The House of Favourite Newspapers

UNAFANYA NINI ZAIDI YA KUMWAMBIA NAKUPENDA?

JAMBO la kufurahisha ni kwamba, ukifungua ukurasa huu, unakuwa na uhakika wa kuongeza kitu kipya katika maisha yako ya kimapenzi. Hata kama huna mpenzi kwa sasa, utajiwekea mazingira mazuri ya kupata mwezi sahihi siku zijazo.  Ok! Sasa turudi kwenye mada yetu. Ni somo muhimu sana kufahamu kwa wanandoa na ambao wanatarajia kuingia kwenye ndoa. Kabla ya kwenda mbali zaidi, hebu tujiulize, unaposema; nakupenda, unamaanisha nini?

Tulia kwa muda, tafakari… mpenzi wako anapokuambia anakupenda, unafikiri nini zaidi kichwani mwako? Wengi huishia kufikiri kirahisirahisi tu, kuwa anampenda fulani au mwezi wake anampenda! Je, umewahi kujiuliza, unampenda mpenzi wako kwa kiwango gani? Je, yeye anakupenda kwa kiasi gani? Upendo wake unamaanisha nini hasa? Upendo wako kwake una maana gani? Ni pendo la ndani kweli au tamaa za mwili?

Unaweza kujiuliza, inawezekana vipi, ukampenda mtu hadi mkafikia kuingia kwenye ndoa, bado ikawa ni tamaa ya ngono tu? Hapa namaanisha kuwa yawezekana vipi, mpendane halafu muingie ndani maelewano yaondoke? Heshima itoweke? Upendo utoweke? Inawezakana vipi? Wengi wanajiuliza: “Tumependana na mume wangu kwa miaka mingi, tumeingia kwenye ndoa na tumeishi humo kwa siku nyingi lakini kwa nini leo hii nimuone amebadilika?”

KUPENDA NA KUPENDWA

Kitu cha msingi ambacho unatakiwa kujifunza hapa ni kwamba, pendo la dhati huishi ndani. Penzi huwa haliishi, halina muda maalum wa kuishi ndani ya mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kama ulimpenda miaka 20 iliyopita kwa dhati ya moyo

wako, basi leo huwezi kumchukia. Upendo ukishaingia ndani ya moyo wa mtu hubaki humo milele, ila kuna mambo madogomadogo au pengine yanaweza kuwa makubwa, yanayoweza kusababisha kuahirisha upendo kwa muda. Nasema kuahirisha kwa sababu hauwezi kuondoka. Ndugu zangu, ujue wazi kuwa, hadi mwenzi wako ameamua kuungana na wewe katika ndoa, si bahati mbaya. Hajabahatisha, bali amekuchagua kutoka kwa wengi.

Kama ndivyo, kwa nini penzi liondoke ghafla? Haiwezekani. Kwa maana hiyo, sasa ni wazi kuwa, penzi huharibiwa na sisi wenyewe. Kuna mambo ambayo yakifanyika hupunguza nguvu ya mapenzi na mwisho wake kusababisha matatizo kama nilivyoeleza hapo juu.

KWANZA JITAMBUE

Lazima ujitambue, ujue nafasi yako kwa mwenzako kisha uhakikishe unasimama sawasawa. Usipojitambua hutaona thamani ya mapenzi, hutaona umuhimu wako kwenye ndoa. Muunganiko wenu hautakuwa wa maana kama hutatambua thamani yako. Lazima mwanamke asimame katika nafasi yake na mwanaume naye asimamie nafasi yake. Kuna baadhi ya watu wakishaingia kwenye ndoa wanaona kila kitu kimeshaisha. Hawaoni umuhimu wa kufikiria kuwa bora zaidi kwenye ndoa.

Ndugu zangu, nyumba inajengwa tena inajengwa kwa umakini wa hali ya juu sana. Huwezi kumuona mwenzako mpya kama wewe mwenyewe hujaonyesha upya katika mambo yako. Mvute mwenzi wako ili akuone kweli unahitaji kuwa mpya, hapo utatengeneza nafasi kwake kubadilika kwenye nyendo zake.

TAFUTA FURAHA YA MWENZAKO

Kati ya mambo yanayoharibu ndoa ni pamoja na kugombana mara kwa mara. Kuna wengine huwa hawawezi kuzungumza sana, kama umemkosea, ataishia kukuambia mara mbili au tatu, baada ya hapo anaamini umeelewa.

Ikitokea ukajua umekosea na mwenzi wako amekujulisha au ukamuona hana furaha, ni jukumu lako kuhakikisha furaha yake inarejea tena. Mpeleleze, jichunguze, ni wapi umekosea? Haraka sana unachukua hatua ya kurekebisha makosa yako. Usiruhusu mwenzako kuwa amenuna muda wote kwa sababu yako. Tafuta amani ya mwenzako.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.