The House of Favourite Newspapers

UNDANI MAFUTA YA UPAKO NI HUU

0

 

BAADA ya watu 20 kufariki dunia kwa kukanyagana mjini Moshi wakigombea kukanyaga mafuta yanayoitwa ya upako, wengi wamekuwa wakijiuliza mafuta hayo ni kitu gani na yana nguvu zipi katika imani?  Risasi Mchanganyiko limetafiti Maandiko katika Kitabu cha Biblia na kubaini undani mzito wa mafuta hayo yaliyoanza kutumika zamani kabla ya Yesu kuzaliwa.

ASILI YA MAFUTA HAYO

Kwa mujibu wa maandiko hayo, mafuta ya upako yalitumiwa na wana wa Israeli au Wayahudi na kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwatawaza watu kuwa wafalme na kwamba yalichukuliwa kuwa sehemu ya mtu kupewa nguvu za Kimungu katika kutawala.

Maandiko yafuatayo yanathibitisha KUTOKA 30:30-31 “Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.”

Maandiko yanaonesha kuwa hakuna mfalme aliyepata kutawala katika nchi ya Israel bila kupakwa mafuta haya ya upako ambayo yanafahamika pia kuwa mafuta ya kutiwa. Kwa mujibu wa maandiko mbalimbali ilikuwa ni marufuku kwa mtu ambaye si Kuhani kupakwa mafuta hayo na yule aliyefanya hivyo alilaaniwa.

Maandiko yafuatayo yanaeleza kwa kina: KUTOKA 30:33 “Yeyote atakayetengeneza mafuta kama haya, au kumpaka mtu asiyestahili kupakwa mafuta haya, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.”

MAFUTA YA UPAKO YALITENGENEZWA KWA KUTUMIA NINI?

Siku hizi kumekuwa na simulizi nyingi kuhusu vitu ambavyo vinatumika kutengenezea mafuta ya upako, lakini maandiko yameweka wazi baadhi ya vitu ambavyo vilitumika kutengenezea mafuta haya yaliyoaminika kuwa na nguvu za Kimungu.

Maandiko katika Kitabu cha KUTOKA 30: 34-35 yanasema: “Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, Utachukua vipimo vinavyolingana vya viungo vitamu vifuatavyo: Utomvu wa natafi, utomvu wa shekelethi, utomvu wa kelbena na ubani safi. Utatumia vitu hivyo kutengenezea ubani kama utengenezwavyo na fundi manukato, utiwe chumvi upate kuwa safi na mtakatifu.”

Hata hivyo, mbali na viungo hivyo vipo vingine ambavyo vimetajwa katika maandiko kuweza kuchanganywa kwenye mafuta ya upako kama manemane, sinamoni na kwamba vitu vyote hivi vilikuwa vya asili na viliweza kupatikana sehemu tofautitofauti.

Sehemu ambazo vitu hivyo vya asili viliweza kupatikana ni pamoja na maeneo ya Wakanaani, Wahiti na Wamwamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

MAFUTA HAYO RUKSA KUTUMIWA LEO?

Katika maandiko hakuna mahali ambapo mafuta ya upako yaliyotengenezwa kwa maelekezo hayo ya Mungu yamepata kupigwa marufuku kutumika katika zama hizi.

Kwa mfano maandiko katika kitabu cha MARK 6 : 7,12-13 yanaeleza jinsi wanafunzi wa Yesu walivyoyatumia mafuta kutibu wagonjwa.

“Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta; watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza. ”

MAFUTA YA KAWAIDA YANAWEZA KUWA YA UPAKO

Kutokana na uchunguzi wa mwandishi wetu katika kitabu cha Biblia, hakuna mahali ambapo wameandika mafuta ya kawaida yanaweza kuombewa na kugeuka kuwa ya upako kama ambavyo baadhi ya wahubiri hivi sasa wamekuwa wakifanya.

Uchunguzi unaonesha kuwa kutokana na mafuta ya upako ambayo ni halisi kuuzwa kwa bei mbaya, wahubiri wengi wamekuwa wakitumia mafuta ya kawaida ya kupikia kuwapaka waumini wao na mengine kukanyaga kwa madai kuwa nayo yanaweza kuondoa shida zao.

SHUHUDA ZA MAFUTA YA UPAKO

Mwandishi wetu alifanya mahojiano na baadhi ya watu ambao wamewahi kutumia mafuta ya kisasa ya upako kuondoa matatizo yao ambapo wengine walisema yanasaidia huku baadhi wakisema hayasaidii chochote.“Nimewahi kwenda kwenye ibada ya mchungaji Mwamposa (Mchungaji Boniface) nikakanyaga hayo mafuta, lakini tatizo langu halikuisha zaidi sana lilizidi,” alisema Josephine Joseph mkazi wa Sinza Mapambano.

Naye Roda Charles alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu mafuta ya upako alisema: “Yanasaidia sana, nilikuwa silali zaidi ya miezi saba, nilikuwa nikilala naona majitu yanakuja kunikaba lakini baada ya kupata mafuta ya upako, shida hiyo imekwisha kabisa.”

KUMBUKUMBU YA VIFO VYA WATU 20

Hivi karibuni watu ishirini walipoteza maisha kwa kukanyagana wakati wakigombea kukanyaga mafuta yanayoitwa ya upako katika ibada iliyoongozwa na Mwamposa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Vifo vya watu hao vilileta simanzi miongoni mwa jamii na kutaka uchunguzi wa kina ufanywe huku wengine wakitaka huduma za aina hiyo zinazoendeshwa kwa kuwapatia watu mafuta, chumvi, vitambaa na kadhalika zichunguzwe na ikiwezekana zifutwe kwa madai ya kuwa haziendani na muongozo wa mafundisho ya Kikristo.

WACHUNGAJI WENGINE NAO WAPINGA

Hivi karibuni Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship; Zachary Kakobe aliungana na Askofu Sylivester Gamanywa wa Wapo Mission International pamoja na Mchungaji Venon Fernandes wa Kanisa la Agape kupinga mafuta ya upako, maji ya upako, keki za upako, bangili za upako, vitambaa vya upako, maji na kadhalika kuwaaminisha waumini kwamba vinatibu na kuleta baraka za utajiri kwa mtu.

Viongozi hao walikwenda mbali zaidi kwa kuitaka serikali kuwakamata manabii na mitume waliodai wanawatapeli watu kwa kudai kuwa vitu hivyo vinatibu na kuleta utajiri badala ya kutumia jina la Yesu kama mwenyewe alivyoelekeza.

Walidai kutumia vitu hivyo ni ushirikina na ni kupotosha imani ya Kikristo inayofundisha kumuamini Yesu kwa kila jambo.

STORI:RICHARD MANYOTA, RISASI

Leave A Reply