The House of Favourite Newspapers

Unachodhani Hakiwezekani, Niamini Mimi, Kinawezekana!

NIMEBAHATIKA kusoma kitabu kimoja kiitwacho The Seven Secrets kilichoandikwa na mwandishi ambaye pia ni mchungaji, John Hagee. Ndani ya kitabu hiki nimepata kujifunza vitu vingi sana kuhusiana na mafanikio lakini yapo maneno ambayo huwa yananivutia sana yaliyopo mwanzo kabisa mwa kitabu hiki.

 

Anaeleza kuwa, hatma ya kuyafikia mafanikio ipo ndani ya imani zetu sisi wenyewe. Kama unaamini ipo siku utatoka katika kiza cha umaskini na kuingia katika nuru ya mafanikio na utajiri, basi upo sahihi.

 

Pia kama unaamini mafanikio yapo kwa ajili ya watu flani tu hivyo mtu kama wewe kuyafikia ni sawa na ndoto za alinacha, upo sahihi.

Labda nikuulize wewe msomaji wangu kwamba, hivi mara ya mwisho kufanya kile kisichowezekana ilikuwa ni lini? Ni lini uliacha kujaribu kufanya jambo fulani kwa sababu watu wengi, ndugu, rafiki na hata jamaa zako wa karibu walikwambia hilo unalotaka kulifanya kamwe halitawezekana?

 

Ninachojua ni kwamba, kuna maelfu ya mambo kadha wa kadha katika maisha yako ya kila siku ambayo mpaka sasa bado hujayapa nafasi ya kuyafanya kutokana na kuamini kwamba hayatawezekana, mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine huenda ndiyo yangeleta tofauti kubwa sana katika maisha yako na kwa wengine.

 

Ndugu yangu, ukweli ulio wazi ni kwamba katika maisha kila jambo linawezekana, yaani hakuna kisichowezekana chini ya jua. Unachotakiwa wewe ni kuwa na imani juu ya uwezo wako. Kujitoa kwa dhati pamoja na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kuelekea kwenye utimilifu wa ndoto na malengo yako uliyojiwekea.

Weka imani na nia ya dhati

Waswahili wana msemo wao unaosema, penye nia pana njia. Tambua kwamba penye nia ya dhati ndipo penye njia ya kweli, kamwe usikate tamaa, amini na ishi ndoto zako kwani kila jambo chini ya jua linawezekana.

 

Usikae tu na kulalamika kwa kushindwa kwako kufanikisha hili na lile, kulalamika pekee hakutaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora bali utakuwa unaongeza tatizo juu ya tatizo. Hii ni kwa sababu pale unapolalamika unakuwa unamaanisha kwamba wewe huna uwezo wala nguvu ya kutatua matatizo yako, jambo ambalo ni hatari sana kwani safari ya mafanikio katika maisha huwa inaanza kwa kushika hatamu juu ya maisha yako.

 

Usikae tu na kusema kwamba unataka hiki na kile bali chukua hatua sasa na usiwe mwoga wa kujaribu mambo mapya kwa hofu ya kuja kushindwa, kukataliwa, kuchekwa na hata kukosolewa kwani huko kwenye kushindwa na kufanya makosa ndiyo sehemu sahihi ya wewe kujifunza.

 

Hivyo basi chukua hatua sasa katika kuelekea kwenye malengo na ndoto zako, kwani mpaka sasa tayari una rasilimali zote muhimu unazopaswa kuwa nazo ili kuweza kufanikisha ndoto na malengo yako katika maisha.

Ninaposema tayari una rasilimali zote muhimu unazopaswa kuwa nazo, nina maana ya kwamba tayari una mitaji mitatu muhimu na ya kipekee ambayo ni watu, akili na muda.

Uwe na ndoto kubwa

Unapoamua kuwa tofauti na wengine katika maisha, unapoamua kuwa na ndoto kubwa katika maisha basi tarajia kukumbana na vikwazo vya kila aina pamoja na kukatishwa tamaa. Ni lazima utakumbana na changamoto na vikwazo vyenye lengo la kuona ukishindwa kufanikisha ndoto na malengo yako uliyojiwekea.

 

Ni lazima pia utakutana na watu watakaokukatisha tamaa kwa kukwambia hilo unalotaka kulifanya kamwe halitawezekana. Na sababu kubwa ya wengi kukwambia hivyo ni kutokana na fikra hasi za kushindwa walizonazo.

Ndugu yangu, yawezekana wewe ni mwanafunzi unayesoma kwa malengo ya kuja kuwa Rubani wa Kimataifa, basi tambua kuwa hilo linawezekana kabisa! Pengine lengo ni kuja kuwa mwanasiasa mashuhuri hadi kufikia ngazi ya uraisi wa nchi, amini pia linawezekana. Haijalishi upo katika familia maskini kiasi gani

kwani ukijaribu hata kufuatilia historia za watu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali utagundua wametoka katika familia za hali ya chini sana. Hivyo kama wao waliweza, kwa nini wewe ushindwe? Pambana na ishi ndani ya ndoto zako.

 

ZINGATIA HILI

Ota ndoto kubwa, ishi ndoto yako na amini kwamba kila jambo linawezekana na kama unashindwa kuamini hilo basi tazama hapo nyuma kwa kuangalia na kufuatilia historia za watu wengi walioweza kufanya mambo makubwa, mambo ambayo yalisemekana hapo kabla kuwa hayatawezekana ila yakawezekana.

Huwa najifunza vitu vingi sana kupitia kwa mmoja wa watu wangu wa mfano (role model) Erick Shigongo. Kwangu mimi huyu ni mmoja wa mashujaa wakubwa sana kwani kutoka kwenye kuitwa majina mabovu kama vile madaso, malazi na mengineyo mabaya zaidi, alipambana sana na leo hii anaitwa majina kama vile mheshimiwa, bosi, mkurugenzi. Haikuwa kazi rahisi lakini naamini hata yeye aliamini kuwa inawezekana na kweli imewezekana, wewe utashindwaje? Amka na chukua hatua sasa!

Makala hii imeandikwa na mmoja wa wasomaji wangu Joseph Charles Moshi ambaye tangu naanza kuandika makala za maisha na saikolojia amekuwa akinifuatilia hadi leo.

Comments are closed.