Unamwachisha kazi mkeo, humpi mahitaji, afanyeje?

loversHABARI zenu wapenzi wasomaji wa safu hii maridhawa ya Sindano za Mahaba. Bila shaka ni wazima, mnaendelea vema na harakati zenu tukielekea kwenye uchaguzi mkuu. Naamini hamtaniangusha, mtapiga kura wote mliojiandikisha ili kuwachagua wale mnaoona wanafaa kuliongoza taifa hili. Na mimi naamini sitawaangusha.

Mimi mwenzenu nina kikatio changu, natarajia kumpigia kura yule ninayeona anafaa kuliongoza taifa hili kwa nafasi ya urais, hivyo ni bora wakati mwingine nikawakumbusha hili kwani ni la kitaifa zaidi.

Kabla sijawachosha sana leo mada yangu itazungumzia wanaume wanaowaachisha kazi wake zao na kuwafuga ndani kama kuku lakini wakashindwa kuwatimizia mahitaji yao.

NDIYO VILIO VYA WANAWAKE

Vilio vya wanawake viko vingi kwa suala hili na ndiyo maana migogoro ndani ya nyumba inakuwa mingi bila kupata ufumbuzi kwani wanawake wengi wameachishwa kazi ukimuuliza kwa nini anakwambia mume hapendi.

Nina kisa cha mama mmoja ambaye anasikitisha kwa kweli na mpaka amenitumia ujumbe huu anasema ndoa yake iko hatarini kuvunjika kwa sababu ameikinai. Hebu msikilize msomaji wangu nawe utajifunza kitu, kama ni mwanaume kwa kupitia mafunzo haya hutamuachisha kazi mkeo na kama utakuwa na mpango huo utahakikisha unampatia mahitaji muhimu.

MSIKIE HAPA

“Mimi ni mke wa mtu ambaye nimejaliwa kupata mtoto mmoja. Kabla ya kukutana na mume wangu nilikuwa nafanya kazi ya mamalishe ambayo ilinisaidia nikafanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kununua kiwanja. Mume wangu alikuwa akiishi Dar, mimi naishi Kibaha na huko ndiko nilikuwa nafanyia kazi zangu.

Baada ya mume kunioa, alinileta Dar na kunitaka niachane na kazi ya mama lishe. Nilimkubalia kwa sababu nampenda na tayari alishanioa. Maisha yalikwenda vizuri ndani ya nyumba mpaka nikajaliwa kupata huyo mtoto.

Kilichosababisha kueleza hili kwako ni mume wangu kubadilika sana. Hanitimizii chochote nyumbani, hataki nifanye kazi yoyote kwani baada ya kuniachisha umama lishe niliamua kusuka maana nina kipaji hicho lakini huwezi amini na hiyo akanikataza. Akitokea mtu anataka niende kwake nikamsuke anakuja juu na kuniambia hataki.

Kazi ya kusuka ukimfuata mtu ndiyo unalipwa pesa nyingi tofauti na mtu kukufuata nyumbani kwako. Mbaya zaidi mwanaume huyu si kama hana pesa, bali anaendekeza familia ya kwao kwani mara nyingi amekuwa akiniagiza niwatumie pesa ndugu zake.

Utasikia akiniambia kuwa mke wangu leo dada yangu ana shida na kitu f’lani kamtumie hii pesa, nakwenda huku nina maumivu. Si kama sipendi aisaidie familia yake la hasha, lakini na mimi mkewe anitimizie basi ukizingatia yeye ndiye sababu ya mimi kuwa tegemezi. Ukweli ndoa yangu naona kama inataka kunishinda kwani najipanga kwenda kutafuta kazi kama akinizuia tena naona ni bora niachane naye,” alisema mama huyo.

Kwa maneno ya mama huyo hakika utakuwa umebaini kitu f’lani kwani wanaume wa aina hii wapo wengi na wake zao hawana pa kusemea.

UNAWAZA NINI KUHUSU HILI?

Inapofikia hatua unashindwa kumtimizia mkeo halafu akaamua kutoka wakati wewe upo kazini yeye anafanya mambo yake tena ndani ya nyumba yako, utafanya nini wewe ukigundua?

MSIWAJARIBU

Wanaume mlioko kwenye ndoa nawasihi wakati mwingine msiwape majaribu wake zenu kwa sababu akifanya usaliti kwa njia ya kujitafutia pesa za mahitaji zaidi mtaumia wote, unaweza usiumie kwa sasa lakini ukaja kuumia baadaye na ukajuta kwa nini ulimsababishia majaribu.

Kama amekubali kuacha kazi yake kwa kukuamini mume wake kwa nini usimtimizie? Na kama mahitaji kwa kipato chako hayatoshelezi kwa nini usimuachie kazi yake ambayo ingewasaidia kuongeza kipato? Mnakosea sana wanaume. Nawasihi mliokosea katika hili basi mjisahihishe pale mlipoteleza kwa kunisoma.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine bomba. Mimi naitwa Bi. Chau.


Loading...

Toa comment