Undani Maiti Yanyofolewa Jicho Kwenye Jeneza

MBEYA: DUNIA ina mambo! Ndivyo inavyoweza kusemwa baada ya maiti ya Timoth Leonard kukutwa kwenye jeneza ikiwa imenyofolewa jicho la kushoto, hali iliyozua taharuki ya aina yake kwa wakazi wa Mwakareli Wilaya ya Rungwe jijini Mbeya, Ijumaa Wikienda linakupa undani wa kisa hicho.

 

Katika mazingira ya kutatanisha, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina liliwakumba wakazi wa Mbeya ambapo.

Timoth alifikwa na umauti Oktoba 8, mwaka huu na mwili wake kupelekwa nyumbani kwa dada yake eneo la Ivumwe jijini Mbeya.

 

Ilielezwa kuwa, wakati zoezi hilo linaendelea, marehemu alikuwa na macho yote na mwili uliagwa na kupelekwa kijijini Mwakareli.

 

“Nilikuwepo wakati mwili ukiagwa eneo la Ivumwe ukiwa salama na viungo vyote, lakini nimeshangaa kupata taarifa hizi kuwa mwili wa marehemu umekutwa hauna jicho la kushoto,” alisema mmoja wa mashuhuda, Emmanuel Mwakisambwe.

 

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda, mmoja wa wanafamilia, Rachel Mwasaga alisema mwili ulilala nyumbani kwa marehemu, asubuhi ndugu walipoamka walishangazwa na marehemu kutokuwa na jicho moja ilihali alifikishwa kutoka Mbeya akiwa na viungo vyote.

 

“Wifi yangu asubuhi wakati taratibu za mazishi zikiendelea, alifunua jeneza ili kuuandaa mwili wa mumewe, lakini alitaharuki kukuta marehemu hana jicho moja,” alisema Rachel huku akibubujikwa na machozi.

 

Tukio hilo liliwashtua ambapo waliita baadhi ya wazee na wachungaji ili kujua kulikoni kwani siyo jambo la kawaida.

Wachungaji na wazee baada ya kushuhudia tukio hilo waliiomba familia kuwa na utulivu na kuwasihi zaidi wamtegemee Mungu.

 

Baada ya nasaha hizo za watumishi wa Mungu, ibada ya mazishi ilifanyika na hatimaye mwili kusitiriwa kwenye nyumba yake ya milele huku baadhi ya watu wakihusisha tukio hilo na imani za kishirikina.

Stori: Ezekiel Kamanga


Loading...

Toa comment