UNDANI WA KIGOGO WA MAFUTA ALIYETEKWA DAR

INASIKITISHA! Kigogo wa kampuni moja ya mafuta (jina tunalihifadhi kwa sababu maalum) ya jijini Dar, Dawson Buberwa Ishengoma, anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana tangu Juni 20, mwaka jana ambapo familia yake imemsaka kila kona bila mafanikio.

 

Ishengoma ambaye pia ni mfanyabiashara mwenye utajiri alidaiwa kutekwa ghafla alipokuwa akirejea nyumbani kwake, Masaki jijini Dar kwa ajili ya kupata chakula cha mchana.

MAJIRANI WANENA

Wakizungumza na Risasi Jumamosi kwa sharti la kutotajwa majina, walisema mazingira ya tukio la Ishengoma yanaonesha alitekwa kwani ingekuwa amepata tatizo la kibinadamu, basi taarifa zingewafikia polisi au hospitali.

 

“Mazingira yalikuwa ghafla sana, mtu anawasiliana na mwanaye anamueleza kuwa anarudi nyumbani hapa Masaki kula halafu ghafla tu hafiki na simu hazipatikani, unafikiri nini kitakuwa kimetokea?” Alihoji jirani mmoja.

 

Jirani mwingine alisema, Ishengoma siyo mtu mdogo kwamba hajulikani hivyo hata kama ingekuwa amepata ajali angeweza kutambulika kwa urahisi na taarifa zingefika kwa mkewe, ndugu au majirani.

“Mazingira yanaonesha kabisa alitekwa maana muda huohuo alitoka kuwasiliana na mwanaye David kwamba anarudi nyumbani kula halafu ghafla tu simu zikawa hazipatikani, tena simu zaidi ya moja,” alisema jirani huyo.

 

MWANAYE ASIMULIA

Akizungumza na mwandishi wetu, mtoto wa mfanyabiashara huyo aliyejitambulisha kwa jina la David Dawson (26) alisema yeye, mama yake na watoto wenzake sita walikuwa wakiishi Masaki jijini Dar katika nyumba ya kampuni hiyo ya mafuta, lakini baada ya tukio hilo, walihama na sasa wanaishi katika nyumba tofauti.

 

Akizungumzia siku baba yake alipotoweka, alisema ilikuwa ni Juni 20, mwaka jana ambapo baba yake alimpigia simu na kumwambia kuwa anakwenda nyumbani Masaki kwa ajili ya chakula cha mchana. “Baada ya kuniambia hivyo nilichukulia kawaida kwa kuwa baba yetu alikuwa na kawaida ya kurudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana kila siku.

 

“Cha kushangaza niliporudi nyumbani mama yangu (Stellah Ishengoma) naye aliniuliza kuhusu baba ambaye kawaida yake hurudi nyumbani mchana kwa ajili ya chakula, lakini siku hiyo alishangaa kutomuona,” alisema mtoto huyo.

 

Alisema baba yake aliyekuwa akifanya kazi na pia kuwa mwanahisa katika kampuni hiyo ya mafuta, hakuwahi kupata vitisho vyovyote kabla ya tukio hilo na hajawahi kusikia mzazi wao huyo labda ana ugomvi wowote hivyo tukio hilo limekuwa ghafla na hawaelewi hasa ni nini kimemkuta baba yao.

 

AZIDI KUSIMULIA

Akizidi kusimulia siku ya tukio, David alisema mama yake alijaribu kumtafuta kwa njia ya simu, lakini simu zake zote zikawa hazipatikani, jambo lililoanza kumpa wasiwasi. “Kufuatia hali hiyo, ilipofika majira ya usiku wasiwasi ulizidi kuongezeka, tulikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambapo tulihojiwa na kuambiwa twende ofisi ya upepelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

 

“Kesho yake nilidamkia ofisi ya kanda maalum na kukutana na mkuu wa ofisi hiyo, (RCO) Camilius Wambura ambaye nilimuelezea mkasa wa baba yetu kupotea ambapo naye alinipa ofisa mwingine anichukue maelezo ambapo yalichukuliwa katika jalada lenye namba DSM/CID/ PE84/2018. “Baada ya maelezo hayo, tuliambiwa tukae baba yetu atasakwa popote alipo, lakini tukaona kimya kinazidi na siku zinazidi kupita baba yetu hatumuoni hadi tunavyoongea na wewe,” alisema mtoto huyo wa Ishengoma.

 

APOKEA VITISHO

David alisema wakiwa kwenye harakati za kumsaka baba yao katika kila kona ya Jiji la Dar, hivi karibuni alianza kupokea simu za vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana wakimtaka kuacha kufuatilia suala hilo (alizionesha namba hizo za simu zinazomtishia).

 

Alisema mbali na yeye kupata vitisho hivyo, familia nzima ilianza kuishi kwa wasiwasi ambapo wao kama watoto walitawanyika na kila mmoja kuishi kivyake katika nyumba nyingine za baba yao huku mama yao akiamua kwenda kuishi jijini Mwanza kwa kuhofia usalama wake. “Sisi tulikuwa watoto saba pamoja na mama yetu tukaamua kuhama pale Masaki ambapo mama alikwenda kuishi Mwanza huku sisi tukihamia kwenye nyumba nyingine za baba hapahapa Dar.

 

“Tunahofia usalama wetu na hivyo tunaishi kwa kujifichaficha maana vitisho vimekuwa vingi kutoka kwa watu hao ambao wanatutaka tuache kufuatilia suala hili la baba yetu,” alisema.

 

WATANGAZA DAU NONO

Kijana huyo wa pili kuzaliwa katika familia ya Ishengoma alisema kama familia, wamekubaliana kutoa dau la shilingi milioni 400 kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa baba yao.

 

RISASI LAMSAKA WAMBURA

Kufuatia sakata hilo, mwanahabari wetu alimtafuta Kamanda Wambura juzi kwa njia ya simu azungumzie sakata hilo ambapo alipopatikana na kutajiwa sakata la kupotea kwa tajiri huyo, aliomba atajiwe jina lake vizuri na baada ya kutajiwa, alisema hawezi kulizungumzia sakata hilo na kumtaka mwandishi wetu amtafute kamanda anayehusika.

 

MURILO ASAKWA

Baada ya majibu ya kamanda huyo mwandishi wetu alimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Murilo Jumanne Murilo ambaye simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyesema kamanda huyo yuko kwenye kikao cha makamanda wote wa Kanda Maalum ya Dar. Simu hiyo ilipopigwa baadaye kujua kama kikao hicho kimemalizika iliita bila kupokelewa kila ilipopigwa.

 

KUHUSU UTAJIRI

Akimzungumzia zaidi baba yake, David alisema baba yake anamiliki magari manne; Prado mbili, Range Rover na Mazda RX8, ghorofa moja lililopo Mnazi-Mmoja na nyumba kubwa iliyopo Goba jijini Dar pamoja na mali nyingine ndogondogo.

STORI: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment