Umeamua Kuoa/ Kuolewa, Basi Achana na Ujana!

Na GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| XXLOVE

NIANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa vitu vyote kwa kunifanya niione tena Sikukuu ya Pasaka ya jana. Bila shaka nawe msomaji wa safu hii utakuwa umesherehekea vizuri bila kokoro yoyote.

Nikupe pole wewe ambaye unasumbuliwa na matatizo kadha wa kadha, kikubwa usikate tamaa na usiache kumshirikisha Mola katika matatizo na furaha yako. Naomba nijikite moja kwa moja kwenye mada ya leo yenye lengo la kuwatahadharisha vijana ambao wanaamua kuoa au kuolewa wakiwa katika umri mdogo wa ujana.

Ndoa ya ujanani si jambo baya na wala si dhambi, ni nzuri na ina raha yake kwa sababu mnaanza kufaidi penzi lenu mkiwa vijana, watu wazima hadi uzee endapo mtajitunza na Mungu akiwatendea mema. Lakini ili mpite hatua zote hizo ni lazima mjue kuwa mtakutana na kila aina ya changamoto, migogoro na mitafaruku mbalimbali kwenye penzi lenu. Kuna wakati mtagombana, mtanuniana, mtafukuzana na mambo mengine mengi yafananayo na hayo.

Kama hutatumia hekima, uvumilivu na akili ya ziada kujua mweza wako hapendi kipi na anapenda kipi, kamwe hamuwezi kufika uzeeni mkiwa pamoja kama wanandoa. Ninachokiona kwa vijana wengi wa sasa ni kuamua kuoana wakiwa vijana lakini wengi akili zao zinakuwa bado hazijajiandaa na suala la ndoa. Kwa kifupi, wengi ni
wakurupukaji.

Mbaya zaidi, wengi wanashindwa kubadilisha akili zao kutoka kwenye tabia na maisha ya ubachela au ujana kuwa tabia za uanandoa au ufamilia.

Tabia za mke na mume siyo uhuni kama enzi za ujana. Wakati mwingine unaweza kusema ni heri vijana wasioe au kuolewa wakiwa bado vijana na badala yake waone wanapofikia umri fulani hivi kwa sababu watakuwa wamejitambua, watakuwa wamemaliza kuhangaika na kupigwa na maisha vya kutosha, hivyo watakapooana watatulia kwenye ndoa.

Nasema hilo kutokana na baadhi ya vijana, iwe wa kike au wa kiume, kuoana wakiwa vijana, lakini mwisho wa siku wanashindwa kuishi kama wanandoa kwa sababu kila mmoja damu yake bado inachemka, akili yake bado inatamani mambo ya ujana.

Kwa mfano; mwanamke unakuta bado anatamani kwenda kukata mauno kwenye ngoma za Mdundiko, Kibaokata, kwenye Msambwanda, klabu au vigodoro. Vivyo hivyo kwa mwanaume naye bado ana akili ya kuendelea kukaa vijiweni na washikaji kwa ajili ya kupiga soga, bila kujua kuwa familia inahitaji kula, kuvaa na kulala.

Mwanaume unakuta bado hajaacha tabia yake ya kwenda klabu kujirusha bila kujali kuwa kwa wakati huo ni baba wa familia, ameungana na mwenzake, hivyo ni hatari kufanya mambo ambayo yataudhi upande wa pili.

Kama umeolewa au kuoa ukiwa ni kijana wa umri wa miaka 23 au zaidi, unapaswa kujirekebisha kitabia, lazima uchukue, uishi na uige tabia za baba au mama mwenye familia bora siyo ilimradi umeoa au kuolewa tu! Kwa kufanya hivyo itakusaidia kwani si umeamua kuingia kwenye ndoa?

Basi lazima akili ya ujana na utoto isiwe nyingi kuliko ya utu uzima. Kama utaongoza na kuishi kwa tabia zako za ujanani basi muda si mrefu ndoa itakushinda. Unakuta mwanaume anajielewa kama baba wa familia, lakini mkewe bado yeye anajiona kama mdada wa kazi kwenye ndoa yake, hivyo anafanya mambo ya wasichana na siyo ya kifamilia.

Halikadhalika kwa kijana wa kiume, unakuta mwanamke anajitambua na kuishi kama mama wa familia bora kwa maana ya kutimiza na kushiriki mambo muhimu, lakini mwanaume ni jipu, hajitambui, hajielewi kama ni kichwa cha familia.

Kwa maoni na ushauri tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_ na_uhusiano au unaweza kujiunga na M&U WhatsApp kwenye namba 0679 979 785.


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment