Unavyoweza kushindwa kwa sababu ya kuogopa kushindwa
Katika makala zangu nilizowahi kuandika huko nyuma, niliwahi kusema kuwa, mafanikio ni kwa kila mtu. Yeyote anayeweka dhamira ya dhati kabisa kwamba anataka kuwa mtu f’lani katika jamii yake, mara nyingi hufikia malengo.
Lakini kumbuka mafanikio hayaji kwa haraka, yanahitaji mtu mwenye subira, ambaye yuko tayari kujaribu na kushindwa, akajaribu tena akashindwa lakini asikate tamaa.
Katika hilo la kushindwa na kuendelea kupambana ndipo wengi wanapofeli. Ndiyo maana leo nimeona nizungumzie jinsi watu wengi duniani wanavyoshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kuogopa kushindwa.
Mtu anayetaka mafanikio, hatakiwi kuwa muoga wa kujaribu. Kwa mfano, wapo watu ambao wana ndoto za kufanikiwa kupitia biashara lakini ni waoga wa kukopa pesa benki na kuanzisha biashara hiyo. Eti wanaogopa kwamba wanaweza kuwekeza pesa hiyo kwenye mkopo, wakapata hasara na kushindwa kurejesha mkopo, hatimaye kujiingiza kwenye matatizo.
Lakini mtu mwenye hofu hiyo anashindwa kujua kwamba wapo wengi waliofanya hivyo, wakapata hasara mara ya kwanza, wakajaribu tena na hatimaye mambo yakawanyookea.
Au nikupe mfano mwingine, wapo watu huko mtaani ambao wanatamani kumiliki gari lakini wanaposikia kuwa f’lani mwenye gari linamsumbua na kumpuputisha pesa zake nyingi kwenye ‘sevisi’, matengenezo ya hapa na pale, wanaogopa kununua gari.
Mimi niseme tu kwamba, hutakiwi kuwa muoga katika kutimiza malengo yako. Siku zote mtu anayejiwekea malengo hatakiwi kuogopa kufeli, atachukulia kwamba kufeli katika hatua za mwanzo ni hatua za kuelekea kwenye kutimiza lengo.
Katika hilo ipo mifano ya watu wengi unaowajua ambao wana mafanikio makubwa sana lakini huwezi kuamini kwamba mwanzoni walijaribu biashara, wakapata hasara lakini hawakukata tamaa, wakajaribu tena na tena na leo hii wana mafanikio makubwa. Hao ndiyo watu wa kufuata nyayo zao.
Unajua kwa nini wengi wanashindwa kwa kuogopa kushindwa? Vipengele vifuatavyo vitakupa elimu zaidi.
Kuogopa malengo
Unavyofikiria zaidi changamoto zitakazotokea kwenye utendaji wa jambo fulani ndiyo unavyoshindwa kufikia malengo.
Zikubali changamoto bila woga kisha ndiyo utapata akili ya kukusukuma ufanye jambo kubwa. Kumbuka kila changamoto kwa mwanadamu ndiyo humfanya apige hatua. Hivi hujawahi kumsikia mtu akisema; ‘Aaa…mimi nimiliki nyumba yangu…! Hiyo ni ndoto.”
Mtu huyo ukimfuatilia utagundua anatamani kuwa na nyumba na siyo kwamba hana uwezo wa kuimiliki bali tatizo anaogopa kujiwekea lengo hilo akihisi halimhusu.
Kuogopa kufanya mambo makubwa
Wazungu wana msemo wao usemao; ‘Aim higher, failure might be success’ wakimaanisha kwamba, lenga mambo makubwa lakini hata kama utashindwa kuyafikia, utakapoishia napo ni sehemu ya mafanikio.
Watu wengi wanaogopa kuweka malengo makubwa wakihisi kufanya hivyo ni kujisumbua. Yaani wameweka akilini mwao kwamba wao ni wa vijilengo vidogo, hiyo siyo sawa na wanaowaza hivyo hawawezi kufikia yale mafanikio makubwa.
Katika kumalizia naomba nikufahamishe jambo. Kama wewe ni kati ya wale ambao wanatamani siku moja wawe na mafanikio makubwa, usiogope kujaribu. Na unapojaribu, tarajia kufaulu au kufeli. Yote mawili yanaweza kutokea.
Kwa hiyo ukifaulu, shukuru Mungu na endelea kupambana, ukifeli pia hutakiwi kuumia bali chunguza ili ujue kipi kimekuangusha.
Unaambiwa ukianguka usigalegale chini huku ukilia, nyanyuka…jipanguse kisha endelea kukimbia kuelekea kule ambako unataka kufika.