UNAUHAKIKA ANAKUPENDA KWA DHATI

ALHAMISI nyingine imewadia ambapo tumekutana katika uwanja huu, ambao tunajifunza mambo mbalimbali kuhusu uhusiano. Naamini ukurasa huu unakusaidia kukuza ufahamu kwenye mambo ya malavidavi na kila siku kuna vitu unajifunza.  Marafiki zangu, hakuna jambo baya katika uhusiano kama kutokuitambua nafasi yako. Hapa namaanisha kwamba, upo na mwenzi wako ambaye ana dalili zote za nje zinazoonyesha kwamba anakupenda, lakini kilichopo ndani yake unakuwa haukifahamu!

Wengi huwa hawana muda wa kufikiria juu ya hilo, lakini napenda kukufahamisha kwamba, lipo penzi la nje, ambalo mwenzi wako anaweza kutumia kila anachoweza kukufanya uamini kuwa anakupenda sana lakini ndani ya moyo wake kukawa na vitu vingine tofauti.

Hii ni mada ambayo itakuwezesha wewe kijana (mvulana/msichana) kufahamu nia ya ndani ya mwenzi wako. Kabla sijaanza kuwapa vipengele muhimu zaidi, tuanze kwa kuangalia tofauti kati ya penzi la ndani na lile la nje.

PENZI LA MACHONI

Hili halipo moyoni, kwa saabu hiyo basi linakuwa la usanii kupitiliza. Anakuwa mtu wa ahadi sana, anaweza kukufanyia mambo makubwa sana kwa nyakati tofauti, kuhakikisha unamuona kama mtu muhimu ambaye maisha anayaweza!

Anaweza kukupiga mabusu mfululizo mkiwa faragha tu, hawezi kufanya hivyo mbele za watu. Mwoga hata wa kukushika mkono. Hawezi kukufanyia mambo ya kimahaba mnapokuwa mmetoka pamoja. Mwingi wa visingizio hata kama mmepanga kutoka kwa ajili ya jambo muhimu. Kimsingi kwa kuwa penzi lake ni la mashaka, siyo la kudumu na halipo moyoni, huwa kama anakutega, akisubiri ukosee kidogo ili muachane. Hana penzi la kweli kwako.

PENZI LA MOYONI

Hili ni penzi la dhati, ni  rahisi kulijua, lakini pia ni vigumu sana kulifahamu! Unatakiwa kuwa makini sana na mwenzi wa aina hii ili uweze kujua msimamo wake. Kwanza kabisa anazungumzia anavyokupenda, siyo mkali wa stori za ngono na mara nyingi amekuwa akizungumzia zaidi maisha na wewe kuliko kuwaza mambo yasiyofaa.

Penzi lake ni la uwazi na hujisikia furaha kukushika mkono na hata kukuzawadia busu mwanana mbele za watu. Anafanya haya kwa sababu anatetea kile kilicho moyoni mwako. Anatetea penzi lake la kweli. Zipo dalili 10 muhimu zaidi, ambazo akiwa nazo mwenzi wako ujue hana penzi la moyoni, badala yake penzi lake ni la machoni. Dalili hizo ni kwa upande wa wanaume na wanawake.

Leo tunaanza na upande wa wanaume kwanza, kabla ya kugeukia upande wa wanawake. Hebu zisome dalili hizo uingize kitu kipya kichwani mwako.

(1) MSEMAJI TU…

Mwanaume ambaye ana nia ya kukutumia na kukuacha, unaweza kupima hata maneno yake, mara zote amekuwa mtu wa maneno mengi ambayo hayatekelezeki! Ahadi zake zimekuwa nyingi ambazo baadaye unagundua kwamba ni hewa.

Huyu hana mapenzi ya kweli na nia yake ni kukuchezea na kukuacha na ndiyo maana anaweza kuropoka hata mambo ambayo anajua wazi kwamba hana uwezo wa kuyatekeleza.

Mchunguze zaidi mwanaume wa aina hii, kwani ni moja kati ya dalili 10 za msingi za mwanaume ambaye hafikirii sana kuwa na wewe hapo baadaye.

(2) HAZUNGUMZII MAISHA YA BAADAYE

Hataki kabisa kuzungumzia juu ya mustabali wa maisha yenu ya baadaye. Hataki mijadala ya mambo ya ndoa, ukianzisha anakukatisha. Hata mijadala hiyo inapotokea kwenye runinga au redio mkiwa naye, atabadilisha chaneli ili asisikilize au kuona.

Huyu bado yupo yupo, anapendezwa na uzuri na mwonekano wako ambao kwake ni pambo la muda tu, na siyo la kudumu kama ambavyo wewe unawaza. Hana mpango na wewe.

(3) ANAPENDA PENZI LA SIRI

Hataki uhusiano wenu ujulikane na ndugu zake/zako wa karibu. Hata inapotokea akalazimika kufanya hivyo, hutoa visingizio vingi sana.

Anaogopa kukutambulisha kwa sababu anafahamu wazi kwamba hana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye badala yake anakutumia tu!

Mada hii itaendelea wiki ijayo, USIKOSE!  Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, Maisha na Ndoa anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

 

Loading...

Toa comment