The House of Favourite Newspapers

Unending Love -74

2

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.
Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa msichana huyo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.

Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India.

Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Wanafunga safari ya kurejea Tanzania huku mara kwa mara Anna akitafuta upenyo wa kumpa mapenzi Jafet. Hatimaye nafasi inapatikana na wawili hao wanajikuta wakiwa peke yao chumbani, kwenye hoteli waliyofikia.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Jafet! Nakupenda sana mwenzio na leo naomba unifurahishe moyo wangu, naomba unipe haki yangu,” alisema Anna na kuanza kuvua blauzi aliyokuwa ameivaa, akaitupa pembeni na kuhamia kwenye suruali, nayo akaivua na kuitupa.

“Hapana Anna! Noo,” alisema Jafet baada ya kumuona msichana huyo akimalizia kuvua nguo zilizokuwa zimesalia lakini tayari alikuwa amechelewa. Anna akiwa kama alivyoletwa duniani, alimvamia Jafet pale kitandani huku akionesha kudhamiria kutimiza azma yake.

Jafet akiwa bado hajui afanye nini, Anna tayari alikuwa kifuani kwake, akamkumbatia kwa nguvu huku akipumua kwa nguvu mithili ya mtu aliyetoka kukimbia mbio za Marathon, mikono yake laini ikibarizi sehemu mbalimbali za mwili wa Jafet. Japokuwa Jafet alijitahidi kujitoa kwenye mtego huo, kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo na yeye alivyojikuta uzalendo ukimshinda, taratibu akaanza kulegea.

Taratibu na yeye akaanza kuonesha ushirikiano, wakagusanisha ndimi zao na kuanza kujivinjari kwenye ulimwengu tofauti kabisa, huku Anna akionesha kuzidiwa zaidi na hisia za huba.

“Nakupenda sana Jafet, nakuomba unisamehe kwa yote niliyokufanyia, nisamehe mpenzi wangu,” alisema Anna huku akilengwalengwa na machozi, Jafet akawa anagugumia kwa sauti ya chini akimbembeleza na kumhakikishia kwamba amemsamehe kwa yote yaliyotokea.
“Niambie kama kweli unanipenda kama mimi ninavyokupenda.”

“Wewe mwenyewe unajua ni kwa kiasi gani nakupenda, unajua jinsi nilivyoumia ulipoamua kwenda mbali nami, nakupenda sana Anna,” alisema Jafet na kuanza kumwagia mabusu mfululizo msichana huyo sehemu mbalimbali za mwili wake, naye akawa anajibu mapigo.

Dakika chache baadaye, maandalizi yalikuwa yamepamba moto huku kila mmoja akionesha kuwa tayari kwa pambano hilo la kirafiki, lisilo na jezi wala refa. Kilichokuwa kinasubiriwa ilikuwa ni kipyenga tu kuashiria kuanza kwa pambano hilo.

“Ngo! Ngo Ngo!” sauti ya mlango wa chumba cha Jafet uliokuwa unagongwa ndiyo iliyowazindua wawili hao kutoka kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa, harakaharaka wakakurupuka na kuachiana kwani muda wote walikuwa wamegandana kama ruba.

“Jafet! Jafet!” sauti ya baba yake Anna ilisikika vizuri ndani ya chumba hicho, ikabidi Anna achukue nguo zake na viatu, akakimbilia kwenye bafu la ndani na kujifungia kwa ndani huku akitetemeka mno.
Jafet naye alikurupuka na kuokota taulo lake chini, akajifunga na kuvaa fulana kwa juu, akaenda kufungua mlango huku akijilazimisha kuvaa uso wa kichovu kuonesha kwamba alikuwa amelala.
Ili kumtoa wasiwasi baba yake Anna, Jafet alifungua mlango wote ili aone kwamba Anna hakuwepo ndani ya chumba hicho.

“Samahani kwa kukusumbua, vipi ulikuwa umelala?”
“Ndiyo, usingizi ulikuwa umeanza kunipitia,” alidanganya huku akijilazimisha kupiga miayo.
“Eti Anna yuko wapi? Naona namgongea mlango wa chumba chake lakini inaonekana umefungwa,” alihoji baba yake Anna huku akiingia ndani ya chumba cha Jafet.

