The House of Favourite Newspapers

Unaingilia ndoa ya mwanao unataka akuoe wewe?

0

Habari zenu wasomaji wa makala haya, mimi nimeamka salama, bila shaka wasomaji wangu ni wazima na mnaendelea vema na ujenzi wa taifa hili, kwa wagonjwa nawaombea heri mtapona.

Tunaelekea uchaguzi mkuu siyo vema nikaanza mada bila kuwakumbusha kupiga kura ili kumchagua yule unayeona anafaa na kumbuka kupiga kura ili usije kujutia kuchaguliwa kiongozi na mtu.

Wiki hii nimekuja na mada hii ya mama wakwe wanaopenda kuingilia ndoa za watoto wao ili kuwakumbusha kuwa si vema mtu akishakuwa na mkewe kufuatiliwa kama mtoto mdogo.

Siku zote nimekuwa na mada mpya kutokana na ujumbe mnaonitumia na wengi mmekuwa mkiomba ushauri kupitia mada hizihizi, sasa leo nina ushahidi wa mwanamke mmoja ambaye yuko kwenye ndoa yake kwa mwaka mmoja ila kikwazo ni mama mkwe ambaye hupendelea kuwatembelea nyumbani kwao mara kwa mara.

Hebu msikie mwanandoa huyu analo la kukujuza na kupitia mkasa wake huenda ukajifunza au wewe mama mkwe mwenye tabia hii huenda ukaiacha kwani inawezekana hata huna lengo baya lakini hujui kuwa unamkera mkweo.

“Mimi ni mwanamke niliyefanikiwa kuishi kwenye ndoa yangu kwa muda wa mwaka mmoja, baada ya kuingia kwenye ndoa nilikuwa nahudumiwa na mama mkwe kwa kila kitu nikajua kwa sababu ya upya wa ndoa yangu kwani hata nilipowauliza wenzangu waliotangulia kwenye ndoa waliniambia ni kawaida mpaka zile siku arobaini nikaamua kukaa kimya.

“Kilichosababisha nikaamua kukwambia Bi Chau ni jinsi mama mkwe wangu anavyonifanyia mpaka sasa, naona si sawa akija tu nyumbani kwangu naiona nyumba chungu natamani kuhama mpaka siku anayorudi kwake.

“Kinachonikera zaidi ni jinsi anavyopenda kuingia chumbani kwangu bila woga na kunipangia niishi vipi na mwanaye wakati tayari tupo kwenye ndoa, amediriki kunipangia hata matumizi ya ndani kitu ambacho si sahihi ile ni nyumba yangu na mume wangu.

“Nakumbuka siku moja alimwambia mume wangu kila anachoninunulia na yeye ampe kama ni kitenge kiwe sare, hivi ni sahihi kweli kuvaa sare na mama mkwe wangu? Labda niko tofauti naomba unisaidie, kwenye suala la chakula gani kipikwe nyumbani pia anakuwa mstari wa mbele, nikiamka tu asubuhi ananiambia leo utapika kitu f’lani hela aachiwe yeye mpaka siku anayoondoka,” alisema msomaji anayeitwa mama Bahati mkazi wa Kigogo.

Jamani wasomaji hii ni kero ya msomaji mwenzenu kaniletea mezani nikaona ni bora niwaandikie akina mama wanaojisahau huko mtaani, najua wapo wengi wa aina hii na leo nimeamua kuwapa funzo dogo tu na nitaanza kwa kuwauliza.

Hivi mtoto wako akishindwa kuoa si utamaliza waganga wewe?      

Wazazi wengi hujisifia na kufurahia kuoa kwa watoto wao wakiwa na maana kuwa mtoto sasa kakua na akishapata watoto ndiyo kabisa furaha huwa inakamilika, sasa wewe mzazi unayetamani mwanao kuwa na wewe wakati wote unamaanisha nini?

Leave A Reply