UNAWEZA KUPATA MWENZA SAHIHI MITANDAONI?

DUNIA ya sasa mambo yamekuwa rahisi. Teknolojia imefanya vitu vingi ambavyo vilikuwa vinachukua mlolongo mrefu kutendeka kwa muda mfupi tu. Waswahili wanasema ni kama vile kumsukuma mlevi jinsi ambavyo mambo yamekuwa rahisi.

Kama zamani ulikuwa ni hadi umuandikie mtu barua kwa njia ya posta, aipate baada ya siku tatu au wiki, sasa hivi mambo yamekuwa rahisi kupitiliza. Yaani ni kiasi cha mtu kuchukua tu simu yake ya kiganjani, anapiga na kuzungumza na mtu aliyeko kilometa 500 au zaidi.

Ni kama dunia ipo kiganjani mwake, anaweza kumpigia si tu kwa maana ya kusikilizana sauti bali anaweza kumpigia kwa mfumo wa video call, yaani wahusika wanazungumza huku wanaonana ‘live’ bila chenga.

Uwanja huo wa teknolojia umekuwa mpana zaidi hata katika suala zima la uhusiano. Sasa hivi watu wanaonana mitandaoni, wanapendana na kuanzisha uhusiano hata bila ya kuonana. Mtu anakuwa na mpenzi ambaye hajawahi kumuona. Mapenzi yanachipuka na kukua hukohuko mtandaoni. Wanapigiana kwa video, wanatumiana jumbe za kimapenzi, wanaonana kupitia mitandao kisha baadaye wanakutana ana kwa ana. Baada ya hapo, kinachofuata ni zinaa. Hakuna maneno mengi, wanafanya yao lakini mara nyingi mapenzi ya namna hii huwa yanavunjika baada ya muda mfupi.

Kwa nini wanaachana muda mfupi? Hapa ndugu zangu ndipo penye msingi wa mada yangu ya leo, zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha watu wa aina hii waachane ambazo leo tutazijadili na kukupa picha kwamba mara nyingi uhusiano unaoanzia kwenye mitandao huwa hauna afya sana. Moja kati ya sababu hizo ni kutokana na matarajio. Unapomuona mtu kwenye mtandao halafu ukaja kuonana naye live na kukuta ni vitu viwili tofauti, hapo ndipo kunaposababisha wawili hawa wasidumu muda mrefu.

Mmoja wao huenda alikuwa na matarajio fulani kutoka kwa mwenzake lakini anasahau kwamba kuna teknolojia ya kutengeneza picha zinazopostiwa mitandaoni hivyo jinsi alivyomuona kwenye mtandao, akija kumuona live anaona kama alikosea. Kinachofuata hapo ni ile aibu tu ya kushindwa kusema bwana hunifai, anajifanya mpo pamoja lakini baada ya muda mfupi anakuacha solemba.

Hawezi kuendelea na wewe sababu hakukupenda kutoka moyoni bali aliitamani ile picha yako na si wewe. Sababu nyingine ambayo pia huchangia wawili hawa kumwagana ni pamoja na suala zima la tabia. Yawezekana kweli wewe ni aina ya mtu ambaye anadhani unamfaa lakini mwisho wa siku, tabia zako zinamshinda.

Upo uwezekano mkubwa wa kukutana na mwanamke ‘mwingi wa habari’ au mwanaume kiwembe. Wapo watu wanaojiuza kabisa kwa kuweka picha zao mitandaoni. Ukimuona kwenye mtandao unaweza kuona mke au mume si huyu kumbe mwenzako ni kiwembe wa kutupa. Ndugu zangu, japo mitandao inaweza kuwa chachu nzuri ya kukutanisha wapendanao lakini kwa kiasi kikubwa mitandao hii ina matokeo hasi hivyo ni vyema sana kuwa makini katika suala zima la kutafuta mwenza sahihi katika mitandao ya kijamii.

Ni nadra sana kupata mtu sahihi kupitia mitandao ya kijamii hivyo ni bora mtu ukutane naye live, umjue angalau mazingira anayoishi, tabia zake na hata watu wanaomzunguka. Raha ya uhusiano mzuri na imara ni ule ambao unaanza kumjua kiundani mtu unayetaka kuwa na uhusiano naye kabla ya kuzama penzini.

Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Loading...

Toa comment