“Kuna muda nilimsikia anasema anataka kwenda kununua ‘ice cream’, labda ametoka nje.
“Huyu mtoto mbona anapenda kutusumbua? Akipatwa na matatizo huko nje itakuwaje? Haya wewe pumzika, kama akija mwambie namtafuta,” alisema baba yake Anna, akatoka kisha Jafet akafunga mlango kwa ndani, akashusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake. Harakaharaka akaenda kugonga mlango wa bafuni alikokuwa amejificha Anna.
“Amesemaje?”

“Anakutafuta sana, jiandae ukamsikilize, nimemdanganya kwamba umeenda kununua ice cream,” alisema Jafet, ikabidi Anna aanze kuvaa nguo zake harakaharaka kwani hakutaka baba yake ashtukie kilichokuwa kinaendelea.

“Lakini Jafet mwenzio nina hali mbaya, si unaniona?”
“Usijali Anna, nenda kwanza kamsikilize baba nakusubiri, mi mwenyewe si unaniona nilivyo na hali mbaya?” alisema Jafet, wakakumbatiana na kubusiana, Anna akasogea kwenye meza ya kujipambia (dressing table) chumbani humo, akajiweka vizuri kisha akafungua mlango taratibu na kuchungulia nje.
Alipohakikisha hakuna anayemuona, alitoka na kuelekea nje harakaharaka, akatoka mpaka getini na kuzugazuga kisha akarudi chumbani kwake. Ile anashika kitasa cha mlango tu, alisikia sauti ya baba yake akimuita.

“Ulikuwa wapi Anna, mbona unatupa kazi ya kukutafuta kama mtoto mdogo?”
“Nilikuwa na hamu ya ice cream baba nikaenda kuangalia nje.”
“Ukitoka uwe unaaga, unatupa wasiwasi.”
“Nilimuaga Jafet,” alisema Anna huku ndani ya moyo wake akijipongeza kwani uongo wake uliendana kabisa na wa Jafet.

“Mama yako anakuita, anasema anataka mlale pamoja, itabidi mimi ndiyo nilale kwenye chumba chako,” alisema baba yake Jafet na kusababisha msichana huyo aishiwe kabisa nguvu. Akakosa cha kujibu zaidi ya kuelekea kwenye chumba alichokuwemo mama yake.

“Nataka kulala na wewe mwanangu, nimejisikia tu leo,” alisema mama yake Anna, kauli iliyoonesha kumtomfurahisha Anna lakini hakuwa na cha kufanya. Kwa shingo upande akakubali kulala na mama yake huku mawazo yake yote yakiwa kwa Jafet, kumbukumbu za walichokuwa wanataka kukifanya muda mfupi uliopita zikawa zinapita ndani ya kichwa chake kama mkanda wa video.

Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwa Anna, kuna wakati alikuwa anatamani kumtoroka mama yake na kwenda chumbani kwa Jafet lakini kila alipokuwa akitingishika kidogo kitandani, mama yake alikuwa akimzungumzisha ili aelewe kwamba hakuwa amelala.

Hatimaye siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi wote wakawahi kuamka na kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea uwanja wa ndege kwa ajili ya kupanda ndege ambayo ingewapeleka mpaka jijini Mwanza.
Saa moja juu ya alama tayari walikuwa wamewasili uwanja wa ndege, baada ya kukamilisha taratibu zote, waliingia mpaka ndani na kukaa sehemu ya abiria kusubiria usafiri. Nusu saa baadaye, tayari walikuwa ndani ya ndege, kila mmoja akiwa amekaa kwenye siti yake.

“Mbona kama huna furaha Anna?”
“Wewe unafikiri kilichotokea usiku nimekifurahia?”
“Lakini mimi sina makosa, isitoshe bado tunayo nafasi kubwa tukifika Mwanza,” alisema Jafet kwa sauti ya chini, kauli iliyomfurahisha sana Anna, akaachia tabasamu pana na kumuegamia Jafet begani. Muda mfupi baadaye, ndege waliyopanda ilianza kuondoka na safari ya kuelekea jijini Mwanza ikapamba moto.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

 

2 Comments
  1. Hussein hassani says

    mweeeee

  2. alex rodrick says

    safi jamaa ana zari kweli anakata mawingu

Leave A Reply