The House of Favourite Newspapers

Umewahi Kujiuliza kwa Nini Hupendwi

TUPO kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kuwa pamoja nasi na kututia nguvu kwa yale yote tunayoyafanya.Karibuni jamvini tuendelee kupeana elimu na ujuzi wa uhusiano wa kimapenzi na maisha kwa jumla.

Kama swali la mada hii linavyouliza, wapo wengi ambao wamekuwa wakiniuliza, wakitaka kujua ni wapi hasa huwa wanakosea na kujikuta wakichezewa, kupotezewa muda kisha kuachwa wakiwa hawana hili wala lile. Katika hali kama hiyo, wengi huishia kusema kuwa hawana bahati ya kupendwa au wana nuksi linapokuja suala la mapenzi!

Hapa ndipo wengi huishia kudanganywa na kujikuta wakitafuta suluhisho kwa kwenda kwa sangoma na kuelekezwa wakaoge maji ya bahari! Kisha huliwa fedha zao na kuishia patupu! Rafiki, kumbuka wajinga ndiyo waliwao!

Jiulize, je, una umri wa kutosha kuwa na mpenzi? Ungependa kumpata mtu anayekuvutia? Je, unahisi umegonga mwamba kumpata mwenza sahihi? Umechoka kuchezewa na kupotezewa muda kisha kuachwa? Je, ni kwa nini hupendwi?

Kama kweli unataka kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi ulio imara na ungependa kumfahamu mwenza sahihi, kabla ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, unapaswa kuwa makini mno na kuzingatia mambo ambayo yatakusaidia kuufanya uhusiano wako uwe imara na wa kudumu na ili upendwe;

MOSI

Jifunze kuwa na adabu au tabia njema wewe mwenyewe. Ukweli ni kwamba, huwezi kuwa na upendo kama huna tabia njema. Ni kawaida sana kumsikia mtu akisema; ‘Mimi ninavutiwa sana na mpenzi mwenye adabu juu ya mambo madogomadogo na hata makubwa na si kwangu tu, bali hata mbele ya rafiki na ndugu zangu.’

Mwingine utamsikia; ‘Mimi huchukizwa sana na mtu ambaye hata kabla ya kuanza mapenzi huniuliza una miradi gani? Nadhani swali hilo laweza kukupa picha kwamba tabia ya mtu huyo ikoje! Huyo anajali zaidi maslahi, kaa mbali naye.’

PILI

Tunza usafi wako wa kuwaheshimu wengine na kujiheshimu mwenyewe. Ukijiheshimu, lazima wengine watakuheshimu. Kwa upande mwingine, ukipuuza usafi huo, utapoteza nafasi ya kumvutia mtu anayehitaji kuwa na wewe. Heshimu mdogo na mkubwa, huo ndiyo msingi wa maisha!

TATU

Jifunze jinsi ya kuzungumza na watu. Mazungumzo yako yawe yenye mvuto na siyo ya kukera au yaliyojaa kisirani. Msingi wa uhusiano wa kudumu ni mazungumzo chanya. Mazungumzo yako yawe yametiwa munyu. NDIYO yako iwe NDIYO na HAPANA iwe HAPANA!

Mara nyingi utasikia mtu akisema; ‘Wengine huvutiwa sana na mambo wanayoyaona kwa mtu, lakini mimi ninavutiwa sana na mambo ninayoyasikia kwa mtu. Mara nying mtu hunena mambo yaujazayo moyo wake!’ Maana yake ni nini? Kupitia mazungumzo, waweza kabisa kumjua mtu huyu ni wa aina gani, je, anafaa au hafai?

NNE

Kama ikitokea ukahisi kwamba mtu unayependezwa naye anaweza kuwa mwenza wako mzuri hadi kwenye ndoa, usichelewe, mwambie kwamba unapendezwa naye. Eleza hisia zako waziwazi na moja kwa moja japokuwa hilo laweza kukuogopesha kutokana na hofu ya kukataliwa. Lakini unapochukua hatua ya kwanza, unaonesha umekomaa na ni mtu jasiri.

Katika hilo, heshimu uamuzi wa mtu. Kama anasema hataki muwe na uhusiano, basi kubaliana na hilo kisha tafuta ‘chimbo’ lingine, usiwe king’ang’anizi.

TANO

Baadhi ya watu huhisi kwamba ni jambo rahisi kumfanya mtu akupende na kuchezacheza michezo hiyo bila mpangilio. Kumbuka mtu anayewachezea wengine kimapenzi hutumia lugha tamu na ishara za mwili zinazoamsha hamu ya ngono kwa muda tu. Mtu kama huyo hana nia ya kufuatia uhusiano wa kimapenzi unaoheshimika. Ukiwa na tabia hii huwezi kupendwa, shughulikia mambo haya yatakufanya kupendwa na kila mtu hata kama siyo kimapenzi.

Kwa leo ninaishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwenye namba hapo juu au tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa kwenye Facebook.

Comments are closed.