The House of Favourite Newspapers

Unatamani uhusiano wa wenzio uwe wako?JIFUNZE!

 KUTAMANI kitu cha mwingine kwa mtazamo chanya yawezekana ikawa ni jambo jema katika maisha. Yaani ukaona mwenzako ana maendeleo fulani, mfano ana nyumba na wewe ukapambana kuhakikisha unapata nyumba.

Yawezekana ukaona mwenzako ana gari, ukajifunza mbinu alizopitia nawe ukazipita na kuhakikisha nawe unamiliki gari. Huo tunauita wivu wa maendeleo. Unamuona mwenzako ana kitu humuwekei chuki. Ikiwezekana unamuuliza, anakufundisha mbinu alizopitia hadi kufikia hatua aliyonayo. Kama ana roho nzuri, atakueleza nawe utafuata njia zake ili uweze kufikia mafanikio aliyonayo.

Akili inawaza. Inalinganisha hatua iliyonayo kwa kumtazama mtu mwingine. Inajipa jibu kwamba kuna kitu kwake hakipo sawa, kimepungua. Mathalan, mwenzake ana gari zuri ambalo akililinganisha na la kwake, anaona la kwake si zuri. Anatamani la mwenzake.

Hayo ndiyo maisha ya wanadamu. Wengi wetu tunatamani mambo mazuri. Tunatamani vitu vizuri. Tukiona vitu vizuri kwa wengine, tunavitamani viwe vyetu. Tunatofautiana tu katika matamanio. Kuna wale wanaotamani kwa mtazamo hasi. Na kuna wale ambao tunatazama kwa mtazamo chanya.

Rafiki yangu, tunaruhusiwa kutamani vitu vya wenzetu kwa kujilinganisha na tulipo katika masuala mbalimbali ya maendeleo lakini si suala la uhusiano. Uhusiano una kanuni zake. Bahati mbaya sana hizo kanuni hazifanani, kila mtu ana zake.

Unaweza kuona kanuni za mwenzako zinakufurahisha, ukaamua kuzitumia lakini zisifae kwako. Uhusiano unapaswa kuwa wako na mpenzi wako. Si vyema sana kujilinganisha na uhusiano wa mtu mwingine. Watu wengi sana wamekuwa wakifanya makosa katika uhusiano. Wanajilinganisha na wengine. Mathalan, mwanaume anatamani namna ambavyo pengine rafiki yake wa kike anavyomjali mpenzi wake.

Anatamani jinsi anavyomheshimu. Anatamani jinsi anavyomwonesha mahaba hata mbele za watu. Hana aibu. Popote pale anakuwa tayari kumbusu, kumuonesha kwamba hakuna mwingine zaidi yake. Yani ni mahaba motomoto.

Upande wa pili, mwenzangu na mimi mwanamke wake anakuwa mkali. Haoneshi ‘makeke’ kama ambayo mwanaume wake anayaona kwa rafiki yake. Anaumia kweli. Anatamani uhusiano wa mwenzake. Akijilinganisha na wa kwake, anajiona kama yuko nyuma. Anajiona kama hayupo na mtu sahihi. Anakinukisha kwa mpenzi wake kwa kumhoji kwa nini yeye hamfanyii kama rafiki yake anavyomfanyia mwenzi wake. Matokeo yake wanajikuta wakiishi maisha ya ugomvi.

JIFUNZE HAPA

Kujilinganisha katika uhusiano kama nilivyoeleza awali ni kosa. Hupaswi kujilinganisha hata siku moja katika suala zima la uhusiano. Ishini ninyi kama ninyi. Penzi lenu linapaswa kuwa la kwenu. Msilinganishe na la watu wengine. Yawezekana mkaona wenzenu wanaishi vizuri au penzi lao ni zuri kumbe nao wana changamoto kubwa ambayo ninyi hamuioni. Wanaifanya siri lakini machoni wanawaonesha ‘mapichapicha’ ambayo yanawavutia.

Lakini inawezekana wakati ninyi mnatamani uhusiano wao nao wanavutiwa zaidi na uhusiano wenu ninyi hamjui. Njia bora kabisa ya kuishi vizuri katika uhusiano ni kutojilinganisha uhusiano wa watu wengine. Kama mnaona kuna kitu hakipo sawa kwenu, tumieni lugha rafiki kujirekebisha.

Kama lengo ni kupiga hatua za uhusiano wenu, mfano labda mnataka kufikia hatua ya uchumba na baadaye ndoa, zungumzeni kwa lugha rafiki. Elekezaneni kwa kuzingatia uwezo wenu. Msilazimishe mambo. Linalowezekana leo, lifanyeni. Linalowezekana kesho basi lifanyeni kesho.

CHANGAMOTO HAZIFANANI

Kila mtu ana changamoto zake kwenye uhusiano. Wengine wanaonekana nje wanacheka kumbe moyoni wanalia. Huwezi kuwajua. Boresha uhusiano wako. Kuwa na msimamo. Shikilia mahali ulipo, hata kama kuna upungufu unaouona, zungumzeni. Tatueni changamoto, mtafikia kilele cha mafanikio mkiwa pamoja. Nicheki Facebook, Twitter & Instagram kwa jina la Erick Evarist

Comments are closed.