UNAVYOWEZA KUTUMIA SIMU KUBORESHA PENZI

TUNAISHI katika dunia ya utandawazi ambapo sasa karibu kila mtu anamiliki simu, hata wale wenye uwezo wa chini kabisa. Ukijaribu kufuatilia, matatizo mengi yanayotokea katika uhusiano wa kimapenzi, yanachangiwa sana na hizi simu za mkononi.  Ni rahisi sana kwa watu waliokuwa wanapendana sana kujikuta wakiwa kwenye mgogoro mkubwa kwa sababu tu meseji ya kimapenzi imeingia kwenye simu ya mwanaume na mkewe, mchumba wake au mpenzi wake ameisoma.

Vivyo hivyo, ni rahisi sana kwa wapendao waliokuwa wakizungumza lugha za bashasha na mapenzi motomoto, hali ya hewa kuchafuka kwa sababu mwanamke ametumiwa meseji au amepigiwa simu na njemba na mwanaume akainasa.

Imefika mahali, simu zinaonekana kama adui wa mapenzi, ndoa zinavunjika, uchumba unaharibika na matatizo mengine lukuki, kisa kikiwa ni simu. Yawezekana hata wewe msomaji wangu, unavyo visa kadhaa ambavyo vilikufanya ukaingia kwenye matatizo na mwenza wako kwa sababu ya simu ya mkononi.

Wakati watu wote wakiziona simu kama ‘sumu’ ya mapenzi, mimi nataka tujadiliane kuhusu upande wa pili, wa jinsi unavyoweza kuitumia simu yako vizuri na kumfanya mwenza wako azidi kukupenda na kukuona wa thamani.

JINSI ULIVYOMSEVU

Ukijaribu kuangalia wanandoa wengi jinsi walivyowasevu  wake au waume zao kwenye simu, utakuta wengi wamewaandika wanaowapenda kwa majina ya watoto wao, mfano Mama Juma, Baba Adam na kadhalika. Kama hawana watoto basi unakuta mtu amemsevu yule ampendaye kwa jina lake, jambo ambalo kitaalam humfanya mwenza ahisi kama hapewi thamani na heshima anayostahili.

Hebu badilika kuanzia leo, msevu mwenza wako kwa jina zuri la kimahaba ambalo hata mwenyewe akiliona, atajisikia amani ndani ya moyo wake. Hata kama mmeshazaa watoto, unaweza kumsevu kwa yale majina matamumatamu kama My Sweetheart, My Honey, My Lovely Wife, Sweet Dad, My Heart na kadhalika.

MPE KIPAUMBELE

Muoneshe kama yeye ni wa muhimu sana kwako, kama unatumia simu za kisasa (smart phones), unaweza kusevu picha yake kama ‘screen saver’ yako, unaweza kumuweka kama display picture (dp), WhatsApp na kwenye mitandao mingine ya kijamii. Unaweza kuona kama ni kitu kidogo, lakini ninakuhakikishia kuna faida kubwa sana kwenye uhusiano wa kimapenzi.

MPIGIE SIMU MARA KWA MARA

Jenga utaratibu wa kuwa unampigia simu mara kwa mara umpendaye hata kama mnalala kitanda kimoja. Kama yupo kazini, muulize kuhusu kazi yake, muulize amekula nini na wakati mwinginempigie tu na mwambie kwamba umem-miss.

Kama yupo nyumbani na wewe upo kazini, muulize hali yake, kama mna watoto muulize kuhusu watoto na wakati mwingine mpigie simu ukiwa huna hata sababu ya kumpigia na mwambie kwamba ulitaka kusikia sauti yake tu. Unapozungumza naye, hebu jitahidi basi kuzungumza kwa lugha laini, tofauti na unayozungumza na watu wengine, zungumza kwa upole, msikilize kwa makini.

MTUMIE MESEJI ‘TAMUTAMU’

Unaweza kukuta mtu ana mke wake nyumbani au mume wake, lakini akimtumia meseji basi ni zile za maagizo tu, lakini akiwa na ‘kamchepuko’, wanatumiana mpaka ‘makopakopa’ ya mahaba, haya ni makosa.

Yule umpendaye ndiye anayestahili hayo, mtumie meseji tamutamu ambazo hata kama alikuwa amenuna, akisoma aishie kutabasamu mwenyewe. Kuwa mbunifu, tafuta nukuu nzuri za mapenzi, wakati mwingine hata meseji za vichekesho zinaweza kukufanya ukasababisha tabasamu kwenye uso wake. Wiki ijayo nitakueleza namna unavyoweza kuzuia matatizo yanayosababishwa na simu za mkononi kwenye mapenzi. Usikose mwendelezo Ijumaa ijayo.

 


Loading...

Toa comment