The House of Favourite Newspapers

UNAMALIZAJE MOGOGORO NA MPENZI WAKO ?

LEO tunaangalia mada muhimu sana katika mapenzi, nachambua juu ya migogoro ambayo inaweza kutokea kati yako na mwenzio, je, unaimalizaje? Katika uhusiano wowote, lazima wakati mwingine kutokee kutokuelewana, vivyo hivyo katika uhusiano wa mapenzi lakini tatizo si migogoro, bali ni jinsi gani unavyoweza kutatua migogoro uliyonayo. Hebu jibu swali hili, umewahi kugombana, kulumbana au kuwa na migogoro na mpenzi wako? Jibu lako litakuwa mwanga wa kuwa na uelewa wa kutosha katika vipengele vinavyofuata. Sasa tuanze moja kwa moja kwa kufahamu maana ya migogoro na malumbano.

MIGOGORO

Ni maneno matatu yenye maana zinazokaribiana, ingawa ukweli ni kwamba yana maana tofauti kidogo! Mnaweza kuwa na mgogoro na mwenzi wako lakini yasiwepo malumbano. Kwamba inawezekana mpenzi wako amekukosea na ukawa mwanzo wa migogoro katika penzi lenu, lakini kutokana na uelewa wako na kukubali kosa mapema ikiwa ni pamoja na kuomba radhi, kukawa hakuna malumbano na mambo yakawa sawa. Wakati huo huo, pia kunaweza kukawa na tatizo

linaloweza kusababisha migogoro ambayo huzaa malumbano na mwisho wake sasa hapo ni ugomvi! Naamini tunakwenda sawa! Kwanini nimeeleza hayo? Nataka twende sawa, hatua kwa hatua katika mada hii ambayo naamini ni tatizo kwa wengi walio katika uhusiano. Baada ya kuona maana ya maneno matatu muhimu ambayo kwa hakika yanakaribiana, ambayo tunayajadili katika mada yetu ya leo, sasa tuone jinsi matatizo hayo yanavyotokea.

HUSABABISHWA NA NINI?

Migogoro ambayo nimeianisha hapo juu, haiwezi kutokea bila kuwa na vyanzo. Lazima kuna mambo ambayo yametokea kwanza,

kabla ya tatizo husika kukua na mwisho wake kuanza migogoro, malumbano kabla ya ugomvi. Kama wahusika hawatakuwa makini, mwanzo wa ugomvi ni mwendelezo wa kuachana hapo baadaye, jambo ambalo mwenye mapenzi na akili timamu hawezi kukubali likachukua nafasi. Hebu sasa pitia mambo hayo.

PENZI HUPUNGUA

Yapo mengi ambayo husababisha migogoro katika mapenzi, lakini kubwa zaidi ni kuchuja au kupungua kwa penzi. Unapokuwa na mwenzi wako, halafu kwa sababu ambazo unazijua mwenyewe unajikuta penzi limepungua,

huo unaweza kuwa mwanzo wa migogoro. Kila atakachokiongea utaona kero, kila wakati utakuwa mtu wa kukasirika na usiyependa kufuatwafuatwa! Katika upande mwingine pia, kama mwenzi wako amejikuta akiingia katika ushawishi na penzi lake kwako kupungua, ni mwanzo wa kuwa na mawasiliano mabaya na wewe,

ambayo bila shaka lazima yatasababisha migogoro ambayo huzua malumbano kabla ya ugomvi. Utashangaa mpenzi wako anakununia bila sababu za msingi, hana raha na wewe, hataki mzungumze chochote kuhusu penzi lenu, hapo ujue ni mwanzo wa migogoro.

 MATATIZO BINAFSI

Hili pia linaweza kuwa chanzo cha ugomvi katika maisha ya wapendanao. Mathalani mwenzi wako ametoka kazini akiwa na matatizo binafsi kichwani mwake, wewe kwa kutokujua unaanza kumuuliza kwa ukali. Hebu soma mfano ufuatao: “Unakuja nyumbani umenuna, sijui una matatizo gani? Ndiyo yale yale, ugombane na wanawake zako huko nje, halafu unakuja kuninunia hapa nyumbani.”

Hii ni moja kati ya kauli mbaya sana kwa mpenzi wako kabla ya kujua sababu ya ukimya na upole aliokuja nao. Yawezekana ana matatizo binafsi, kwanini uanze kumhisi vibaya? Tulia, fikiria kwa makini kabla ya kutamka chochote kwa mpenzi wako. Mada hii itaendelea wiki ijayo ambapo tutaangalia kwa kina njia bora za kutatua migogoro na mpenzi wako

Comments are closed.