The House of Favourite Newspapers

Unamsomesha mwanao kwa gharama kubwa ili iweje?

0
Schoolboy Writing in Notebook
Ni wiki nyingine tulivu tunakutana tena kupitia safu hii ambayo inagusia mambo mbalimbali yanayohusu maisha yetu ya kila siku.

Ni safu yako wewe mwenye uchu wa mafanikio, inakuhusu wewe uliyeathirika kisaikolojia unayeshindwa kufanya mambo ya kimaendeleo kutokana na kuwa na msongo wa mawazo.

Kwa maana hiyo kama una jambo lolote ambalo linakutesa, linakukosesha amani na kukufanya ushindwe kuyafurahia maisha yako, usisite kuwasiliana nami kwa namba zilizopo hapo juu ili tuweze kwenda sawa.

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nataka kuzungumzia faida za kuwasomesha watoto wetu na madhara makubwa tunayoweza kuyapata kwa kushindwa kufanya hivyo.
Kila mwenye akili timamu anajua thamani ya elimu katika maisha ya sasa. Ukijaribu kufanya uchunguzi utabaini kuwa, wengi waliofanikiwa wamekwenda shule licha ya kwamba wapo ambao wana bahati zao, hawajasoma lakini maisha yao ni supa.

Kwa kifupi elimu ni kitu cha msingi sana kwa maisha ya binadamu wa leo. Ndiyo maana wapo wanaodiriki kujinyima na kutumia gharama kubwa ili kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule.

Wazazi wengi ukiwauliza wanawasomesha watoto wao ili iweje, watakuambia ili siku wakiwa wamezeeka, wasaidiwe.

Ni kweli moja ya faida ya wazazi kuwasomesha watoto wao ni ili baadaye watoto hao waje kuwa na maisha mazuri na ikiwezekana wawasaidie pale watakapokuwa hawana uwezo wa kufanya kazi.

Lakini je, hayo tu ndiyo pekee yanayowafanya wazazi wengi watilie mkazo katika suala la elimu kwa watoto wao? Huenda wengi wanatarajia hayo lakini kumsomesha mwanao unajiepusha na mambo mengi.

Kukufilisi
Kama ulikuwa hujui, mwanao usipomsomesha anaweza kuja kukuongezea majukumu uzeeni, kukuaibisha na hata kukuua

Ipo mifano mingi ya wazazi waliojikuta wanapoteza mali na fedha zao nyingi kutokana na matatizo ya watoto wao. Ni wazazi wangapi unaowajua ambao wamefikia hatua ya kuuza rasilimali zao ili wakawawekee dhamana watoto wao mahakamani kwa kufanya matukio ya wizi, ubwiaji na uuzaji wa unga?

Kimsingi unaposhindwa kumsomesha mwanao unamuandaa kuja kuwa mwizi au jambazi. Atafanya matukio makubwa ambayo ili kumuokoa utalazimika kutoa pesa zako na kama huna unaweza kujikuta unauza mali zako, bado hajakuingiza kwenye matatizo makubwa na kukupa msongo wa mawazo?
Utegemezi

Usipomsomesha mwanao, akakua akiwa hana muelekeo wa maisha, utafika muda ataoa. Kama wewe mzazi umejenga nyumba yako ni lazima huyu atataka umpe angalau chumba kimoja cha kuishi.

Mbaya zaidi ni kwamba, hata baada ya kumpatia hifadhi atakuwa tegemezi kwako. Utamlisha yeye na mkewe kwa kuwa hana kipato. Zaidi ya yote, akiona maisha yamemuwia magumu usishangae akakimbia na kukutelekezea familia, bado atakuwa hajakuongezea majukumu huyu?

Kwa maana hiyo basi, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunawasomesha watoto wetu kwa gharama yoyote. Faida si tu kwamba wataweza kujitegemea na kutusaidia pale tutakapokuwa tumezeeka, lakini pia watatufanya tuwe na amani na maisha yetu ya kila siku.

Leave A Reply