The House of Favourite Newspapers

Unapoachwa Ni Muda Muafaka wa Kufikia Malengo -2

couples

Mpenzi msomaji sote tuseme asante kwa Mwenyezi Mungu kwa kila jambo analotutendea katika maisha yetu ya kila siku. Pasi na shaka una sababu milioni moja za kumshukuru kwa kuwa ametunuku nafasi ya kusoma mada hii kwa mara nyingine tena.

Wiki iliyopita ninaamini ulibahatika kusoma sehemu ya kwanza ya mada hii inayozungumzia kutumia nafasi ya kuachwa na mpenzi wako kwa ajili ya kutengeneza mafanikio au kufikia malengo yako.

Siku zote matatizo ndiyo huzalisha mafanikio, huzalisha biashara, huzalisha kazi, huzalisha ajira na mengine mengi. Hivyo kama na wewe ni miongoni mwa wengi walio kwenye matatizo ya kimapenzi na mwenza wako, kwa nini usitumie nafasi hiyo kufanikisha malengo yako?

Ni kweli, kuachwa ni jambo baya sana, linauma, linakondesha, wengine huharibikiwa kabisa na maisha kwa sababu tu wameachwa au wameachika kwa wapenzi wao.

Tumia nafasi ya kuachwa kuhakikisha unafikia malengo yako. Nasema hivyo kwa sababu ni dhahiri una uchungu wa hali ya juu unaotokana na kuachwa na umpendaye, basi badilisha uchungu huo kukutoa kwenye mapenzi na kukupeleka katika kutimiza ndoto zako.

Tamani kujinasua pale ulipo. Inawezekana ndiyo sababu ya mpenzi wako kukuacha. Pia inawezekana wewe si chaguo lake sahihi, basi pigana upate fedha ili uwe sahihi japokuwa inawezekana isiwe kwake tena.

Si umeachwa? Kwanza kubali kuwa kuachwa ni changamoto kisha tumia muda huo kutafakari, jiulize kwa nini umeachwa? Je, umechwa kwa sababu huna fedha, elimu, kazi nzuri au labda wewe siyo chaguo lake?

Baada ya kujiuliza maswali hayo na majibu utakayoyapata, basi weka nguvu nyingi na hasira za kuachwa katika kutimiza malengo yako, hakika utafanikiwa.

Fahamu kwamba, watu wengi ambao wamefanikiwa ni wale waliopitia mambo magumu kwenye maisha yao, waliokutana na misukosuko ya hapa na pale lakini mwisho wa siku wamepigana kwa kuugeuza udhaifu kuwa mafanikio.

Nataka kukuambia kuwa, kuachwa haimaanishi labda wewe ni mbaya ndiyo maana umeachwa. Wakati mwingine unaachwa kwa ajili ya kusudi f’lani, pengine ili uweze kufikia malengo f’lani.

Kwa mfano, inawezekana ukaachwa na mpenzi wako wa awali ili usononeke kisha ukutane na mwingine kwenye usafiri wa basi ambaye atakupa faraja ya maisha yako na pengine ndiye mwandani wako ambaye ulipangiwa na Mungu ila hukumjua na hukujua kuwa utakutana naye wapi.

Unapoachwa, ndicho kipindi pekee cha kufanya mambo ya maendeleo kwani unakuwa umeumizwa kwa hiyo ukitumia maumivu hayo kufanya kazi kwa bidii ili siku moja aliyekuacha akuheshimu, inapendeza sana, kwani unakuwa unafanya kazi kwa msukumo wa hali ya juu.

Ila usifanye kazi kwa ajili ya kuja kumringishia, la hasha! Fanya kazi huku akili yako ukiiambia ikomae uone kama itashindwa kumilika pikipiki, gari au nyumba? Uoneka kama itashindwa kuwasomesha watoto wako, uone kama itashindwa kulipa kodi ya pango na mambo mengine?

Kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.

Kwa maoni zaidi jiunge na M&U WhatsApp kwa Na. 0657486745, Insta:mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu kwenye Facebook; https://www.facebook.com/Mimi-na-Uhusiano-1584071311866497/

halotel-strip-1

Comments are closed.