasumbua ni wivu Wabongo tuna wivu na chuki.

 

Risasi: Vipi kuhusu familia yako huku Bongo?

Machozi: Nilikuwa na familia yangu Tanzania na tuliishi vizuri tukiwa na malengo mazuri tu lakini uvumilivu ulimshinda mwenzangu akaanza kufanya mambo ya ajabu wakati mimi nimekuja huku kutafuta maisha mwisho wa siku nikasikia ameolewa, basi nikawa sina cha kufanya na niliumia zaidi aliposema mtoto pia sio wangu ni wake peke yake wakati tumelea wote tangu anazaliwa mpaka anafikisha miaka mitatu iliniuma sana ila nikamjibu tu sawa nikaamua kuendelea na maisha yangu.

Risasi: Mmeshafunga Ndoa?

Machozi: Ndio sisi ni wanandoa ila tulikubaliana kutoweka pabliki labda mpaka nimuulize kama naweza kutoa picha za ndoa nisije nikatoa halafu mwisho wa siku mnasikia nimefungwa na mke wangu (anacheka) si unajua Wazungu walivyo itakuwa noma.

Risasi: Umezaa naye watoto wangapi?

Machozi: Mmoja tu wa kike anaitwa Miya binti yangu mzuri sana na nina mpenda mno.

SHAMUMA AWADHI

Loading...

Toa comment