The House of Favourite Newspapers

UMUHIMU WA KULA TENDE WAKATI WA MFUNGO

LEO katika makala haya, yataangazia ulaji wa tende, na kwa kuzingatia kuwa huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tende ndiyo tunda pekee linaloliwa kwa wingi na Waislamu, pengine kuliko tunda lingine lolote. 

 

Mtu aliye kwenye mfungo, mara zote huwa kiwango chake cha sukari mwilini hupungua na kutakiwa airejeshe tena kwa kula vyakula vitakavyosaidia kufanya hivyo mara tu anapotakiwa kufuturu. Aina ya kwanza ya sukari itumikayo mwilini ni ya glukosi. Lakini sukari inayoshuka kwa watu ambao hawajala wala kula kwa muda mrefu, inaweza kuwasababishia kupatwa na kizunguzungu au kulegea.

 

Hivyo basi, ulaji wa tende mara mtu anapotakiwa kufuturu, humfanya aliyefunga asijihisi kuchoka sana na huwa na nuru zaidi ya macho. Pia tende zitamsaidia kuimarisha na kuboresha mfumo wa usagaji wa chakula tumboni, hivyo ataondokana na matatizo ya ukosefu wa choo au matatizo ya kupata choo kigumu kinachosababisha maumivu wakati wa kujisaidia.

 

Mfungaji akila tende zitamsaidia kupata virutubisho vya ‘amino acids’ ambavyo ni muhimu mwilini, pia mwili wake utapata aina mbalimbali za madini na vitamin za kutosha, ambazo zinapatikana kwenye tunda hili maarufu ambalo lina kiasi kidogo cha mafuta yasiyo na lehemu. Sukari inapoliwa kwa njia ya chakula au kinywaji, mara zote viwango vya glukosi ya mwili hujisawazisha yenyewe na kumfanya mlaji aliyefunga asijihisi.

Ingawaje tende mara nyingi si chakula kinachopendelewa sana na watu wenye njaa, lakini ndicho chakula kisicho na mafuta na ni chanzo madhubuti cha sukari. Mfungaji akila tende, atajipatia kiasi cha kutosha cha protini na vitamin B1, B2, B3, B5, A1, na C, virutubisho ambavyo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya mwili kwa ujumla.

 

Wale walio kwenye mfungo, muda wa kufuturu ukiwadia, wanashauriwa pia kuchanganya tende na maziwa halisi kisha wale. Na kama wanajisikia uchovu, badala ya kunywa vinywaji baridi vinavyodaiwa kuongeza nguvu, wale tende hata punje tatu tu zinatosha.

 

Tunawashauri kuanza kufungua kwa kula tende ili kuurejeshea mwili nguvu iliyopotea kwa siku nzima. Kwa sababu tende pia ina madini aina ya potasium na kiasi kidogo cha chumvi. Madini haya husaidia uimarishaji wa mishipa ya fahamu.

 

Ulaji kiasi wa madini ya potasium husaidia kumwepusha mtu na maradhi ya kiharusi. Pia tende husaidia kupunguza lehemu mwilini. Mfungaji mwenye tatizo la kukauka damu mwilini (anemia), anaweza kupata ahueni kwa kula tende kwa wingi ambayo ina kiwango cha kutosha cha madini ya chuma ambayo huhitajika katika utengenezaji wa damu mwilini.

 

Wakati vitu vingine vitamu vinadaiwa kuwa huozesha meno, lakini utamu wa tende huzuia uozaji wa meno. Kwa mtu aliye na tatizo sugu la kukosa choo, anatakiwa kuloweka tende za kutosha kwenye maji kiasi cha lita moja kwa muda ili kupata juisi nzito, muathirika anywe na atapata choo laini.

Kwa matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume, mchanganyiko maalum wa tende, maziwa, asali na unga wa hiriki vinaweza kuondoa tatizo hilo. Chukua kiasi cha kiganja kimoja cha tende, loweka kwenye maziwa ya mbuzi kiasi cha lita moja, ziache zilowane kisha zisage kwenye maziwa hadi zichangayike, weka vijiko vitatu au vinne vikubwa vya asali pamoja na nusu kijiko cha chai cha hiriki, kisha kunywa mchangayiko huo kila siku hadi utakapoona mabadiliko ya kuridhisha.

 

Tende ni dawa ya wale wenye matatizo ya wembamba wa kupindukia na wanataka kuongeza uzito, ulaji wa tende kila siku unaweza kuwasaidia. Lakini hii ina maana wale wanaohitaji kupunguza uzito, ulaji wa tende kwa wingi hauwezi kuwafaa. Tende husaidia pia kuondoa hali ya ulevi kwa wale wanaokunywa pombe.Tunda hilo husaidia pia kuimarisha nuru ya macho na tatizo la kutokuona usiku.

Comments are closed.