The House of Favourite Newspapers

Umezalishwa, Kila Mtoto Na Baba Yake? Soma Hapa!

0

KILA kukicha unapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila hatua unayoipiga na kukutana nayo katika maisha yako ya kila siku. Shukrani kwako msomaji ambaye umekuwa ukinitumia ujumbe na kunipigia simu kwa ajili ya kutoa maoni yako juu ya mada mbalimbali ninazozileta hapa.

 

Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, ni ukweli usiopingika kwamba wanawake walio wengi hukumbana na changamoto nyingi katika maisha ya uhusiano. Lakini kwa sababu Mungu amewajalia uvumilivu, mara nyingi wamekuwa wakishinda, wakisimama imara na mwisho wanafanikiwa katika maisha yao.

Kama wewe ni mwanamke ambaye umezalishwa watoto kadhaa na kila mtoto ana baba yake, basi mada hii inakuhusu! Kwa mfano; wewe ni mama wa watoto wanne na kila mtoto wako ana baba yake, lakini mwisho wa siku unaishi maisha ya ajabu ya mateso kwa sababu wazazi wenzako, hawana msaada wowote kwako.

 

Kama mzazi mwenzako au wazazi wenzako hawana ushirikiano wowote na wewe, jiuliza mara mbili-mbili, inawezekana ukawa na matatizo wewe mwenyewe au wao wamekuona wewe ni shamba la bibi au inawezekana wewe ndiye ulijilengesha kwa mwanaume f’lani kwa sababu ya muonekano wake au kuhisi pengine kuna kitu unaweza kunufaika au kuolewa kabisa na mwisho ukafanikiwa kuwa sehemu ya urithi wake.

 

Kama wewe ni miongoni mwa wanawake ambao wamezalishwa na mwanaume au wanaume halafu ukaachwa ni lazima ukubaliane na ukweli wa hicho kilichotokea. Unapokubali ukweli inakufanya uweze kufungua akili yako kwa kufanya mambo mengine kuliko kuendelea kulalamika au kulialia.

 

PAMBANA Pamoja na kuwa ulifanya kosa kubwa la kuruhusu kila mtoto kuwa na baba yake bila kujali mazingira ya kuzalishwa na wanaume tofauti, ni lazima ujikubali kisha upambane na hali yako ili uweze kuwasomesha watoto wako.

 

Kama umezalishwa na wanaume wengine halafu unaona hawana muelekeo wa kukusaidia, ni jukumu lako sasa kuhakikisha unapigana huku na kule ili uweze kuwasomesha watoto wako. Kama akili yako itaendelea kuwategemea wanaume wako ambao hawana msaada wowote kwako na kwa watoto wako, utafeli katika maisha yako na watoto wako wataishi kwenye maisha magumu.

 

Siku zote makosa ndiyo yanaweza kukufanya kuwa imara na mwenye nguvu na mafanikio kwa sababu unajua ni wapi ulijikwaa, ukataka kuteleza au ukateleza kabisa. Usikubali kushindwa au kulia kwa sababu umetelekezwa, pambana usiku na mchana ili uweze kufikia malengo yako. Siku zote mwanamke ni mtu mwenye nguvu sana katika jamii na ndiyo maana maendeleo ya wanaume wengi waliofanikiwa, basi nyuma yao kuna wanawake wao.

 

Ni kweli unateseka na watoto wako, lakini usichoke, huo ni mtihani ambao umeupata hivyo ni lazima uushinde, ukikubali kushindwa, basi ndiyo umejimaliza katika maisha yako. Kwa leo naomba niishie hapa, ninaamini kuna jambo utakuwa umelipata katika makala haya. Kwa maoni; tembelea Facebook Page:mimi na uhusiano, Insta:@ mimi_na_uhusiano au jiunge na Mi&u WhatsApp kwa namba zilizopo hapo juu.

XX LOVE NA GABRIEL NG’OSHA

Leave A Reply