UNAVYOWEZA KUSALITIWA KWA KUTOMSIFIA MKE WAKO!

KUNA dada mmoja ameolewa na anafanya kazi benki. Dada huyu kila akitoka hujitahidi kuvaa vizuri lakini mume wake hajawahi kumwambia amependeza.  Mwanamke huyo kitoka nyumbani kwake kwenda kupanda gari kutuoni hupita sehemu ambayo hukaa vijana na kupiga stori. Kuna kijana ambaye kila siku yule dada akipita humsifia kuwa kapendeza na ana umbo zuri. Basi mwanamke huyo hujisikia raha sana na ikafika wakati akawa anajisikia kumpenda.

Unajua kwa nini? Ni kwamba, wanawake wengi sana wanapenda kusifiwa na ndiyo maana mwanamke yoyote akitembea umbali mrefu, akawa anapishana na wanaume lakini hakuna anayemsalimia wala kumwambia amependeza hujisikia vibaya sana. Labda nikuulize wewe msomaji wangu hasa wewe mwanaume, yapo mengi mazuri ambayo huenda mpenzi wako anakufanyia, je unachukua dakika chache kumsifia na kumshukuru?

Naamini Mungu amekujaalia kuwa na mpenzi mzuri, unaona hatari gani kumsifia kwa hilo mpaka wanaume wengine wafanye hivyo? Unadhani unatumia nguvu gani kumsifia mpenzi wako kutokana na mahaba mazito anayokupata? Kwa taarifa yako kumsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia kuna faida nyingi sana lakini kwa leo nitagusia chache.

Kwanza kunaongeza mapenzi. Mke anaposifiwa kuwa anayajua mahaba hata kama si kwa kiwango kikubwa, anafarijika sana. Anajihisi aliyekamilika kwa kufikia hatua ya kufanya mambo yakamridhisha mpenzi wake na kwa mazingira hayo anaamini huwezi kumsaliti. Hisia hizo zitamfanya azidi kukupenda.

Pia unapomsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia, unamfanya aongeze kasi ya kukufanyia ili nawe uzidi kumpenda. Kwa mfano, unapokutana na mpenzi wako kisha ukamwambia ‘umependeza kweli mpenzi wangu, nazidi kukupenda kwa unavyovaa’.

Mtu anayeambiwa maneno haya atajitahidi sana siku zote aonekane nadhifu na wa kuvutia kwa mpenzi wake akijua kwamba, akivaa ili mradi kuvaa, hatamfurahisha mpenzi wake. Kwa maana hiyo kumsifia mpenzi wako kunamfanya azidi kuwa bora.

Ukitaka kujua ukweli wa hili, fuatilia na utabaini kuwa, wanawake wanapokatiza mitaa na kukutana na wanaume wakasifiwa kwa uzuri au kwa mavazi, hufarijika sana. Kwa taarifa yako sasa ni kwamba, mwanaume wa nje akijenga tabia ya kumsifia mkeo kila mara, kuna uwezekano mkubwa sana wa kukumegea penzi lako. Nasema hivyo kwa kuwa, wapo wanaume ambao wanatumia mwanya huo.

Mke ameishi na wewe kwa muda mrefu lakini hujawahi kumsifia kwa namna yoyote, akitokea mwanaume wa nje akawa anamsifia kila wakati, anaweza kujikutana analainika na hata akitokewa uwezekano wa kuchomoa ni mdogo sana. Ninachotaka kusisitiza leo ni kwamba, tusifiane pale inapobidi huku tukijua kuwa kwa kufanya hivyo tutapata faida. Tusiwe na tabia ya kuchukulia poa kila tunachofanyiwa na wapenzi wetu.

Kama kavaa, kapendeza msifie. Angalizo katika hili la mavazi ni kwamba, kuvaa kwa kiyaanika maungo yake au kubana mwili siyo kupendeza. Ukimsifia mpenzi wako akiwa kavaa nusu uchi, watu watakushangaa. Kwa leo naomba niishie hapo

 

Amran Kaima

Loading...

Toa comment