UNAJIHISI MPWEKE? Tiba Yako Ipo Hapa!

MARAFIKI uwanja wetu ni mpana, leo nimeona tugeukie upande wa saikolojia. Nitazungumza na wale wenye upweke mioyoni mwao, nikiamini mwisho wa mada hii kuna kitu wataondoka nacho.

 

Ukamilifu wa binadamu hukamilishwa na changamoto. Ndiyo maana wataalamu wa mambo ya mafanikio wanasema binadamu tumeumbwa kwa ajili ya kutatua changamoto. Hii inamaanisha kuwa siku changamoto zikifikia ukingoni basi na maisha nayo yatakuwa yamefika mwisho.

 

Tazama, wengine wanasomea urubani, wengine udereva, wengine udaktari, wengine ualimu, uandishi wa habari nk. Lengo la kusoma huko ni kwa ajili ya kuja kutatua changamoto baadaye.

 

Hata mume na mke wanapoungana, ni kwa ajili ya kutatua changamoto. Mume atataka kuwa baba, kadhalika mke atapenda kuwa mama, lakini lazima wajiandae kuwa wazazi bora kwa kuhakikisha wanajenga misingi imara kwa ajili ya maisha yajayo ya mtoto wao.

 

Kwa ujumla kukutana na changamoto katika maisha ni jambo la kawaida na linampasa kila binadamu kwa sababu ndiyo ukamilifu wa ubinadamu wenyewe na zaidi maisha. Inawezekana kuna mambo yanakusababishia upweke na kukukosesha amani.

 

Yapo mengi yanayoweza kuwa chanzo cha upweke. Huenda ikawa ni mapenzi, maradhi, umasikini, kusemwa vibaya, kufukuzwa kazi nk. Changamoto ni namna ya kukabiliana nazo au kukaa nazo mbali. Wengi huwa wanashindwa kuelewa cha kufanya wanapokabiliwa na upweke. Je, ufanyaje unapokabiliwa na upweke?

USIKAE PEKE YAKO

Jambo la kwanza kabisa kuzingatia kwa mtu ambaye anakabiliwa na upweke ni kutoruhusu kukaa peke yake muda mrefu. Kukaa mwenyewe kunasababisha kuongeza mawazo juu ya jambo linalokusumbua.

Ili kuepusha hilo au kupunguza ni vema kuwa karibu na watu wengine. Kuwa na wengine kutakufanya uzungumze mambo mbalimbali yahusuyo maisha, siasa, michezo nk, na hivyo kukusahaulisha yanayokusumbua.

TAFUTA MICHEZO

Ikiwa ni lazima kukaa mahali peke yako ni vyema utafute kitu cha kufanya. Inaweza kuwa mchezo wa kwenye simu, kompyuta au chemsha bongo yoyote ambayo itaifanya akili yako ichangamke. Muhimu ni kutokuacha gepu la akili kuacha kufanya kazi na kufikiria changamoto ulizonazo. Mbinu hii ni muhimu sana.

MSHIRIKISHE MWINGINE

Usipende kukaa na jambo kichwani kwa muda mrefu peke yako Kumwambia mwingine kunaweza kukupa ahueni. Jambo la msingi la kuzingatia ni kuhakikisha mtu utakayemshirikisha ni yule unayemwamini. Usimwambie mtu yeyote, kwani kwa wasio wastaarabu ni rahisi kusambaza kwa wengine.

 

Unapomshirikisha mwingine unakuwa umetua mzigo. Unaweza kupewa ushauri kulingana na namna ambavyo mhusika amepata kukutana na changamoto kama hiyo. Kubaki na jambo linalokuumiza muda mrefu ni hatari, kwani unaweza kusababisha kupata madhara makubwa zaidi ikiwemo shinikizo la damu.

TAFUTA SULUHU

Ni jambo gani linalokuumiza? Tafakari kwa kina. Kazi? Maradhi? Umasikini? Ugomvi na ndugu au nini? Kujua tatizo lako ni hatua ya kwanza, lakini kushughulikia ni hatua inayofuata yenye umuhimu zaidi.

 

Kama ni maradhi, waone wataalamu wa afya. Pengine unaweza kuwa unajitesa na mawazo kwa maneno ya mitaani, kumbe kitaalamu huna tatizo kubwa. Kama ni ajira, tafuta mahali pengine; kufukuzwa kazi siyo mwisho wa maisha. Unaweza kujiuliza, unatafutaje?

 

Tumia simu yako vizuri kusaka taarifa za ajira mpya. Kimsingi mwisho wa siku, tatizo lazima litatuliwe. Mwisho wa upweke wako ni wewe kupata jibu la changamoto inayokukabili. Unaweza kupata kwa kuhangaika mwenyewe au kupitia rafiki / marafiki uliowashirikisha.

CHANGAMOTO NI MAISHA

Usivunjwe moyo na changamoto unazokutana nazo, maana ndiyo ukamilifu wa maisha. Mtu yeyote au taasisi yoyote inaweza kukumbwa na changamoto. Usijione wa kwanza. Kuwa na moyo mkuu, huku ukitafuta suluhisho badala ya kuendelea kulalama. Bila shaka somo langu limeeleweka vyema.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.


Loading...

Toa comment