The House of Favourite Newspapers

UNA UHAKIKA ANAKUPENDA KWA DHATI?-2

KATIKA mada hii ambayo imeanza wiki iliyopita, tunajifunza namna ya kumtambua mwenzi ambaye amepoteza uwezo wa kupenda.  Tayari tumeshaona dalili za awali katika sehemu ya kwanza ya mada hii. Sasa tunamalizia vipengele vilivyosalia.

Bila shaka baada ya kuona vipengele hivyo, utakuwa unajua upo na mpenzi wa aina gani na kwa nini ana mabadiliko ya hapa na pale katika uhusiano wenu.

TUENDELEE…

(IV) MTU WA WASIWASI

Mara zote amekuwa na wasiwasi, hapendi mkae sehemu za uwazi, anafikiria juu ya kuachwa, huku utumwa mkubwa zaidi ukiwa ataificha wapi aibu yake siku na wewe ukimwambia utamwacha.

Ana hofu na uhusiano wenu, hana amani na ni kama yupo mguu nje, mguu ndani. Yupo kituoni akisubiri kuachwa muda wowote. Siyo kwamba umemwambia unamwacha, ila ana hofu moyoni mwake kutokana na makovu aliyokuwa nayo huko nyuma.

(V) HAPENDI MAHABA

Anachukia michezo ya kimahaba, hapendi utani wa kimapenzi na kumwambia unampenda kila wakati. Ni mwoga pia wa surprise. Kwake mapenzi ni kama karata tatu, kwa hiyo hawezi kujiachia sawasawa kwako.

(VI) ANAPENDA KULIA

Ukimuudhi kidogo, machozi yanashuka machoni mwake. Unaweza kushangaa kosa dogo tu, mwenzio analia, sababu kubwa hapa ni kwamba, halizwi na kosa lako, analizwa na makosa ya wapenzi wake wa nyuma.

Imani yake ni kwamba, machozi yake yanaweza kuwa furaha. Ndiyo mkombozi wake na pengine humsaidia kupunguza hasira iliyojaa kifuani mwake. Halii kwa kosa lako la mara moja au mbili pekee, bali huwaza juu ya wengi waliomkosea huko nyuma.

(VII) ZAWADI MARA NYINGI

Kwa kuwa anajihami na hana uhakika na anachokifanya, anaweza kuwa mtu wa zawadi mara kwa mara. Unaweza kushangaa kwa wiki akakupa  zawadi zaidi ya mara mbili. Haamini ni njia ipi ya kuboresha penzi, kwa kuogopa kuachwa, anahisi kukupa zawadi nyingi ni kukushika vyema.

(VIII) ANAPENDA KUTULIA NA WEWE

Anapenda kukaa na wewe muda wote, akuangalie machoni na ikiwezekana usitoke kabisa kwenda nje. Kama anajua siku yako ya mapumziko, atahakikisha anawahi asubuhi ili kukufanyia kila kitu.

Anaogopa ukienda nje, ni rahisi kukutana na wajanja zaidi yake, ambao wanaweza kukuzuzua na kumsahau! Anaamini zaidi katika kukuchunga. Anajua akiwa na wewe muda mwingi ni rahisi zaidi kukuchunga.

(IX) ANATISHIA KUKUACHA

Kosa dogo tu, anaweza kukuambia: “Kama vipi tuachane, siwezi kuendelea na wewe tena.” Ukitulia na kupima kosa la kukuambia hivyo hulioni, kinachomsumbua hapo ni uwezo wa kupenda.

Ana hasira na muda wote anawaza kuachwa, sasa angalau anataka kuweka historia kwamba safari hii hajaachwa, bali ameacha! Kubwa zaidi hataki kuumiza sana moyo wake, maana tayari ameshajihisi yeye ni wa kuonewa tu. Hataki kuruhusu kuonewa tena, anataka kuibuka mshindi katika vita ya kutoswa na kutosa! Anataka kukutosa!

(X) ANAKUELEZA UKWELI

Akishindwa yote kabisa, anaweza kuamua kukueleza ukweli wa mambo, kwamba anahisi hakupendi. Angalau hii ni nzuri zaidi, maana utakuwa umeujua ukweli na kazi yako hapo sasa itakuwa ni kuhakikisha unatibu tatizo lake.

Kumbuka kwamba si kwamba hakupendi bali hana uwezo wa kupenda! Lakini hii ni angalabu sana kutokea, wengi hawasemi, vitendo vyao vitaongea. Kusema huwa ni hatua ya mwisho kabisa. Kwamba baada ya kuhangaika kukufanya vituko vya hapa na pale kwa muda mrefu bila mafanikio, basi hufikia uamuzi wa kusema ili uelewe kilichopo.

Hapo hutakiwi kukasirika. Kama ulikuwa unahisi tu, bas sasa utakuwa umeshajua kinachomsumbua kwa uhakika kabisa. Kazi yako ni kumhakikishia kuwa unampenda kwa dhati, yupo moyoni mwako na kwamba ameingia kwenye uhusiano sahihi. Hakuna jambo kubwa analohitaji mwanamke kama kuwa kwenye uhusiano salama. Ukiweza kumuonyesha hilo tu, basi mwanamke wako atakuwa kwenye himaya yako siku zote… utafurahia uhusiano wako kwa hakika.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandikia vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Sasa anaandaa kitabu cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

 

Comments are closed.