The House of Favourite Newspapers

Unateswa na Mapenzi au Ndoto Zako?

0

GABRIEL NG’OSHA | IJUMAA WIKIENDA | XX  Love

KWANZA nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake wa kuniruhusu kuendelea kutumia pumzi yake. Nikukaribishe tena msomaji wa safu hii uipendayo ya XXLove inayokupa elimu ya uhusiano na maisha ya kila siku.

Mada ya leo inazungumzia namna ambavyo watu wamegawanyika katika kuteswa. Kuna watu wanateswa na umaskini wao, wengine utajiri, kuna watu wanateswa na kutotimiza ndoto zao huku wengine wakiteswa na mapenzi.

Hapo ndipo utakapoamini kuwa dunia ina mambo mengi sana ya kushangaza, kufurahisha, kuhuzunisha, kusikitisha, kufunza na kuonya.

Ukweli ni kwamba baadhi ya watu huteswa na mambo mengi mno kila siku. Inawezekana anateswa na mapenzi au anateseka kwa kushindwa au kutokufikia ndoto zake.

Wewe umewahi kujiuliza ni kipi kinachokutesa katika maisha yako? Je, ni mapenzi au kutimiza ndoto zako?

Mateso yote huwa ni mabaya na hakuna mwenye mateso mazuri au ya ahueni kati ya anayeteswa na mapenzi na yule anayeteswa na ndoto au maono aliyonayo.

Kila mtu anatamani kupata mwenza au mpenzi anayempenda na mwenye kuishi naye siku zote, tena kuishi kwa upendo, furaha na raha tele. Vivyo hivyo kila mtu anatamani kufikia ndoto au maono aliyonayo katika maisha yake.

Lakini kwa kuwa hakuna kitu au kazi rahisi ndiyo maana kila kukicha watu wanapambana kuhakikisha wanafikia malengo, lakini bado njiani wanakutana na changamoto nyingi sana, zikiwemo za kukatisha tamaa, kuliza, kuchekesha na kadhalika.

Hebu tazama, wakati wewe unateseka na kunyanyasika kwa sababu ya mateso ya mkeo kuwa mapepe au mumeo kuwa mzinzi, jirani yako yeye anateseka na ugumu wa maisha alionao, anatamani atoke hapo alipo ili afikie ndoto zake.

Anatamani awe na uwezo wa kubadilisha mboga saba, lakini hajapata, anatamani apate kipato cha kuweza kumpeleka mwanaye shule nzuri, lakini imeshindikana.

Usiku kucha anaomba, anapigana kwa kila namna kufikia ndoto zake wakati huo wewe kila kukicha unazunguka kwa waganga, mara Sumbawanga, Kigoma, Mbeya na kwingineko kwa sababu ya mapenzi.

Jiulize sana, ni kwa nini unateseka kwa sababu ya mapenzi? Kama huteswi na mapenzi, jiulize ni kwa nini unateseka kwa sababu ya maono, ndoto au malengo uliyonayo? Kama huteswi na vyote viwili, yaani NDOTO AU MAPENZI basi jiulize unateswa na nini?

Mpenzi msomaji, jichunguze kwa makini katika maisha yako kisha nitumie maoni yako kuhusu kile kinachokutesa kisha maoni hayo nitayachapisha kwenye kona hii ili kupanua mjadala na kupata suluhu ya kile kinachokutesa.

Kwa maoni na ushauri tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta: mimi_ na_uhusiano au unaweza kujiunga na M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.

Leave A Reply