The House of Favourite Newspapers

Unachotarajia kwa Mpenzi Wako, Ukikikosa Moyo Huumia Sana!

Na GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| XXLOVE

PENZI msomaji ni matumaini yangu kuwa umzima wa afya njema na karibu tena kwenye Jumatatu nyingine murua kabisa. Leo kwenye safu hii pendwa ya XXLove ambayo ni mahususi kwa kupeana elimu ya mapenzi na maisha kiujumla, tunajikita kwenye kuangalia matarajio ya wengi wanapoingia kwenye uhusiano huwa ni nini na kama matarajio hayo yakikosekana ni nini hutokea?

Ifahamike kuwa katika uhusiano wowote ule, watu wawili wanapokuwa pamoja, wanakuwa tayari katika akili zao wamejenga matarajio au matumaini ya kunufaika na uhusiano husika.

Inapotokea wakakosa kile walichokitarajia, basi moyo huumia sana. Moyo unapokosa ulichokitarajia, hata maana ya kuwa na uhusiano hupotea na kukata tamaa iliyojaa kila aina ya maumivu.

Ndiyo! Moyo huumia kwa sababu hujutia kudanganyika. Ngoja tutumie mfano wa mama mzazi ambaye huonesha upendo mkubwa kwa mwanaye tangu tumboni hadi anapokua mtu mzima.

Unajua matarajio ya moyo wa mama kwa mwanaye yanakuwa ni yapi? Ukweli ni kwamba, endapo mtoto huyo akikua na kushindwa kukidhi matarajio ya upendo wa mama ambayo ni kumjali kwa kuonesha upendo uleule na kumtunza, upendo huo hubadilika na kuwa laana ya mzazi.

Hapa ndipo moyo wa mama huumia kupita kiasi, kwamba hujikuta akiwaza mambo mengi juu ya namna alivyohangaika na mwanaye huyo, lakini matarajio yake yanakuwa hayajatimia. Kama mzazi aliyepitia uchungu, huumia sana! Ndiyo. Huumia kwani hana moyo wa chuma. Ana moyo wa nyama kama wewe.

Vivyo hivyo, kwenye uhusiano wa mwanamke na mwanaume, kila mmoja huwa na matarajio yake. Yanapokosekana huwa ni maumivu makubwa. Unaweza ukajiuliza matarajio hayo yanaweza kuwa ni yapi? Ni kusaidiana katika shida na raha.

Kubebeana matatizo, yawe ya kiafya, kiuchumi, kifamilia au yoyote yale. Ni kujengeana heshima kwenye jamii na kusaidiana kufikia malengo ya juu ya kimaisha. Kujenga familia yenye siha bora, upendo na furaha.

Inapotokea mpenzi wako akashindwa kukusapoti katika hali yoyote kati ya hizo, swali la kwanza huwa ni je, ana faida gani? Ogopa sana swali hilo anapojiuliza mwenza wako. Maana yake ni kwamba huna msaada hivyo hakuhitaji.

Unajua baada ya kuwepo kwa hali hiyo nini hufuata? Anayejikuta ameshindwa kupata kile alichokifuata kwa mwenza wake, hujikuta kwenye tafakuri kuntu. Hukosa usingizi na furaha.

Hutafakari faida na hasara za kumkosa mwenza wake huyo katika maisha. Anapoona faida ni nyingi kuliko hasara hasa akilenga kutafuta heshima kwa jamii, basi kinachofuata ni kutafuta pengine pa kupooza maumivu kwani huona ndiyo suluhisho pekee la kufikia matarajio yake. Mpenzi msomaji wangu, hisia za kimapenzi si jambo la kucheza nalo kwani ni jambo la msingi. Hisia za kimapenzi hazipaswi kupuuzwa hata kidogo.

Tambua kwamba mwenzako angependa akuone unajali hisia zake. Kama hilo halipo kwenye uhusiano au halipewi kipaumbele, linaweza kusababisha mengine yote kuharibika. Zaidi sana, kumbuka wewe na mpenzi wakoni watu wa jinsi tofauti, kinachowafanya muungane kiasili ni hizo hisia za kimapenzi kati yenu.

Tafakari na nakusihi ukarekebishe penye hitilafu katika uhusiano wako. Zaidi sana uwe bora leo kwa mpenzi wako kuliko ulivyokuwa jana! Kwa maoni, ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.

Comments are closed.