UNATAKA KUANZISHA UHUSIANO MPYA? SOMA HAPA

 ULIMWENGU wa vijana wa sasa kumpata mwenza sahihi wa kufanya naye maisha ni nadra sana. Wengi wamegeuza suala la uhusiano kama vile mchezo wa mpira wa miguu au siti ya basi. Leo mtu utamuona yupo na huyu, kesho amehamia kwa mwingine.  

 

Uaminifu umepungua, mapenzi ya dhati yametoweka. Watu wanaishi kiujanjaujanja tu. Mtu ana mpenzi wake lakini ukikutana naye ni kama hana. Ni rahisi tu kumrubuni na akaingia kwenye uhusiano mpya, ule wa kwanza akaupa mapumziko au akaachana nao kabisa. Ndugu zangu hili ni tatizo kubwa. Wakati mwingine unaweza kujikuta hutamani kuanzisha uhusiano kwa sababu kila unayeingia naye kwenye uhusiano unajikuta mmeachana ndani ya muda mfupi. Matokeo yake sasa kila mtu anaishi kwa hofu tu katika uhusiano.

 

Watu wamekuwa waongo. Tamaa zimekuwa mbele. Wanawake wanataka wanaume wenye fedha, wanaume nao pia wanazo tamaa katika suala la fedha na uzuri wa sura. Kinachoendelea sasa ni usanii tu, mtu anajifanya yupo na wewe kumbe ana mtu mwingine. Mapenzi ya kweli yamepungua. Mtu ubahatishe kweli kumpata mtu sahihi kati matapeli wa mapenzi waliojaa kila kona. Baadhi yao hujifanya ni wema lakini unapoanzisha nao uhusiano, unakuja kugundua kwamba si wema hata kidogo.

 

Ni vyema basi kila mtu akawa makini, akajua nini cha kufanya kabla ya kuanzisha uhusiano mpya maana vinginevyo unaweza kujikuta umepoteza muda kwa kuhangaika na wapenzi tofauti na mwisho wa siku ukaambulia matatizo mbalimbali yakiwemo magonjwa.

 

UTULIVU WA MOYO

Kwa kawaida mtu anapokuwa hana mpenzi, macho yanakuwa juujuu. Kila atakayekuja, atakayemuona barabarani anafikiri anaweza  kuwa mpenzi wake. Hapo ndipo tunapokosea. Si kila unayemuona anafaa kuwa mwenzi wako. Unapaswa kumfahamu vizuri, kumjua angalau kidogo historia yake kabla ya kuanzisha naye uhusiano. Kama ndiyo kwanza umekutana naye, zungumza naye kwa maana ya kubadilishana naye mawasiliano na kisha uanze kumuweka karibu kwa maana ya urafiki.

 

Kwenye kipindi hicho cha urafiki, utamjua mtu huyo ni sahihi au la. Utagundua namna anavyojiheshimu, anavyoishi na hata marafiki alionao. Kwa kufanya hivyo itakusaidia wewe kufanya maamuzi kutokana na jinsi ulivyomchunguza kama anafaa au hafai.

 

Tuliza moyo wako, jifanye kama huhitaji kuwa na mtu lakini kumbe unahitaji. Usikurupuke tu msome mtu kwanza ana tabia za aina gani ndipo uamue. Kuna tabia unaweza kuziona katika hatua za awali na ukizipima kwenye mizani ya ubongo wako zinavumilika hata kama ni mbaya, jipe muda. Kuwa naye na unaweza kumbadili.

JITATHIMINI

Hili nalo ni la msingi, wengi hujisahau na kuamini kwamba wapo sahihi. Yawezekana nawe si mtu sahihi hivyo ni vizuri ukaipinga nafsi yako na kukubali kujifunza. Kama hujatulia, macho yako bado yapo juujuu na huridhiki basi jirekebishe.

 

Kama una tabia mbaya mathalan mzinzi kupitiliza, mkorofi kupita kiasi basi una kila sababu ya kujirekebisha. Kama unataka kuwa na mtu sahihi, ni vyema na wewe ukawa mtu sahihi kwanza. Jichunguze kwanza wapi unakosea, nini kinakufanya usiishi na wenza? Ukishajifanyia tathimini na kugundua makosa yako basi utakuwa na uwanja mpana sasa wa kuingia kwenye uhusiano. Jifunze hata kwa kusoma majarida mbalimbali kama hivi magazeti, na wanasaikolojia  mbalimbali utajua wapi unakosea.

 

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale

Loading...

Toa comment