The House of Favourite Newspapers

UN Yaisaidia Somalia Baada ya Mafuriko Mabaya

UMOJA wa Mataifa (UN) umetuma misaada ya dharura nchini Somalia kufuatia mvua kubwa ambazo zimenyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kusababisha mafuriko.

 

Misaada hiyo imetumwa hasa katika wilaya ya Beletweyne ambapo taarifa zinasema watu zaidi ya 270,000 wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kuharibika katika mafuriko.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP linashirikiana kwa karibu na wizara inayohusika na masuala ya kibinadamu na majanga nchini Somalia na pia mashirika mengine ya serikali.

Tayari WFP imetuma helikopta kusaidia shughuli za kibinadamu kati ya Beletweyne na sehemu zilizo karibu zilizoathiriwa vibaya na mafuriko kutoka Mto Shabelle.

WFP ina mpango wa kusaidia familia 4,000 kutoka vijiji saba kwenye wilaya ya Beletweyne. Pia itapeleka tani 24 za biskuti kwa njia ya helkopta, ikifanya safari kadhaa kwenda Beletweyne.

Karibu tani 20 za biskuti zimesafirishwa kutoka Mogadishu kwenda Baidoa kwa njia ya barabara na pia kwenda mji wa Bardale ulio kusini magharibi, kwa njia ya ndege.

Mvua kubwa zisizo za kawaida na mafuriko yamezidi kuzikumba Somalia, Sudan Kusini na Kenya mwaka huu. Watabiri wa hali ya hewa wanatarajia mvua hizo kubwa zitaendelea kunyesha hadi Desemba.

Comments are closed.