Umeshaona kuna vikwazo, ya nini kulazimisha penzi?
MUNGU ni mwema, mpenzi msomaji wa safu hii. Ni Jumamosi nyingine tunakutana katika safu hii na kuweza kupata darasa la uhusiano kama kawaida yetu.
Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita tulijifunza kuhusu tatizo la watu wengi kupishana na waoaji na waolewaji. Tuliweza kupata elimu kuwa watu wengi wanashindwa kuheshimu hisia za watu ambao wana kiu ya kweli ya ndoa na kujikuta wakiangukia katika mikono ambayo si salama.
Tukirudi katika mada yetu ya leo iliyopo hapo juu, inatufundisha kukubaliana na matokeo hasi.
Siku zote watu ni wagumu kukubaliana na ukweli unaouma. Mtu anaona kabisa anakoelekea kuna giza lakini wapi, hakubali tu. Anajifariji kwa kusema eti giza hilo ni ishara ya ushindi. Anakubali kuteseka kwa muda mrefu akiwa na matumaini kuwa ipo siku atafarijika.
Ndugu zangu, tunapaswa kujiongeza pale tunapokutana na vikwazo katika maisha yetu ya uhusiano. Mifano ipo mingi ya vikwazo ambavyo katika hali ya kawaida huwezi kusogea mbele.
Kama mtu ameshakwambia ana mtu mwingine, anampenda zaidi kuliko wewe, kwa nini usikubaliane na matokeo?
Mbaya zaidi, huyo mtu aliyekuambia kwamba ana mtu mwingine, wana mikakati ya kuoana, wewe bado hukubali. Eti unapambana kurudisha nyuma akili ya mtu.
Mwenzako ameshapeleka posa sehemu nyingine, kwa mtu mwingine, wewe bado unapigania awe wako. Ni akili au matope?
Msingi wa kung’ang’ania ni nini? Hadi kufikia hatua ya kupeleka posa kwa mtu mwingine, jua tayari ameamua kukuweka wewe pembeni.
Hakuna sababu ya wewe kuumia. Usihangaike maana huwezi kumbadili, kubaliana tu na matokeo usonge mbele.
Mfano mwingine, ndiyo kwanza unaanzisha uhusiano. Unakiona kikwazo cha dini. Mwenzako ni imani tofauti na wewe. Mnalijadili na kuona kuna ugumu kwake na kwako kubadili dini. Kila mmoja ana msimamo kwa ndugu zake, hawezi kubadili.
Mnatafakari kuhusu uwezekano wa nyinyi kufunga ndoa ya bomani, pande zote mbili haziafiki, nyinyi pia hamuafiki. Mnabaki kuvutana, huyu anataka hili huyu hataki. Unaanza kulazimisha mambo ambayo kimsingi yatakuletea matatizo.
Eti ngoja twende hivyohivyo halafu tutajua mbele kwa mbele. Kwa nini ukubali kuanzisha safari ambayo unajua haina mwanga mzuri mbeleni. Kwa nini usiteseke leo kwa kufanya maamuzi magumu kabla hujazama penzini?
Kama umeona dini ni kikwazo mbona una nafasi ya kusubiri umpate yule ambaye mtaendana imani. Ni busara zaidi kulitafakari suala la dini mapema kabla hamjafika mbali. Lipeni kipaumbele suala hilo kwani mkiliacha liende tu, athari zake ni kubwa huko muendako.
Kama muafaka umekosekana, ni vyema kila mmoja akamruhusu mwenzake aendelee na maisha yake. Kila mmoja hataumia kwa kuwa ndiyo kwanza mnaanzisha uhusiano kuliko pale mtakapokuwa ‘mmeshashea’ vitu vingi maishani.
Mfano mwingine waweza kuwa umegundua mwenzako hana tabia njema. Labda pengine ni mwizi, jambazi au mvuta bangi. Umeshahangaika namna ya kumbadilisha tabia hiyo imeshindikana. Anakwambia umuache na maisha yake na kama unamhitaji basi ukubaliane na tabia yake.
Kwamba uvumilie uvutaji bangi au ikiwezekana na wewe uvute ili muendane. Hicho ni kikwazo. Unapaswa kukiepuka mapema. Usilazimishe kitu ambacho unaona kitakupa maumivu mazito huko mbeleni. Kiepuke mapema!
Hivyo ni baadhi ya vikwazo, najua wewe mwenyewe msomaji ukijitathimini vizuri utakuwa unaviona vikwazo vingi ambavyo vinakwamisha uhusiano wako kusonga mbele.
Unaona kabisa hakuna suluhisho lakini unazidi kuteseka bila sababu, amua sasa kuepukana navyo, uwe huru na utampata mwingine ambaye mtaendana.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!