The House of Favourite Newspapers

Unanyonyesha halafu huogi, mume atachepuka

0

NI Jumanne tena ambapo naamini kabisa kwamba, wapenzi wasomaji wangu wa safu hii ya elimu ya mapenzi na maisha tuko pamoja tena kufuatilia nini nimewaletea leo.

Mada yangu ya wiki iliyopita ilipokelewa kwa mikono tofauti. Ni ile mada iliyosema; zijue faida za kiafya za kufanya mapenzi. Wengine walisema hakuna kitu kama hicho, wengine walisema wanashukuru kwa elimu.

Wapo waliokwenda mbali zaidi kwa kunirushia maandiko wakisema kukutana kimwili mara nyingi kwenye maandiko kumekatazwa japokuwa wasomaji hawa hawakuweza kuniambia ni andiko gani na linapatikana kwenye kitabu gani cha dini.

Leo mada yangu inasema; unanyonyesha halafu huogi, mume atachepuka. Ni mada pana kidogo kwa walio kwenye ndoa lakini hata wale wanaotarajia, vyema wakijifunza kabisa.

USAFI WA MWILI
Wataalam wanasema kuwa, mwanamke asipooga kwa siku mbili anasumbua pua za mwenza wake kuliko mwanaume asipofanya hivyo.

Wanaume walio wengi, wanaporudi majumbani na kukuta wake zao wakiwa katika mazingira ya uchafu, hususan wa mwili hukereka licha ya wengi wao kutosema.

WANAONYONYESHA, DALILI ZA MAGONJWA
Baadhi ya wanawake wanapofikia hatua ya kupata mtoto na kuanza kunyonyesha, baaasi! Atajiachia na kuwa tofauti na zamani. Kama alivaa gauni huku ananyonyesha, pindo za gauni nazo zitagusana na maziwa ya mama mpaka kukakamaa.
Kwanza hali hiyo inachangia kumpa magonjwa mtoto anayenyonya achilia mbali kuwa kero kwa mumewe.

Maziwa yanapogandiana kwenye nguo, baada ya muda huwa mgando na hivyo ni rahisi kupitia maziwa hayo, mtoto kupata magonjwa kama ya kuharisha.Lakini pia wewe mwenyewe, sehemu hiyo yenye maziwa yaliyoganda, nzi wanaweza kutua na kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Lakini kwa upande wa wanaume, kulala na mkewe (kwa wale wanaolala na wake zao kitanda kimoja wakiwa wananyonyesha), hupata tabu ya harufu yenye mchanganyiko wa maziwa yaliyomwagikia kwenye gauni na yale yanayonyonywa na mtoto kwa wakati huo, hususan kama mwanamke atakuwa hajaoga! Wapo!!

MWANAMKE ANAVYOTAKIWA KUWA
Siku zote, mwanamke ndani ya nyumba anatakiwa kuwa msafi wa hali ya juu. Kama ni mama wa nyumbani, mumeo anaporudi kutoka kazini anatakiwa kukukuta katika hali ambayo, kama hajakuzoea afikirie ulikuwa unajiandaa kwa mtoko kumbe sivyo, kujipenda.

Mwanamke ukishaamka na kuandaa mazingira mazuri ya mtoto au mumewe kuondoka kwenda kutafuta, ni vizuri ukaingia bafuni kuoga na kujipodoa kwa kuvaa nguo safi kama za kutokea.

Pia, ni vizuri ukajipamba kwa kuvaa hereni, bangili, cheni na hata kidani kama unacho. Hata kama kuna ghafla imetokea, mumeo akirudi akiwa na wageni wake, ukutwe katika mazingira ya mvuto ili kumjengea heshima mume wako.

Na hata ikifika jioni, ni vizuri mwanamke ukaoga tena na kubadili nguo na kujiopodoa kwa kiwango cha juu. Si lazima ukajipodolee saluni, nyumbani inatosha kwa kuwa huendi kwenye harusi.

KUKWEPA KUCHEPUKIWA
Kama mumeo atazoea kurudi na kukukuta ukiwa katika hali ya uchafuuchafu, ni rahisi sana kukinai na wewe hivyo kujikuta akiamua kuchepuka si kwa sababu ya kufuata mahaba mazito bali mwanamke msafi kwani anakuwa na mvuto zaidi.

Wapo wanawake mitaani ukiwaona wanakwenda duka la jirani tu unaweza kusema anakwenda kupanda daladala kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kumbe ni usafi tu na mvuto wa kila siku kwa lengo la kudumisha ndoa yake isichepukiwe.

Leave A Reply